Wanyama awamwagia sifa Harambee Stars

Muktasari:

  • Wanyama kaisifia timu kwa kujikakamua na kumaliza nafasi ya tatu kundi C huku ushindi pekee waliosajili ukiwa dhidi ya majirani Tanzania walipoteza  mechi zao zote.

NAHODHA wa timu ya taifa Harambee Stars, Victor Wanyama kaipongeza kikosi licha ya kubanduliwa nje ya mashindano ya AFCON 2019 juzi Jumanne.

Baada ya kucharazwa na Senegal Jumatatu imani ya Stars kutinga hatua ya 16 bora ilisalia kwa dua la kuzitaka timu mbili Angola na Benin kupoteza mechi zao ili Stars ipate fursa ya kupenya kama mojawepo ya timu nne bora zilizomaliza katika nafasi ya tatu.

Hata hivyo, ni Angola tu ndiyo iliyopoteza dhidi ya Mali huku Benin ikilazimisha sare tasa dhidi ya Cameroon.

Kwa maana hiyo Stars waliokuwa na alama tatu sawa na Benin wakachujwa kutokana na tofauti ya idadi ya mabao.

Wanyama awasifia Stars

Licha ya yote, Wanyama kaisifia timu kwa kujikakamua na kumaliza nafasi ya tatu kundi C huku ushindi pekee waliosajili ukiwa dhidi ya majirani Tanzania walipoteza  mechi zao zote.

“Kikweli pamoja na kubanduliwa, naionea fahari timu yetu pamoja na benchi la ukufunzi. Kila mdau alijituma, tulijitahidi kadri ya uwezo wetu. Wakati mwingine tunakosea ila ndio hula ya wanadamu na kikubwa zaidi ni kujifunza kutokana na makosa yetu ili tuweze kujiboresha.

Migne kuwakopi Uganda

Ni kauli iliyoungwa mkono na Kocha wa Stars, Sebastian Migne aliyesema ushiriki wao ulikuwa ni funzo tosha huku akitolea mfano Waganda aliosema ni mfano mwema wa kuigwa.

“Kwetu kuwa hapa baada ya miaka 15 ni funzo tosha. Bado hatujaiva na kwa hakika tunahitaji ushiriki zaidi wa mashindano ya hadhi kama hii ili kubobea. Kwa mfano waangalieni Waganda walifuzu makala yaliyopita hawakufika mbali, wamerudi safari hii na mnaona walivyoboreka tunahitaji kuwa kama wao,” Migne akasema akirejealea hatua ya kufuzu kwa Uganda waliotinga 16 bora.

Waziri Amina achafua Stars

Naye Waziri wa Michezo Balozi Amina Mohammed aliamua kuwachafua Stars kwa kuwaandalia karamu ba’kubwa katika hoteli moja iliyopo kwenye ufuo wa mto Nile, huku akiwapa wosia wa kutokataa tamaa na kuwataka wahakikishe wanafuzu kwa makala yajayo vile vile.

“Jamani ninachosema ni hichi, mmejitahidi. Tupo hapa baada ya miaka 15 hata Roma haikujengwa kwa siku moja. Ningependa tena kuona mkifuzu kwa Makala yajayo,” Waziri Mohammed alisema.

Kikosi cha Stars kiliwasili nchini Jumanne jioni baada ya kuwa nje ya nchi kwa mwezi mzima tangu walipoingia kambini Mei 31 kule Ufaransa.