Watakimbiza mwanzo mwisho msimu huu

Muktasari:

Makala haya yanakuletea baadhi ya maeneo ambayo KMC inaonekana kuimarika na kutokuacha kitu kama ambavyo ilikuwa msimu uliopita.

LIGI Kuu Bara inaanza leo lakini KMC watakuwa miongoni mwa timu nne pamoja na Simba, Yanga na Azam zitakazoshindwa kutupa karata zao wikiendi hii kutokana na kuwa na majukumu ya kuiwakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika na Ligi ya Mabingwa.

Licha ya kuwa ni msimu wake wa pili tu kwenye Ligi Kuu, KMC ni miongoni mwa timu zinazotazamiwa kufanya vizuri msimu huu baada ya kutisha katika msimu wake wa kwanza walipomaliza katika nafasi ya nne na kupata nafasi ya kuiwakilisha nchi katika Kombe la Shirikisho Afrika.

Makala haya yanakuletea baadhi ya maeneo ambayo KMC inaonekana kuimarika na kutokuacha kitu kama ambavyo ilikuwa msimu uliopita.

Nyota wazawa

Wachezaji 25, waliokuwa katika kikosi cha KMC, ni wazawa ambao hawa wote wamesajiliwa kucheza Ligi Kuu Bara ili kuhakikisha timu hiyo inafanya vizuri kwa kushirikiana wale ambao walikuwa msimu uliopita na waliosajiliwa kutokea katika timu nyingine mbalimbali.

Wachezaji hao ni Boniface Maganga, Kenny Ally, Ramadhani Kapera, Amos Charles Abdallah Mfuko, George Sangija, Charles Ilamfia, Rayman Mgungila, Abdul Hilary, Salim Ayee, Sadala Lipangile, Omary Ramadhani, Hassan Kabunda, Mohamed Samatta, Cliff Buyoya, Juma Kaseja, James Msuva, Rehani Kibingu, Ally Msengi na Ismail Gambo.

Wengine wachezaji wazawa waliokuwa kwenye kikosi cha KMC, msimu huu Ally Ramadhani, Kelvin Kajili, Vitalis Mayanga, Denis Richard na Abbas Amiri.

Mastaa wapya

KMC msimu huu imefanya usajili wa wachezaji wasiopungua saba ili kuziba upungufu uliojitokeza msimu uliopita ambao walishangaza wengi baada ya kumaliza katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara.

Msimu huu KMC ina wakali saba ambao wanatazamwa kuja kuibeba KMC katika mashindano yote ambayo watashiriki msimu huu kulingana na kile ambacho walikifanya msimu uliopita.

Wachezaji hao saba ambao wanatazamwa kuja kuibeba KMC msimu huu ni Kenny Ally waliyemtoa Singida United, Ramadhani Kapera aliyesajiliwa kutokea Kagera Sugar, Amos Charles aliyetokea Mbao, Abdallah Mfuko na Vitalis Mayanga waliotokea Ndanda, Salim Ayee aliyetokea Mwadui, Mohamed Samatta aliyetokea Mbeya City.

Nyota wa Kigeni

Kikosi cha KMC, msimu huu kina wachezaji 31, ambao kati ya hao nyota sita ni raia wa kigeni kutoka katika nchi tatu tofauti ambao wamekuja kuongeza nguvu na kuhakikisha timu hiyo inapata matokeo mazuri na kupiga hatua katika mafanikio zaidi ya msimu uliopita katika mashindano yote ambayo watashiriki.

Wachezaji hao sita wa kigeni waliopo katika kikosi cha KMC ni Yussuf Ndikumana na Jonathan Nahimana hawa wote walikuwa kwenye kikosi msimu uliopita ambao ni raia wa Burundi na kiungo mzoefu Jean-Baptiste Mugiraneza, aliyesajiliwa msimu huu anatokea nchini Rwanda.

Nyota wengine wapya kikosini KMC, Melly Sivirwa na Javier Besala Bokungu kutoka DR Congo na Serge Alain kutoka Ivory Coast.

