Wenger sasa akata mzizi wa fitina Ulaya

Muktasari:

Wenger aliyekuwa akipewa nafasi ya kumrithi Slavisa Jokanovic wa Fulham, amesema ataweka bayana timu atakayoinoa Januari, mwakani. Claudio Ranieri, kocha mwenye uzoefu na Ligi Kuu England, amerejea baada ya kukubali ofa ya kuinoa Fulham.

London, England. Arsene Wenger, ameweka ngumu kurejea katika soka baada ya kuombwa na klabu ya Fulham inayoshiriki Ligi Kuu England.

Wenger aliyekuwa akipewa nafasi ya kumrithi Slavisa Jokanovic wa Fulham, alisema ataweka bayana timu atakayoinoa Januari, mwakani. Claudio Ranieri, kocha mwenye uzoefu na Ligi Kuu England, amerejea baada ya kukubali ofa ya kuinoa Fulham.

Mtaliano huyo mwenye miaka 67, anakumbukwa na mashabiki wa soka Ulaya, baada ya kuipa Leicester City ubingwa wa England mwaka 2015.

Mmiliki wa Fulham Shahid Khan alisema wiki iliyopita alikutana na makocha mbalimbali kwa ajili ya kuhojiwa na Wenger alikuwa miongoni mwao.

Kwa mujibu wa kigogo huyo, Wenger alimwambia hana mpango wa kufundisha soka England na anatarajia kurejea katika benchi Januari.

Mfaransa huyo aliifundisha Arsenal kwa miaka 22 kabla ya kuondoka na nafasi yake kujazwa na Unai Emery.

Wenger mwenye miaka 69, ameendelea kushikilia msimamo wake licha ya kuwindwa na klabu tofauti Ulaya.