Wachezaji ghali wa kila umri kuanzia miaka 13 hadi 34 duniani

Muktasari:

Kwenye orodha ya wanasoka ghali kwa kila umri, inawahusisha pia mastaa kama Paul Pogba, Virgil van Dijk, Cristiano Ronaldo na Neymar aliyeingia mara mbili kwenye orodha hiyo kwa wanasoka ghali wa kila umri kuanzia miaka 13 hadi miaka 34.

LONDON,ENGLAND.DIRISHA hili la uhamisho wa majira ya kiangazi huko Ulaya limezidi kunoga, huku usajili uliofanywa hadi sasa ukivunja rekodi kadhaa.

Kwa mfano, Real Madrid ililipa kiasi cha Pauni 88.5 milioni kunasa huduma ya supastaa wa Kibelgiji, Eden Hazard na hivyo kumfanya aweke rekodi ya kuwa mwanasoka ghali zaidi kwa walio na umri wa miaka 28.

Kwenye orodha ya wanasoka ghali kwa kila umri, inawahusisha pia mastaa kama Paul Pogba, Virgil van Dijk, Cristiano Ronaldo na Neymar aliyeingia mara mbili kwenye orodha hiyo kwa wanasoka ghali wa kila umri kuanzia miaka 13 hadi miaka 34.

Finley Burns – Miaka 13, Pauni 175,000

Manchester City ina historia ya kutumia pesa nyingi kunasa wachezaji makinda kama ilivyofanya kwa beki Finley Burns iliyemnasa kutoka Southend kwa Pauni 175,000 dirisha la uhamisho Januari 2017.

Burns ndiye mchezaji aliyesajiliwa kwa pesa nyingi zaidi kwa walio na umri kama wake wa miaka 13 kitu ambacho huduma zake pia itakuwa pamoja na kusomeshwa.

Sheyi Ojo – Miaka 14, Pauni 2 milioni

Liverpool ilishinda vita ya kunasa huduma ya Sheyi Ojo kipindi hicho alipokuwa na umri wa miaka 14 ilipolipa Pauni 2 milioni huko MK Dons kupata huduma yake. Chelsea nayo ilikuwa ikimtaka Ojo mwaka 2011.

Sasa ana umri wa miaka 22 Ojo bado anasubiri nafasi Anfield huku akitolewa kwa mkopo sana. Msimu huu atakuwa Rangers ya Kocha Steven Gerrard.

Raheem Sterling – Miaka 15, Pauni 5 milioni

Liverpool ilikwenda QPR na pesa yao Pauni 5 milioni kuinasa huduma ya Raheem Sterling kipindi hicho alipokuwa na umri wa miaka 15. Kiasi hicho cha pesa ni kikubwa kuwahi kulipwa kwa mchezaji wa umri huo. Sterling baada ya kuitumikia kwa mafanikio Liverpool, wababe hao wa Anfield walimpiga bei kwa Pauni 49 milioni kwenda Manchester City na kuingiza faida ya Pauni 44 milioni.

Pietro Pellegri – Miaka 16, Pauni 17.1 milioni

Kinda Pietro Pellegri aliweka rekodi ya kuwa mchezaji mwenye umri wa miaka 16 aliyenaswa kwa pesa nyingi zaidi wakati Januari mwaka huu aliposajiliwa na AS Monaco akitokea Genoa kwa ada ya Pauni 17.1 milioni.

Majeraha yamemtibulia Pellegri kuanza makali yake hadi sasa, lakini matumaini ni makubwa kwake kutokana na kipaji alichokuwa nacho.

Alexandre Pato – Miaka 17, Pauni 23.2 milioni

Kiwango chake bora akiwa Internacional ya huko Brazil kiliifanya AC Milan kuzama mfukoni na kutoa Pauni 23.2 milioni kunasa huduma ya straika Alexandre Pato kipindi hicho akiwa na umri wa miaka 17.

Hakuna mchezaji mwingine mwenye umri kama huo alinaswa kwa pesa nyingi kuliko yeye na ndiyo maana anashikilia rekodi ya kuwa mchezaji ghali kwa umri huo. Hiyo ilikuwa mwaka 2008.

Rodrygo Goes – Miaka 18, Pauni 42 milioni

Usajili huu umefanyika dirisha hili la majira ya kiangazi huko Ulaya na Real Madrid imekubali kuilipa Santos Pauni 42 milioni kwa ajili ya kunasa huduma ya kinda Rodrygo Goes. Haijafahamika kama Madrid itamtoa kwa mkopo Rodrygo baada ya kujiunga nao, lakini yote kwa yote anabaki kuwa mchezaji ghali zaidi kwa waliowahi kusajili wakiwa na umri huo.

Kylian Mbappe – Miaka 19, Pauni 166 milioni

Baada ya kuvutiwa na huduma yake aliyokuwa akitoa huko AS Monaco, Paris Saint-Germain iliamua kuwa moja ya timu zilizolipa pesa nyingi sana kununua mchezaji kinda kwa pesa ndefu, ilipolipa Pauni 166 milioni kunasa huduma ya supastaa wa Kifaransa, Kylian Mbappe.