Jezi za nyumbani na ugenini

Kikosi cka KMC msimu huu watakuwa na jezi aina tatu tofauti na msimu uliopita walikuwa wakitumia za aina mbili kwa maana ya nyeupe za juu chini bukta nyeusi ambazo walikuwa wakitumia katika michezo ya nyumbani na nyeusi ambazo zilikuwa na michirizi ya pinki kwa mbali hizo walikuwa watumia katika mechi za ugenini.

Msimu huu mbali ya kuwepo na hizo mbili lakini wameongeza nyingine ya tatu ambayo itakuwa inatumika pindi watakapokutana na timu ambayo ina jezi yenye rangi hizo mbili ambayo watatumia itakuwa ya pinki juu na bukta za bluu kama ambavyo walifanya katika mechi ya kwanza dhidi ya AS Kigali katika Kombe la Shirikisho Afrika wiki mbili zilizopita.

Katika kuhakikisha jezi zao ni mali, waliingia mkataba wa miaka mitano na kampuni ya michezo ya kubahatisha M-Bet, wenye thamani ya Sh 1, Bilioni ambayo hayo maandashi yatakuwa yakikaa mbele ya jezi ya juu yoyote ambayo itavaliwa na wachezaji wa timu hiyo wanapokuwa mazoezini au kwenye mechi.

Uwanja wa nyumbani

Kikosi cha KMC, ambacho kinaiwakilisha nchi katika Kombe la Shirikisho Afrika, kitatumia Uwanja wa Taifa katika mechi yao ya marudiano leo hapa nyumbani dhidi ya AS Kigali baada ya mechi yao ya kwanza kutoka suluhu pale Kigali Rwanda.

Katika Ligi Kuu Bara, kikosi cha KMC, kitakuwa kikitumia Uwanja wa Uhuru kama uwanja wake wa nyumbani lakini watakapocheza dhidi ya timu kongwe za Simba na Yanga watatumia uwanja wa Taifa kama uwanja wa nyumbani na hata pale watakapocheza michezo ya ugenini kama ambavyo ilikuwa msimu uliopita.

Uwanja wa Uhuru unaweza kuwa na faida kwa KMC, kwa maana una eneo zuri la kuchezea na hasa katika mchezo wa kumiliki mpira muda mwingi kama ambavyo kocha wa timu hiyo Mayanja anahitaji, lakini itakuwa faida kwa timu yoyote ambayo watakutana nayo kwani eneo la kuchezea linaruhusu.

Ufundi wa makocha

Kikosi cha KMC, ni miongoni mwa timu kwenye ligi ambazo zilifanya mabadiliko ya benchi la ufundi baada ya kuachana na Ettiene Ndayiragije aliyekwenda kujiunga na Azam, na wao kumchukua kocha wa zamani wa Simba na Kagera Sugar kwa nyakati tofauti, Jackson Mayanja.

Mayanja ni miongoni mwa makocha ambao wanaamini katika soka la kucheza kwa maana ya kumiliki mpira muda mwingi na kushambulia kuanzia nyuma huku timu yake ikianza na washambuliaji wawili kama alivyofanya katika mechi ya kwanza na AS Kigali ugenini alipoanza na Vitalis Mayanga na Salim Aiyee.

Katika mfumo wa kucheza kwenye mechi nyingi Mayanja ameonekana kuwa muumini wa kutumia mfumo wa 4-4-2, ambao unakuwa na mabeki wanne, viungo wanne na washambuliaji wawili au muda mwingine anatumia (4-3-3), ambapo kunakuwa na mabeki wanne, viungo watatu na washambuliaji watatu.

Kikosini inajivunia mdunguaji anayetisha Aiyee na uwapo wa kipa mzoefu Juma Kaseja ambaye ameshashiriki michuano mingi ya kimataifa wakati akidakia klabu za Simba na Yanga na pia timu ya taifa ya soka, Taifa Stars.

Licha ya kuwa nje ya timu ya taifa ya Tanzania kwa miaka mingi, hatimaye alirejeshwa hivi karibuni na kutokana na kipaji chake aliisaidia Stars kuing’oa Harambee Stars ya Kenya katika kufuzu kwa fainali za Chan.