Wachezaji Yanga wagomea mazoezi wakidai mishahara yao

Thursday April 25 2019

 

By Charity James

Dar es Salaam. Wachezaji wa Yanga wamegoma kufanya mazoezi leo asubuhi kwenye Uwanja wa Chuo cha Maafisa wa Jeshi la Polisi, Kurasini mjini Dar es Salaam wakishinikiza walipwe malimbikizo ya mishahara yao pamoja na fedha za usajili.

Tukio hilo limetokea asubuhi ya leo Uwanja wa Chuo cha Maafisa wa Jeshi la Polisi, Kurasini mjini Dar es Salaam wakati wachezaji walipokutana kwa ajili ya mazoezi ya asubuhi.

Wachezaji wote walifika mazoezini mapema Saa 2:00 asubuhi ya leo, lakini wakawaagiza Manahodha wao, Ibrahim Ajibu na Juma Abdul waende kumuambia kocha Mwinyi Zahera hawatafanya mazoezi kwa sababu viongozi wamewapuuza.

Chanzo cha ndani kutoka ndani ya klabu hiyo kililiambia Mwanaspoti wamechukua uamuzi huo wakitaka kulipwa malimbikizo ya mishahara yao ya miezi mitatu na bonasi.

Yanga inajiandaa na mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Azam FC mchezo unaotarajiwa kuchezwa katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Advertisement