Mshambuliaji huyo amekuwa mmoja kati ya wachezaji wenye vipaji vikubwa sana na bila ya shaka atauzwa kwa pesa ndefu atakapoamua kuondoka Paris.

Ousmane Dembele – Miaka 20, Pauni 135.5 milioni

Staa wa Kifaransa mwenye kipaji kikubwa, Ousmane Dembele alikwenda kujiunga na Barcelona akitokea Borussia Dortmund kwa Pauni 135.5 milioni. Huduma yake ilinaswa kwa pesa nyingi na kumfanya kuwa mmoja kati ya wachezaji waliosajiliwa kwa pesa nyingi sana kwa wakali walio na umri wa miaka 20 lililofanyika Agosti 2017.

Neymar – Miaka 21, Pauni 71.5 milioni

Mwaka 2013, Santos ya Brazil na Barcelona ya Hispania zilifanya biashara ya kuuziana supastaa wa Kibrazili, Neymar kwa ada ya Pauni 71.5 milioni.

Uhamisho huo ulimfanya Neymar kuwa mchezaji ghali zaidi kwa walio na umri wa miaka 21, huku jina lake likitokea mara mbili kwenye orodha hii ya wachezaji ghali wa kila umri duniani.

Huko Barcelona alikwenda kuunda kombinesheni matata kabisa na wakali Lionel Messi na Luis Suarez.

Frenkie de Jong – Miaka 22, Pauni 65 milioni

Baada ya kuhusishwa sana na Ligi Kuu England, hatimaye kiungo wa Kidachi, Frenkie de Jong alikwenda kujiunga na Barcelona kwa ada iliyotajwa kuwa ni Pauni 65 milioni. Uhamisho huo ambao utamfanya staa huyo aondoke Ajax na kwenda kukipiga huko Barcelona msimu huu unamfanya De Jong kuwa mchezaji ghali kwa wenye umri wa miaka 22, kwa sababu hakuna mchezaji mwingine hadi sasa aliyenaswa kwa pesa ndefu kushinda hiyo.

Paul Pogba – Miaka 23, Pauni 89 milioni

Juventus iliipiga Manchester United Pauni 89 milioni wakati ilipoiuzia kiungo wa Kifaransa, Pauni Pogba kwenye majira ya kiangazi mwaka 2016.

Huduma yake ilivyonaswa kwa pesa nyingi hivyo, kwanza ukiweka kando suala la kuwa rekodi kwa kipindi hicho, lakini hadi sasa Pauni 89 milioni bado inashikilia rekodi ya kuwa ghali kuwahi kulipwa kwa mchezaji mwenye umri wa miaka 23. Pogba ndiye mchezaji anayeshikilia rekodi hiyo kwa sasa.

Gareth Bale – Miaka 24, Pauni 85.3 milioni

Mwaka 2013, Real Madrid ilivunja rekodi ya dunia wakati ilipotoa Pauni 85.3 milioni kunasa huduma ya winga wa Tottenham Hotspur, Gareth Bale.

Kwa kipindi hicho, ada hiyo ilikuwa rekodi ya dunia, lakini hadi sasa licha ya kuvunjwa kwenye uhamisho wa jumla, Bale bado anashikilia rekodi ya kuwa mwanasoka ghali zaidi kwa wale waliosajiliwa wakiwa na umri wa miaka 24.

Neymar – Miaka 25, Pauni 200 milioni

Supastaa Neymar ametokea tena kwenye orodha hii. Safari hii ni wakati alipohama kutoka Barcelona kwenda Paris Saint-Germain na mabingwa hao wa Ufaransa walitoa Pauni 200 milioni kunasa huduma yake.

Ada hiyo bado inashikilia rekodi ya uhamisho hadi sasa, lakini jambo jingine Neymar anashikilia pia rekodi ya kuwa mwanasoka aliyenaswa kwa pesa nyingi zaidi kwa walio na umri wa miaka 25. Ni ngumu kuvunja rekodi hiyo.

Virgil van Dijk – Miaka 26, Pauni 75 milioni

Januari mwaka jana beki wa kati wa Kidachi, Virgil van Dijk alifanya uhamisho wa ndoto zake wakati alipohama kutoka Southampton kwenda kujiunga na Liverpool. Hata hivyo, uhamisho huo uliigharimu pesa nyingi sana Liverpool na iliweka rekodi ya kumfanya Mdachi huyo kuwa beki ghali zaidi duniani ilipolipa Pauni 75 milioni kupata huduma yake. Lakini, jambo jingine ada hiyo inamfanya Van Dijk kuwa mwanasoka ghali kwa wenye umri wa miaka 26.

Luis Suarez – Miaka 27, Pauni 75 milioni

Baada ya fainali za Kombe la Dunia 2014, Barcelona ilifanikiwa kunasa moja ya huduma matata kabisa kutoka kwa mshambuliaji wa kati wa kutoka Amerika Kusini, Luis Suarez.

