Wachezaji Prisons waitisha Simba

SIMBA ina kibarua kizito mbele ya Prisons timu hizo zitakapokutana Alhamis ijayo kwani kikosi cha wajelajela hakina masihara kinapocheza uwanja wa nyumbani.

Hata hivyo, Simba inaweza kupata wepesi kutokana na uchovu ambao watakuwa nao Prisons kwani hawatakuwa wamepata muda wa kupumzika baada ya kutoka kucheza na JKT Tanzania mjini Dodoma.

Prisons itaikabili JKT Tanzania kesho kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma na baada ya mchezo itasafari kurudi Sumbawanga kucheza na Simba Alhamisi.

Licha ya wachezaji wa Prisons kulalamikia ratiba inawabana na kuwachosha, lakini wamesema watapambana kiume ili kuvuna pointi tatu.

Rekodi zinaonyesha Simba imekuwa ikipata wakati mgumu inapoikabili Prisons kwenye uwanja wa nyumbani wa Sokoine, Mbeya, lakini hivi sasa maafande hao wamehama na wanatumia Uwanja wa Nelson Mandela, Sumbawanga.

Katika mechi mbili za msimu huu ambazo Prisons imecheza kwenye uwanja huo imeshinda moja dhidi ya Namungo kwa bao 1-0 na imepoteza moja dhidi ya Azam kwa bao 1-0. Katika mchezo dhidi ya Azam, Prisons ilicheza kwa kiwango bora lakini ikajikuta ikiruhusu bao dakika ya 89.

Katika misimu mitano mfululizo tangu mwaka 2015, Prisons imekutana na Simba kwenye Uwanja wa Sokoinea mara tano, huku Wekundu wa Msimbazi wakishinda mara mbili sawa na wajelajela, lakini timu hizo zikitoka sare mara moja. Jambo la kushangaza ni kwamba katika ushindi huo wa Simba kwenye misimu hiyo hawajawahi kuwafunga wajelajela bao zaidi ya moja.

Msimu uliopita timu hizo zilitoka suluhu wakati ule wa 2018/2019, Simba iliichapa Prisons bao 1-0 katika mchezo uliofanyika Agosti 28, 2018 na ikapata tena ushindi kama huo katika msimu wa 2017/2018 katika mchezo uliofanyika Novemba 18, 2017.

Prisons mara ya mwisho kuifunga Simba kwenye ligi kwenye Uwanja wa Sokoine iikuwa Novemba 9, 2016 ilipoichapa mabao 2-1. Awali iliibamiza Simba bao 1-0 msimu wa 2015/2016 katika mchezo uliofanyika Oktoba 21, 2015.

WACHEZAJI PRISONS

Beki wa timu hiyo, Salum Kimenya amesema anaona mechi yao na Simba itakuwa na ushindani mkubwa, lakini anaziachia dakika 90 ziamue kwa aliyejiandaa vizuri kuchukua pointi tatu muhimu.

Kimenya alisema wanaiona Simba ni timu ya kawaida kama zilivyo nyingine kwenye ligi, hivyo watacheza kwa nidhamu kuhakikisha wanautumia vyema uwanja wao.

“Inawezekana kuifunga Simba kwani tumewahi kuifunga, ingawa tunatambua kwamba wana nia ya kutetea ubingwa wao, hivyo watakuja kwa ushindani utakaofanya mechi iwe nzuri,” alisema.

“Mechi itatawaliwa na ufundi, mbinu ambavyo ndivyo vitakavyoamua nani mbabe ndani ya dakika 90 siku hiyo, hivyo tunaendelea kuhamasishana kuelekea mchezo huo.”

Beki wa Prisons, Benjamin Asukile amesema kuwa Simba imewazidi ubora wa mchezaji mmojammoja, lakini kitimu hawakiwezi kikosi chao.

“Itakuwa mechi ngumu. Tunawaheshimu Simba ni timu kongwe na ina wachezaji wazuri. Kikosi cha Simba ukikiangalia kwa mchezaji mmojammoja wako vizuri ila kitimu sisi tumewazidi, hivyo tunawasubiri uwanjani na dakika 90 zitaamua,” alisema.

Asukile alisema mchezaji anayemkubali na kumhofia Simba ni kiungo Clatous Chama ambaye amekiri ni mtulivu uwanjani na ana madhara makubwa kama asipodhibitiwa vizuri.

Kwa upande wa mshambuliaji, Lambart Sabiyanka alisema mechi yao na JKT Tanzania itakuwa kipimo sahihi kuelekea kucheza na Simba, ingawa alikiri kutakuwa na changamoto ya wao kuchoka na safari.

“Akili zetu kwa sasa zinawaza mechi na JKT Tanzania ambayo imetoka kupoteza mechi mbili dhidi ya Simba na Ruvu,” alisema.