Watakiwasha Ligi Kuu ya wanawake

MSIMU mpya wa Ligi Kuu ya Wanawake unatarajiwa kuanza Oktoba japo tarehe hajapangwa hadi sasa. Jumla ya timu 12 ndizo zitakazoshiriki ligi hiyo zimeonekana kufanya usajili wa wachezaji ambao unatarajiwa kusumbua sana kutokana na viwango walivyoonesha msimu uliopita.

Mbali na wachezaji wapya waliosajiliwa kwenye vikosi husika, pia kuna wachezaji wa zamani wa timu hizi ambao pia wanatarajiwa kuwa watakuja kusumbua sana kwa kuangalia pale walipoishia msimu uliopita. Mwanaspoti inakuletea nyota ambao wanatarajiwa kuonyesha kiwango kikubwa kwa msimu huu.

Oppah Clement (Simba Queens)

Miongoni mwa wachezaji waliochangia Simba kuchukua ubingwa wa kwanza wa Ligi Kuu msimu uliopita ambapo alimaliza msimu kwa kufunga mabao 16 na kuwa mmoja kati ya wachezaji wawili wa Simba ambao walifunga mabao mengi. Oppah amekuwa na muendelezo wa kufunga mabao zaidi ya kumi kwa misimu miwili. Kiwango alichoonesha msimu uliopita kinaashiria huenda akawa na makali zaidi katika msimu huu.

Fatuma Mustafa (JKT Queens)

Amekuwa hapewi heshima kubwa huenda kwa sababu aina ya timu ambayo anachezea kutokuwa na kundi kubwa la mashabiki, lakini fundi huyu amekuwa na muendelezo wa kufunga mabao mengi tokea aanze kucheza katika Ligi Kuu, msimu wa 2016-17 alifunga mabao 18, 2017-18 alifunga mabao 25, 2018-19 alifunga mabao 38 na msimu uliopita mabao 31 na amekuwa mfungaji bora kwa misimu miwili mfululizo. Msimu huu pia anatajwa kuwa huenda atasumbua kutokana na uwezo wake mkubwa wa kufumani nyavu.

Aisha Masaka (Yanga Princess)

Msimu uliopita aliichezea Alliance Girls na akafanikiwa kufunga mabao 17 hadi msimu unamalizika, hiyo iliifanyaYanga Princess kumsainisha ili kuboresha safu yao ya ushambuliaji ambayo haikuwa na makali kwa msimu uliopita ambapo ilimaliza ikiwa imefunga mabao 53, na mchezaji aliyefunga mabao mengi alikuwa ni Shelda Boniphace aliyefunga mabao 11.

Hivyo Masaka ana uwezo mkubwa wa kufumania nyavu kama alivyofanya akiwa na Alliance anatarajiwa kufanya makubwa katika kikosi hicho. Lakini licha ya Aisha kujiunga na Yanga lakini usajili wake unaonyesha bado ni mchezaji halali wa Alliance ambayo inadai kuwa amebakisha mkataba wa mwaka mmoja, Mwanaspoti ilimtafuta Mwenyekiti wa Alliance, Stephano Nyaitati ambaye anasema wamewasilisha barua kwa TFF, baada ya kumuona mchezaji huyo anaichezea Yanga.

Asha Rashid (JKT Queens)

Msimu uliopita alisumbuliwa na majeraha yaliyomfanya asiendeleze vita yake ya kuwania tuzo ya mfungaji bora. Licha ya kuukosa mzunguko wa pili lakini alionesha kuwa ni mchezaji hatari kwani mpaka anakaa nje tayari alikuwa na mabao 19 ambayo yalimfanya kumaliza nafasi ya pili kwenye mbio za ufungaji. Mwalala anatarajiwa kuonesha kiwango kikubwa msimu huu kutokana na uwezo wake aliionesha kwa misimu mitatu mfululizo ndani ya ligi na timu ya Taifa.

Stumai Abdallah (JKT Queens)

Kwenye orodha ya wafungaji bora watatu wa msimu uliopita, yeye pia alikuwepo kwa kufunga mabao 19, sawa na Mwalala, licha ya kuwa ni kiungo lakini amekuwa na uwezo mkubwa wa kufumani nyavu. Naye anatajwa kuwa atasumbua sana kwa msimu ujao.

Mwanahamisi Omary (Simba Queens)

Ukipenda muite Gaucho. Ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa na amekuwa anacheza kwenye kiwango kikubwa kwa muda mrefu, yeye pia anatarajiwa kuendeleza moto kwa msimu ujao, msimu uliopita alifunga mabao 16 na kushika nafasi ya nane kwenye orodha ingawa walikuwa watatu wenye idadi hiyo. Mwanahamisi ambaye ameiwezesha Simba Queens kuchukua ubingwa wa kwanza tokea ipande daraja msimu wa 2017-18 naye anatajwa kuja kusumbua sana.

Amina Ramadhani (Ruvuma Queens)

Ni mchezaji kinara kwa utupiaji wa mabao ndani ya Ruvuma, kwenye msimu uliopita ambapo alimaliza akiwa na mabao 18, uwezo mkubwa wa kufunga kwa kutumia mipira ya kichwa na miguu, sambamba na kukaa kwenye nafasi unamfanya kuwa mchezaji tishio awapo uwanjani, anatarajiwa kuwa ni miongoni mwa mafundi ambao wanaweza kusumbua kwa msimu ujao.

Acha tuone msimu huu makali yao.