Willian akaribia kutua Arsenal bure

Wednesday July 29 2020

 

London, England. Arsenal imetajwa kuongoza mbio za kumuwania winga wa Chelsea, Willian baada ya nyota huyo raia wa Brazil kushindwa kufikia makubaliano ya kusaini mkataba mpya na klabu yake.

Taarifa iliyotolewa na mtandao wa The Sun, imefichua kuwa mazungumzo baina ya wawakilishi wa Arsenal na wale wa mchezaji huo yako katika hatua za mwisho ambapo Willian mwenye umri wa miaka 31 atajiunga nao akiwa mchezaji huru baada ya mkataba wake na Chelsea kumalizika msimu huu.

Chelsea ilikuwa inapanga kumuongezea mkataba wa miaka mwili, nyota huyo huku yeye akihitaji uwe na urefu wa miaka mitatu jambo ambalo wameshindwa kufikia muafaka na kupelekea Willian aamue rasmi kufungasha virago na kusaka malisho mazuri zaidi.

Na klabu takribani tano zimetajwa kuingia katika vita ya kumuwania Willian lakini ni Arsenal ambayo kwa mujibu wa taarifa kutoka katika vyanzo mbalimbali vya habari zinaeleza kuwa wameshafikia muafaka na kilichobakia ni mchezaji huyo kusaini mkataba wa miaka mitatu kuichezea timu hiyo ambayo ni mpinzani wa jadi wa Chelsea.

Taarifa hizo zimekolezwa zaidi na kauli ya Wakala anayemsimamia winga huyo, Kia Joorabchan ambaye amedai kuwa kuwa timu mbili kubwa zinazoshiriki Ligi Kuu ya England ambazo zimeonyesha nia ya kumsajili Willian

“Ana ofa mbili kutoka katika timu zinazoshiriki Ligi Kuu ya England lakini pia kuna ofa kutoka Ligi Kuu ya Marekani (MLS). Pia ana ofa mbili mezani kutoka timu nyinginezo barani Ulaya.

Advertisement

Hivyo Willian yuko katika hali nzuri na mara baada ya msimu kumalizizika, atatoa uamuzi wake,” alisema Joorabchan

Kitendo cha mchezaji huyo kukaribia kutua Arsenal, Kinadaiwa kimeanza kuipa hofu Chelsea ambayo inafikiria kutompanga kwenye kikosi chake kitakachocheza mchezo wa Fainali ya Kombe la FA dhidi ya Arsenal, Agosti Mosi.

Ikiwa Willian atajiunga na Arsenal, itakuwa ni mwendelezo wa timu hiyo kuvuna wachezaji kutoka Chelsea.

Kabla yake, wachezaji wengine waliowahi kuichezea Arsenal wakitokea Chelsea ni Yossi Benayoun, William Gallas, Petr Cech, Lassana Diara ma David Luiz.

Advertisement