Watano Exim waula Afcon

Muktasari:

  • Naye Mkuu wa Idara ya Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Exim, Stanley Kafu alisema kampeni hiyo inatoa nafasi kwa washindi hao kuishuhudia Stars ikitimiza ndoto zake za kushiriki katika mashindano ya AFCON baada ya zaidi ya miaka 30 kupita.

WATEJA watano wa Benki ya Exim wameula baada ya kutangazwa washindi wa tiketi za kwenda kuishangilia Taifa Stars kwenye Fainali za Kombe la Afrika (Afcon) 2019 nchini Misri.

Washindi hao walitangazwa juzi kupitia kampeni ya ‘Deposit & Win – Twende Tukaliamshe Misri’ iliyotoa fursa kwa wateja wa benki hiyo kulipiwa gharama zote za safari na malazi ili waweze kushuhudia mechi za Stars katika fainali hizo za 32.

Walionyakua tiketi za awali ni Mussa Mohammed (Mtwara), Athumani Hassani (Manyara), Deogratius Kessy (Arusha), Msimu Ngaruka (Dar es Salaam) pamoja na Justine Tembo (Arusha).

Akizungumza baada ya kupatikana kwa washindi hao kupitia droo yao iliyosimamiwa na Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), Mkuu wa Huduma za Rejareja wa benki hiyo, Andrew Lyimo alisema washindi hao wamelipiwa gharama zote za safari ikiwemo visa, tiketi ya ndege, gharama za tiketi ya kushuhudia mechi hizo pamoja na fedha za kujikimu.

Naye Mkuu wa Idara ya Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Exim, Stanley Kafu alisema kampeni hiyo inatoa nafasi kwa washindi hao kuishuhudia Stars ikitimiza ndoto zake za kushiriki katika mashindano ya AFCON baada ya zaidi ya miaka 30 kupita.

Kafu alisema kampeni hiyo ni sehemu ya mkakati wa kibenki katika kutafuta kesho bora kwa wateja wake na jamii kwa ujumla, ambapo pamoja na mambo mengine wamekuwa wakiunga mkono ajenda za kitaifa ikiwemo michezo.

Tanzania inashiriki fainali hizo kwa mara ya pili baada ya kufuzu mara ya kwanza mwaka 1980 zilipofanyikia Nigeria na imepangwa Kundi C na Senegal, Algeria na Kenya.

Stars itaanza kampeni Juni 23 dhidi ya Senegal kabla ya kurudi tena uwanjani siku mbili baadaye kuikabili Kenya na kumalizia Julai 3 kwa kuvaana na Algeria, na kama itapata matokeo mazuri itafuzu hatua ya 16 bora.