Huduma ya fowadi huyo ilinaswa kwa Puani 75 milioni akitokea Liverpool, ambayo iliamua kumpiga bei staa wake. Hata hivyo, ada hiyo iliyolipwa inamfanya Suarez kuwa mwanasoka aliyesajiliwa kwa pesa nyingi zaidi kwa wanasoka wenye umri wa miaka 27.

Eden Hazard – Miaka 28, Pauni 88.5 milioni

Dili la Eden Hazard kwenda Real Madrid linasekana ada yake itapanda hadi kufikia Pauni 130 milioni kutokana na vile ambavyo atakwenda kufanya kwa wababe hao wa Bernabeu. Lakini kwa sasa Chelsea imeripotiwa kuweka kibindoni Pauni 88.5 milioni kwenye mauzo ya mchezaji huyo na kumfanya Hazard awe ameweka rekodi ya kuwa mchezaji aliyenaswa kwa pesa nyingi zaidi kwa wanasoka walio na umri wa miaka 28.

Diego Costa – Miaka 29, Pauni 57 milioni

Straika wa Kihispaniola mwenye asili ya Brazil, Diego Costa uhamisho wake wa kutoka Chelsea kwenda Atletico Madrid uliofanyika akiwa na umri wa miaka 29 umemfanya amnyang’anye Zinedine Zidane rekodi ya kuwa mwanasoka ghali kwa wenye umri wa miaka 29. Saini ya Costa ilinaswa kwa Pauni 57 milioni na hivyo kuwa mchezaji ghali kwa walionaswa wakiwa na umri wa miaka 29 duniani. Kwa maana hiyo, Costa kwa sasa ndiye mchezaji ghali kwa wenye miaka 29.

Paulinho – Miaka 30, Pauni 42 milioni

Baada ya kucheza hovyo akiwa na kikosi cha Tottenham Hotspur, Mbrazili Paulinho alitimkia zake Ligi Kuu China, ambako alitamba kwa miaka miwili kabla ya kunasa dili la kwenda kujiunga na Barcelona akiwa na umri wa miaka 30.

Barca ilimnasa Paulinho baada ya kulipa Pauni 42 milioni na hivyo kumfanya mchezaji huyo kuwa ghali zaidi kwenye wenye umri huo.

Hata hivyo, Paulingo amedumu Barca kwa miezi sita na sasa amerudi tena China.

Gabriel Batistuta – Miaka 31, Pauni 22 milioni

Fiorentina na AS Roma zilifanya biashara ya kuuziana mshambuliaji Gabriel Batistuta kwa Pauni 22 milioni akiwa na umri wa miaka 31. Ilikuwa pesa ndefu kulipwa kwa mchezaji mwenye umri huo, ambayo imebaki kuwa rekodi hadi sasa ‘Batigol’ ndiye mwanasoka ghali zaidi kwa walionaswa wakiwa na umri wa miaka 31. Mabao yake yaliisaidia Roma kubeba ubingwa wa Serie A msimu wa 2000/01 ambao ulikuwa wa kwanza tangu 1983.

Fernando Llorente –Miaka 32, Pauni 15 milioni

Straika wa Kihispaniola aliyeenda hewani kisawasawa, Fernando Llorente alinaswa na Tottenham Hotspur akitokea Swansea City kwa ada ya Pauni 15 milioni mwaka 2017.

Uhamisho huo ulifanyika wakati Llorente akiwa na umri wa miaka 32 na hivyo kumfanya awe anashikilia rekodi ya kuwa mwanasoka ghali zaidi aliyenaswa akiwa na umri huo. Hakuna mchezaji mwingine hadi sasa kwenye dunia ya soka mwenye umri wa miaka 32, ambaye alinaswa kwa pesa zaidi ya hiyo.

Cristiano Ronaldo –Miaka 33, Pauni 99.2 milioni

Si wengi waliokubaliana na pesa iliyolipwa na Juventus kupata huduma ya supastaa Cristiano Ronaldo kwenye umri aliokuwa nao. Wababe hao wa Italia walimsajili staa huyo kutoka Real Madrid kwa uhamisho ya Pauni 99.2 milioni na hivyo kuwa miongoni mwa mastaa walionaswa kwa pesa nyingi, lakini pia kushikilia rekodi ya kuwa mwanasoka ghali zaidi kwa walio na umri wa miaka 33. Juve ilimsajili Ronaldo kwa madhumuni ya kufanya vizuri Ulaya.

Jose Fonte – Miaka 34, Pauni 5 milioni

Baada ya kushindwa kupata nafasi ya kuanza kwenye kikosi cha kwanza cha West Ham United, beki Jose Fonte alitimkia zake China alikokwenda kujiunga na Dalian Yifang.

Staa huyo alinaswa na Wachina hao kwa ada ya Pauni 5 milioni na hivyo kuwa mwanasoka aliyenaswa kwa pesa nyingi zaidi kwa wakali walio na umri wa miaka 34. Hakuna mchezaji mwingine mwenye umri wa miaka hiyo aliyenaswa kwa pesa inayozidi kiasi hicho kilicholipwa kwa Fonte.