Wikiendi ya kushikana mashati FDL

Saturday June 27 2020
fdl pic

Ligi Daraja la Kwanza (FDL), wikiendi hii itasimamisha nchi wakati jumla ya mechi 10 zitakapochezwa katika miji tofauti ambapo leo Jumamosi jumla ya mechi tisa zitachezwa na kesho kutakuwa mchezo mmoja.

Katika kundi B kutakuwa na mechi tatu za watani wa jadi wanaotoka katika eneo moja (Derby) ambapo  Pamba itacheza na Gwambina FC ambao ni vinara wa kundi hilo, Green Warriors na Transit Camp za Dar es Salaam zitaumana zenyewe wakati  huko Geita nako kutakuwa na mchezo wa ndugu wawili ambao ni Gipco na Geita Gold.

Chama la Wana 'Stand United' ya Shinyanga, itawakaribisha AFC ‘ Machalii wa Arachuga’, na Rhino Rangers atacheza na Mashujaa FC Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora.

Kundi A, Majimaji atacheza na Dodoma, Ihefu FC ikivaana na Afrcan Lyon, Mbeya Kwanza na Friends Rangers huku Iringa United ikiikaribisha Cosmopolitan.

Kesho Jumapili kutakuwa na mchezo mmoja wakati Mlale FC ambayo imekumbana na rungu la kucheza bila mashabiki ikiikaribisha Njombe Mji kwenye Uwanja wa Majimaji.

Mlale wanaingia kwenye mchezo huo wakiwa na pigo la kufungiwa miezi sita kocha wao, Rashid Mpenda na faini Ya Sh 300,000 kwa kosa la kuwa kinara kwenye fujo zilizosababisha mchezo kuvunjika walipokuwa wakicheza na Dodoma Jiji FC.

Advertisement

Mchezo huo unakuwa na umuhimu mkubwa kwa Njombe Mji inayonolewa na Kocha, Kenneth Mkapa katika kufufua matumaini ya kucheza hatua ya mtoano ya FDL.

Ikumbukwe wiki iliyopita, Njombe Mji ilipoteza kwa kuchapwa bao 1-0 mbele ya Majimaji iliyokuwa kwenye uwanja wa nyumbani.

Mlale FC haina cha kupoteza baada ya hesabu zake za kusalia FDL kuonekana kugonga mwamba na tayari safari ya kushuka daraja ikiwa imewadia.

Katibu wa timu hiyo, Baraka Ambakisye anasema tayari kikosi hicho kimewasili salama Songea kwaajili ya mpambano wa leo.

"Kocha na wachezaji wote wanafahamu umuhimu wa mchezo huu ili kuhakikisha lengo kupanda Ligi Kuu linaendelea kubaki vichwani mwetu licha ya kusalia kwa michezo michache ligi kumalizika," anasema Ambakisye.

Wakati huohuo jana Ijumaa Boma FC imeambulia sare ya tisa kwenye Ligi Daraja la Kwanza (FDL) na kufanya timu hiyo kuendelea kubaki nafasi ya nane ambayo sio salama kwa upande wao.

 

Advertisement