Wamerithi jezi, wamerithi mikoba

Muktasari:

Sasa buana kuna majembe yametua pale Msimbazi na fasta yamekabidhiwa jezi za wakali ambao walifunika nazo kinyama. Jamaa wamerithi jezi na wamedhamiria kuzitendea haki zaidi ya walioziacha.

WANYAMA wapya wameshatambulishwa pale Msimbazi na hizi ni habari mbaya kwa wapinzani wa Simba katika msimu huu ambao jamaa wanapigania kubeba taji lao la tatu mfululizo la Ligi Kuu ya Bara.

Katika kuthibitisha kuwa Wekundu wa Msimbazi wamepania msimu huu, yule ‘mtu mbaya’ Meddie Kagere ‘MK 14’ ameshatuma salamu katika mechi ya kwanza tu kwenye msimu mpya katika ardhi ya nyumbani. Mnaisoma hiyo? Jamaa ametupia tatu buana katika ushindi wa 3-1 dhidi ya wale Power Dynamos ya Zambia Jumanne katika kilele cha Simba Day kwenye Uwanja wa Taifa.

Yaani MK14 ameendeleza palepale alipoishia msimu uliopita ambao alikuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Bara alipotupia mabao 23, ikiwamo ‘hat-trick’ moja. Mnahesabu huko? ‘hat-trick’ mbili hizo tayari kwenye ardhi ya Tanzania.

Sasa buana kuna majembe yametua pale Msimbazi na fasta yamekabidhiwa jezi za wakali ambao walifunika nazo kinyama. Jamaa wamerithi jezi na wamedhamiria kuzitendea haki zaidi ya walioziacha.

DEOGRATIAS KANDA (7)

Wengi walikuwa wanajiuliza nani anakuja kurithi namba ya mgongoni iliyokuwa inavaliwa na nyota Emmanuel Okwi.

Winga Deo Kanda akajilipua kuivaa jezi hiyo na katika mchezo wake wa kwanza akiwa nchini na aliweza kuonyesha kitu cha tofauti kilichowashtua mashabiki wengi.

Kanda ana spidi, uwezo wa kumiliki mpira lakini pia chenga za maudhi ambazo alikuwa akizipiga uwanjani na kuwafanya mashabiki wabaki vinywa wazi.

Uwezo aliouonyesha kama akiendelea kufanya hivyo, bila shaka mashabiki wa soka Simba watamsahau kipenzi chao, Okwi kwani Kanda ameonyesha kila kitu alichokuwa nacho mguuni licha ya kwamba umri umekwenda.

SHARAF ELDIN SHIBOUB (8)

Hakuna kiungo kutokea nje ya Bongo aliyeweza kuteka hisia za mashabiki wa Bongo kama alivyofanya fundi wa mpira kutoka Rwanda, Haruna Hakizimana Niyonzima.

Niyonzima ni miongoni mwa viungo bora waliowahi kucheza soka la Bongo, na ameondoka kishujaa akiwa na rekodi ya kubeba mataji ya Ligi Kuu ya Bara mara tano mfululizo – mara tatu mfululizo akiwa Yanga na mara mbili mfululizo akiwa Simba.

Hivi sasa hayupo na nafasi yake imechukuliwa na Shiboub kutoka Sudan, na jamaa tayari ameanza kuwasahaulisha taratibu machungu ya Niyonzima.

Katika mchezo dhidi ya Power Dynamos kila shabiki aliyekuwa uwanjani, alikuwa ananogewa na namna ambavyo kiungo huyu alivyokuwa akicheza soka lake kwa utulivu.

Shiboub ana uwezo mkubwa wa kuuchezea mpira atakavyo, akiuambia njoo unamfuata, anapiga pasi za hatari fupifupi na hata zile za kutoka upande mmoja wa uwanja hadi mwingine, lakini vilevile katika upande wa ukabaji kiungo huyu yuko vizuri.

Kwa namna moja ama nyingine anawasahaulisha mara mbili mashabiki wa Simba, James Kotei na Niyonzima ambao wameondoka huku wakipendwa na mashabiki kwa shughuli yao pale kwenye dimba la kati.

FRANCIS KAHATA (25)

Hili litabaki kuwa pengo katika kikosi cha Gor Mahia kutokana na namna ambavyo alikuwa mhimili mkubwa katika kikosi hiko kipindi chote alichokuwepo.

Simba ilianza kumpigia hesabu kwa muda mrefu lakini kujiunga nayo ilikuwa ikishindikana kutokana na mkataba kumbana kuondoka na Simba haikuwa tayari kuuvunja.

Hata hivyo, hakuna marefu yasiyokuwa na mwisho kwani hivi sasa anaonekana akiwa ndani ya uzi wa Msimbazi licha ya kuwa na vuta ni kuvute ya muda mrefu.

Ugumu unaokuja kwa Kahata ni jezi namba 25, ambayo ilikuwa inavaliwa na winga Shiza Kichuya ambaye alijitengenezea ufalme wake Simba kabla ya kutimka. Kichuya alikuwa akipiga kona za hatari ikiwamo kufunga kwa mpira wa moja kwa moja anaoupiga kutokea kwenye kibendera cha kona. Waulize Yanga!

Kahata hapa ana mtihani wa kuweka utawala wake.

BENO KAKOLANYA (30)

Kakolanya anasubiliwa na mashabiki wengi wa Simba kuonyesha ule ukali wake wa kuokoa michomo kama ambavyo alikuwa nao Yanga.

Deogratius Munishi alishindwa kupambana na Aishi Manula, licha ya kukaribia kumaliza msimu alionyesha kiwango lakini benchi la ufundi halikuwa na imani naye tena.

Kakolanya baada ya kutua alipewa jezi no 30 ambayo ilikuwa inavaliwa na Dida, lakini katika mchezo wa Simba Day kipa huyu alionyesha utulivu wa hali ya juu hasa katika upangaji wa mabeki.

Hali hiyo ilimsaidia kukaa dakika 21 katika kipindi cha kwanza bila kushambuliwa, hii inatokana na namna ambavyo unaweza ukawapanga mabeki na wakatulia. Je, watazitendea haki jezi? Tusubiri.