Wageni hawa kazi wanayo

Muktasari:

Hata hivyo, hadi wanang’ara, wachezaji wa kigeni wanakuwa wanapitia changamoto nyingi kama vile lugha, mazingira, vyakula na staili ya timu.

PAZIA la Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2019/2020 litafunguliwa rasmi mwishoni mwa wiki hii kwa mechi kadhaa zitakazochezwa kwenye baadhi ya viwanja nchini.

Kuanza kwa ligi hiyo ni mwanzo wa kutamba kwa baadhi ya nyota kadri watakavyoonyesha viwango bora kwa msimu huo, lakini pia inaweza kuwa chanzo cha anguko la wachezaji wengine ambao watashindwa kuonyesha viwango bora.

Kwa muda mrefu, nyota wa kigeni wamekuwa wakitamba kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara katika nafasi mbalimbali wanazocheza kuanzia ile ya kipa, walinzi, viungo na washambuliaji.

Mfano katika misimu miwili iliyopita wachezaji wa kigeni wametwaa tuzo ya ufungaji bora wa Ligi Kuu mfululizo huku wale wa nafasi nyingine, wengi wakionyesha viwango bora kulinganisha na wazawa ambao ni wachache tu waliotamba.

Hata hivyo, hadi wanang’ara, wachezaji wa kigeni wanakuwa wanapitia changamoto nyingi kama vile lugha, mazingira, vyakula na staili ya timu.

Kwa kulitazama hilo, makala hii inakuletea orodha ya nyota wa kigeni waliosajiliwa na timu mbalimbali za Ligi Kuu ambao huenda wakakutana na wakati mgumu kwenye msimu ujao.

Tairone da Silva

Beki wa kati ambaye ni raia wa Brazil aliyesajiliwa na Simba katika kipindi cha usajili wa dirisha kubwa akirithi nafasi iliyoachwa na Juuko Murshid aliyeondoka.

Tairone anakabiliwa na wakati mgumu wa kuchukua nafasi na kutamba kwenye kikosi cha Simba kwani tayari kombinesheni ya Erasto Nyoni na Paschal Wawa imefiti na wachezaji hao wana uzoefu wa kutosha na wanaelewana vilivyo.

Lakini pia suala la lugha linaweza kumuweka kwenye wakati mgumu kwani anazungumza lugha ya Kireno ambayo haitumiki hapa nchini.

David Molinga ‘Ndama’

Ni usajili wa dakika za mwisho uliofanywa na Yanga kabla ya kufungwa kwa dirisha kubwa la usajili akitokea kwenye klabu ya Renaissance Du Congo ambako alishika nafasi ya tano katika kufumania nyavu kwenye Ligi Kuu ya DR Congo msimu uliopita akipachika mabao 11.

Kiwango kisichoridhisha ambacho amekionyesha kwenye baadhi ya mechi ambazo alipata nafasi ya kucheza na imani ya benchi la ufundi la Yanga kwa washambuliaji Sadney Urikhobi na Juma Balinya inaweza kumuweka kwenye wakati mgumu ndani ya timu hiyo.

Donald Ngoma

Hakuna asiyejua ubora na kiwango cha mshambuliaji Donald Ngoma katika kufumania nyavu na kutengeneza nafasi za mabao.

Hata hivyo, amekuwa akisumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara ambayo yamekuwa yakimuweka nje lakini pia usajili wa wachezaji Richard Djodi na Iddi Selemani ‘Nado’ unaweza kumfunika Ngoma aliyenaswa na Azam FC akitokea Yanga.

Gerson Fraga Vieira

Nahodha wa zamani wa timu za vijana za Brazil, kwa sasa yupo ndani ya kikosi cha Simba ambacho kimemsajili kwa ajili ya kuziba pengo la James Kotei aliyeondoka.

Hata hivyo Vieira mwenye uwezo wa kucheza nafasi ya beki wa kati na kiungo wa ulinzi, anakabiliwa na wakati mgumu kwenye kikosi cha Simba cha kuwapora nafasi Jonas Mkude na Sharaf Shiboub ambao wametengeneza muunganiko mzuri lakini hata akisema arudi kwenye nafasi ya beki, atakutana na kombinesheni ya Erasto Nyoni na Paschal Wawa.

Daniel Amoah

Mmoja wa wachezaji wazuri wa nafasi ya ulinzi kwenye kikosi cha Azam FC akiwa na uwezo wa kucheza kama beki wa kati na pia pembeni.

Ujio wa kocha Etienne Ndayiragije unaonekana kama shubiri kwake kwani amekuwa hapewi nafasi kwenye kikosi cha kwanza na badala yake nyota aliyeibukia kwenye kikosi cha vijana cha Azam FC, Oscar Masai ndio amekuwa akiaminiwa zaidi.

Wilker da Silva

Ni mshambuliaji wa kati kutoka Brazil ambaye amesajiliwa na Simba akitokea Bragantino ya huko kwao.

Hata hivyo mshambuliaji huyo amekutana na safu kali ya ushambuliaji ya Simba inayoundwa na Meddie Kagere na nahodha John Bocco ambao wanaelewana vyema ndani ya uwanja jambo linaloweza kumfanya awe na kazi ya ziada anayotakiwa kuifanya ili apate nafasi kikosi cha kwanza.

Issah Bigirimana

Wengi walitegemea kuona akiingia moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza cha Yanga baada ya kusajiliwa kutokana na kiwango bora alichoonyesha wakati alipokuwa anaitumikia APR.

Hata hivyo anaonekana kushindwa kulishawishi benchi la ufundi la Yanga na kujikuta akisotea benchi na kama asipobadilika anaweza kuichezea kwa msimu mmoja tu.