Wanariadha hawa rekodi zao bado zinatesa watu Bongo

Muktasari:

Kwa wanariadha wa Bongo pia tumeshuhudia miaka mingi rekodi zikiendelea kuvunjwa na nyingine zikiendelea kudumu. Hawa hapa wanariadha na rekodi zao tamu zinazotamba.

WAKATI kidume, Eliud Kipchoge akiwa na ndiye mtu mwenye kasi dunia kwenye mbio ndefu (marathon) kutokana rekodi zake tamu alizoziweka katika tasnia hiyo, hapa Bongo pia wapo wakali.

Achana na rekodi aliyoweka, Vienna, Austria ya saa 1:59:40 ambayo haitambuliki na Shirikisho la Riadha duniani (IAAF), kutokana na sababu mbalimbali, lakini rekodi aliyoiweka Berlin Marathon mwaka 2018 ya saa 2:01:39 ndio inatambulika.

Kwa wanariadha wa Bongo pia tumeshuhudia miaka mingi rekodi zikiendelea kuvunjwa na nyingine zikiendelea kudumu. Hawa hapa wanariadha na rekodi zao tamu zinazotamba.

AUGUSTINO SULLE -MARATHONI

Mfukuza upepo huyu ndiye anayeshikilia rekodi ya bora ya muda ya taifa kwa wanariadha wanaokimbia mbio ndefu (marathoni).

Sulle alifanya hivyo Toronto Marathon mwaka 2018 alipotumia muda wa saa 2:07:45 na kuvunja ile ya mkongwe Juma Ikangaa aliyoiweka mwaka 1989 katika New York Marathon alipomaliza mbio kwa muda wa saa 2:08:01, japo Samson Ramadhan mwaka 2003 kule London Marathon alitumia muda huo.

BANUELIA MLASHANI -MARATHONI

Kwa upande wa kina dada, rekodi ya taifa inashikiliwa na Banuelia Mlashani aliyoiweka Tokyo Marathon mwaka 2002 alipotumia muda wa saa 2:24:00.

Mwanadada huyo alivunja rekodi ya Blanka James ya saa 2:26:00 aliyoiweka mwaka 1989 kule Barcelona ambayo ilidumu kwa miaka 13.

ISMAIL JUMA - NUSU MARATHONI

Kwa upande wa mbio za nusu marathoni kazi inaendelea kuwa ngumu kwa muda uliowekwa na Ismail Juma mwaka 2017 kule Istanbul ya nusu marathoni kwa muda wa dakika 59:30.

Ismail alivunja rekodi ya 59:52iliyowekwa na Dickson Marwa mwaka 2008 huko Ras Al Khaimah nusu Marathon. Awali Faustin Baha ndiye alikuwa akifuata kwa dakika 59:45 iliyowekwa Lisbon Mwaka 1996.

MAGDALENA SHAURI - NUSU MARATHONI

Ametamba kwa muda mrefu kwenye mbio ndefu kabla ya kujiunga na timu ya JWTZ. Lakini majeraha ya hapa na pale yalimfanya kupotea kwa muda kwenye tasnia hiyo.

Mapema mwaka huu alitupa karata yake kule Dubai Nusu Marathon ambapo alifanikiwa kumaliza mbio kwa muda wa saa 1:06:19 na kuivunja ile ya saa 1:07:37 aliiweka Restuta Joseph mwaka 2000 kule Uingereza.

EMMANUEL GINIKI - 10KM

Giniki ni mpwa wa wanariadha mashuhuri nchini, Gidamis na Alfredo Shahanga. Aliandika muda wake bora wa taifa katika mbio za km 10 kule Uholanzi Oktoba, 2018 alipomaliza nafasi ya pili kwa muda wa dakika 27:38.

Awali muda bora ulikuwa umewekwa na Fabiano Joseph 21 Mei 2006 Great Manchester Run United Kingdom Manchester, alipotumia 27:41.

Kwa upande wa kina dada rekodi bado inakamatwa na Restuta Joseph aliyoiwekwa mwaka 1996 Ufaransa alipomaliza mbio kwa muda wa dakika 30:16.

FILBERT BAYI - MITA 1500

Bingwa wa mashindano ya Jumuiya ya Madola mwaka 1974 kule Christchurch, New Zealand alipoiweka rekodi ya dunia ya mbio hizo kwa muda wa dakika 3:32:16 baadaye ilivunjwa na Sebastiane Coe mwaka 1979 alipotumia dakika 3:32:15 ambaye sasa ni Rais wa IAAF.

REKODI NYINGINE

Rekodi ya Mita 100 ni Sekunde 10.1 ya Jumanne Chobanga ya mwaka 1979, mbio za mita 200 ni sekunde 21.27 ya Ali Gulam aliweka 2015 African Games huko Jamhuri ya Congo, mita 400 ni sekunde 45.74 ya Claver Kamanya mwaka 1968 kwenye Olimpiki, Mexico.

Mbio za mita 800 ni dakika 1:45.28 ya Samwel Mwera mwaka 2005 Brazil Rio de Janeiro, Brazil, mita 1000 dakika 2:17.85 ya Samwel Mwera pia mwaka 2003 Italia Oristano. Mita 3000 dakika 7:39.27 ya Filbert Bayi kule Bislett Games Norway Oslo mwaka 1980, Mita 5000 ni dakika 13:03.62 ya John Yuda mwaka 2002 Golden Gala, Roma Italia.

Kilomita 5 dakika 13:36 ya Andrew Sambu mwaka 1995 United Kingdom London, mita 10000 dakika 27:06.17 ya John Yuda mwaka 2002 huko Memorial Van Damme Brussels, Ubelgiji.

Kilomita 15 muda wa dakika 42:15+ ya Gabriel Geay mwaka 2017, Kilomita 25 ni saa 1:13:56 ya John Yuda 2001 Berlin 25K Germany, Kilometa 30 ni saa 1:30:09 ya Augustino Sulle aliiweka 2018 Toronto Waterfront Marathon Canada.