Wimbo wa Alicia na Diamond wawatoa povu mashabiki

Saturday September 19 2020

 

By Nasra Abdallah

Ikiwa ina siku moja tangu wimbo wa Alicia Keys utoke ambao amemshirikisha msanii wa Tanzania Diamond Platnumz, wadau wamekuwa na maoni tofauti huku wengine wakilalama Diamond kupewa muda mchache katika wimbo huo.

Wimbo  huo unaoenda kwa jina la Wested Energy,audio yake imeachiwa jana Septemba 18 ikiwa ni kati ya nyimbo 15 zinazopatikana katika albamu mpya ya msanii huyo kutoka pande za Marekani iliyopewa jina la ‘Alicia’.

Hamu ya kusubiri wimbo huo ilipamba moto siku moja kabla baada ya  Alicia kutangaza ujio wa albamu yake hiyo kupitia mtandao unaotoa habari zake na kueleza kumshirikisha Diamond katika wimbo mmoja.

Kama vile haitoshi alitoa orodha ya nyimbo anazopenda kuzisikiliza kwenye mtandao wa muziki wa Spotify, huku akitaja nyimbo mbili bora anazipenda kwa Diamond kuwa ni African Beauty aliomshirikisha Omarion na ule wa Nana alioimba na Mr. Falvour wa nchini Nigeria.

Hata hivyo jana baada ya kuachiwa kwa wimbo huo, baadhi ya watu wamekuwa na maoni tofauti ambapo wengine wamelalamika Diamond kupewa sekunde chache katika wimbo huo  tofauti na walivyokuwa wakiifikiria.

Mtu mmoja aliiyejitambulisha kwa jina la  Wonderboy, aliandika ‘Hongera Alicia kwa nyimbo nzuri lakini ningetamani Diamond angeiimba kiitikio kizima katika wimbo huo, lakini tunasubiri video yake.

Advertisement

Mwingine aliyejitambulisha kwa jina Nelisiwe Almas, amesema”Umenivunja moyo malaika wangu  Alicia Keys, kwani namjua Diamond ni mzuri kwenye kuimba  walau ungempa hata dakika moja , lakini sio mbaya tunasubiri remix yake.

Sass Boy  amesema’Alicia umemuibia tu Diamond mashabiki zake, hakuna chochote ulichomfanyia katika wimbo huo,”

Wakati Mutwiri Timothy, amesema’Umemmalizia bure nguvu zake Diamond, mpe tena nafasi ingine japokuwa wimbo ni mzuri.

Kutokana na povu hilo kutoka kwa raia mbalimbali, mume wa Alicia , swizzbeatz, aliwapooza kwa kumuomba Diamond awajulishe mashabiki zake kwamba  hiyo ni sehemu ndogo ya ushiriki wake katika albamu hiyo.

“Kaka yangu wa maisha tafadhali wajulishe mashabiki zako kwamba ulifanya kama ulivyoombwa katika rekodi hiyo na hii ni sehemu ndogo tu,”aliandika Swizzbeatz.

Diamond alijibu kuwa jambo hilo ni kweli na kueleza kuwa mabomu mazuri zaidi yanakuja.

Advertisement