Wagombea uenyekiti Yanga waviziana kupiga kampeni

Muktasari:

  • Yanga pamoja na kuwa kwenye kipindi cha mpito kwa maana ya kuwa na ukata kwenye klabu yao,  wanaongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL),  wakiwa na pointi 50.

WAKATI Mbaraka Igangula akianza jana kuzindua kampeni zake,  mpinzani wake,  Jonas Toboroha ambaye naye anagombea nafasi ya uenyekiti wa Yanga SC,   kumbe alimtegea na kuamua kuanza leo.

Toboroha alisema hakuona sababu za kuanza kampeni zake jana na badala yake aliamua kuanza leo kwenye ukumbi wa makao makuu ya klabu ya Yanga,  uliopo Jangwani, jijini Dar es Salaam.

Katika uzinduzi wake leo mchana,  alisema inshu za mishara kwa wachezaji wa Yanga itasikika kwenye bomba kama atapata tena nafasi ya kuiongoza klabu hiyo.

"Nikiingia tu madarakani nitalimaliza hilo. Nawahakikishia hilo wanachama na mashabiki wote wa Yanga,  kikubwa ni wao kuniamini na kunipa hiyo nafasi ya kuwa mwenyekiti wao mpya, " alisema Tiboroha.

Hata hivyo katibu  huyo wa zamani wa Yanga,  alisema anachakujifunza kutoka kwa viongozi wa sasa wa Yanga ambao wameweza kuifanya timu kuwa na hamasa pamoja na kuwa kwenye kipindi hiki cha mpito.

"Bila ya wachezaji kupata mishahara yao kwa wakati ni ngumu kuona timu inafanya vizuri lakini kwa Yanga ni tofauti hapo nitoe pongezi zangu za dhati kwao, " alisema.

Yanga pamoja na kuwa kwenye kipindi cha mpito kwa maana ya kuwa na ukata kwenye klabu yao,  wanaongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL),  wakiwa na pointi 50.