Wageni VPL watikisa kwa mabao

Muktasari:

 Meddie Kagere ndiye mfungaji bora wa msimu uliopita kwa mabao 22.

Dar es Salaam. Wakati Ligi Kuu ikiingia raundi ya tano mwishoni mwa wiki hii, makali ya nyota wazawa katika kufumania nyavu yanaonekana kupungua.

Licha ya kuanza kwa kasi raundi ya kwanza, mambo yameonekana kuanza kugeuka taratibu, huku nyota wa kigeni wakichomoza kwa kufunga mabao katika mechi zilizopita.

Kutokana na uwepo wa klabu chache ambazo zimesajili wachezaji wa kigeni, kupungua kwa namba ya mabao kwa wachezaji wazawa kunaonekana kujitokeza zaidi kwa timu za Simba, Yanga, Namungo na Azam, ambazo kila moja imesajili zaidi ya wachezaji watano wa kigeni msimu huu.

Takwimu zinaonyesha katika raundi ya kwanza ya Ligi Kuu msimu huu, wachezaji wazawa wamepachika idadi kubwa ya mabao lakini namba imekuwa ikipungua kutoka raundi moja kwenda nyingine.

Katika raundi ya kwanza, jumla ya mabao 14 yalifungwa katika mechi tisa, mabao 10 yalipachikwa na wachezaji wazawa na manne ya wageni.

Mambo yalianza kubadilika katika raundi ya pili, ambayo ilikuwa na jumla ya mabao 13 yaliyofungwa katika mechi zote tisa za raundi hiyo, huku kukiwa na upungufu wa bao moja kutoka katika idadi ya mabao yaliyofungwa na wazawa katika raundi ya kwanza, wakifunga tisa, huku wageni wakiwa na manne.

Namba hiyo ya mabao ya wazawa, iliendelea kupungua katika raundi ya tatu, ambayo licha ya kuwa na jumla ya mabao 14 yaliyofungwa, ni nane (8) tu yaliyopachikwa nao na wageni wakifunga sita.

Na raundi iliyopita, namba ya mabao ya wachezaji wazawa iliendelea kupungua kutoka nane hadi saba (7) huku wageni wakipachika mabao sita (6), wakitimiza idadi ya mabao 13 yaliyofungwa katika raundi hiyo ya nne ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Haiishii hapo tu, kwani ukiondoa Hassan Kabunda wa KMC na Mzamiru Yassini wa Simba, wazawa wengine wameonekana kukosa muendelezo wa kufumania nyavu katika zaidi ya mechi moja licha ya wageni kufanya hivyo.

Mzamiru alifunga bao moja katika mchezo wa kwanza, ambao Simba ilicheza na Ihefu na kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 na kisha kurudia tena katika mechi ya sare ya 1-1 na Mtibwa Sugar, wakati Kabunda alifanya hivyo dhidi ya Mbeya City waliyoichapa mabao 4-0 na karudia tena wakati KMC ikishinda 2-1 dhidi ya Prisons.

Kwa upande wa wageni, Prince Dube wa Azam FC, Lamine Moro (Yanga), Medie Kagere na Chris Mugalu wa Simba, wote wamefunga mabao katika mechi mbili.

Dube alifunga katika mechi dhidi ya Polisi Tanzania na akafanya hivyo dhidi ya Prisons, wakati Lamine Moro akifunga dhidi ya Mbeya City na Mtibwa.

Kwa upande wa Kagere na Mugalu, kila mmoja alifunga bao katika mechi ambazo Simba ilicheza dhidi ya Gwambina na Biashara United.

Mshambuliaji wa zamani wa Simba, Musa Hassan ‘Mgosi’ alisema wachezaji wa kigeni wamekuwa na muendelezo mzuri kwa sababu wanajituma.

“Wenzetu wamekuwa wakitambua wajibu wao na wanajitahidi kuhakikisha wanakuwa na ubora wao siku hadi siku, lakini sisi wengi tumekuwa na hulka ya kuridhika pale tunapoonesha kuanza vizuri. Tunatakiwa kubadilika,” alisema Mgosi.

Mshambuliaji wa Namungo FC, Blaise Bigirimana alisema hamu ya kutimiza malengo yake ndiyo imemfanya apachike mabao mawili hadi sasa.

“Lengo la kwanza ni kuisaidia timu yangu lakini lingine ni kuona namaliza nikiwa mfungaji bora wa ligi au kufunga idadi kubwa ya mabao hivyo najitahidi kujituma ili nitimize malengo hayo,” alisema Bigirimana.