Wabongo wanaokipiga majuu wacharuka

Tuesday June 11 2019

 

By Eliya Solomon

MATUKIO ya kibaguzi kwa wanamichezo yamekuwa yakipigwa vita kwa kiasi kikubwa. Mwaka jana shirikisho la soka Italia lilitoa adhabu kwa mashabiki wa Inter Milan kutoingia kwenye mechi mbili za timu yao kutokana na kufanya vitendo vya kibaguzi.

Mashabiki wa Inter walifanya vitendo hivyo dhidi ya Kalidou Koulibaly wakati wa mechi ya Ligi Kuu ya Italia ‘Serie A’, Desemba 26 mwaka jana ambapo Napoli walilala 1-0 huku beki huyo akipagawa na mwishowe kutomaliza mchezo huo kwa kuonyeshwa kadi nyekundu.

Ukiachana na tukio hilo la ubaguzi lililomkumba beki huyo wa Napoli kutokea Afrika, wapo nyota wa Kitanzania ambao na wenyewe wamekumbana na matukio tofauti ya ubaguzi wa rangi wakiwa katika majukumu yao ya uchezaji soka.

Michael Lema - Austria

Mshambuliaji kinda wa Kitanzania, Michael Lema anasema akiwa na kikosi B cha Sturm Graz ambacho alikuwa akikichezea kwenye Ligi Daraja la Tatu, Austrian Regionalliga, aliwahi kutupiwa ndizi.

Lema anasema alichokifanya ni kuiokota na kwenda kwenye benchi lao la ufundi na kumuomba rafiki yake amhifadhie akiwa na kusudi lake, baada ya muda kinda huyo wa Kitanzania akapachika bao.

Advertisement

“Nilivyofunga tu, nilikienda kuchukua ile ndizi na kwenda upande ule ule na kumenya na kuanza kuila, niliwaacha hoi tangu siku hiyo sijawahi kukutana na tukio lolote la ubaguzi,” anasema Lema.

Emily Mgeta – Ujeruman

Beki wa zamani wa Simba, Emily Mgeta ambaye kwa sasa anacheza soka la kulipwa Ujerumani anasema ubaguzi nchini humo “upo wa chini kwa chini, unaweza kupita sehemu unakuta mtu anakuzomea kwa sauti ya nyani.”

“Kabla ya kuja huku niliambiwa kuwa kuna ubaguzi, isitoshe nimekuja kutafuta maisha. Kwa hiyo mengine naona ni kama mambo ya kawaida kwa sababu wanachofanya hakinikwamishi kwenye mambo yangu,” anasema beki huyo wa VfB Eppingen.

Said Mhando - Italia

Mhando ambaye ni mzaliwa wa Italia, anasema nchini humo ambako amezaliwa na kukulia ameanza kukutana na ubaguzi tangu akiwa na mdogo kwa hiyo siyo kitu kipya kwake japo amekuwa akichukizwa nacho.

Kiungo huyo ambaye yupo kwa mkopo Cuneo akitokea Ascoli ya Serie B, anasema kuna kipindi alikuwa na mawazo ya kwenda mbali ambapo atakuwa huru na maisha yake.

“Nilitathimini hilo na kupata ufumbuzi kuwa siwezi kutatua tatizo kwa kulikimbia, nawajibika kuwa mstari wa mbele kupambana kwa kupinga ubaguzi,” anasema Mhando.

Amahl Pellegrino - Norway

Mshambuliaji wa Strømsgodset ya Norway, anasema asili yake ya mchanganyiko wa Mwarabu, imekuwa ikimweka mbali kubaguliwa, nyota huyo ambaye ni Mtanzania anadai vinginevyo angekuwa akishikana mashati wa wabaguzi nchini humo.

Pellegrino anasema yeye hana uvumilivu na kama angekuwa anakutana na mtu yeyote ambaye anaonyesha vitendo vya ubaguzi basi wangekuwa wanamalizana papo hapo.

“Yani huyo mtu atanipiga au nimdunde kwa sababu siwezi kufanyiwa unyama wa namna hiyo, sipendi dharau na mtu anapofanya ubaguzi ni kama anakutusi kitu ambacho kwangu siwezi kukiruhusu,” anasema.

Zakaria Kibona - Finland

Mtambo wa mabao wa IF Gnistan ya Daraja la Pili Finland, Kibona anasema amezoea vitendo vya ubaguzi nchini humo ambavyo amekuwa akikuambana navyo, kikubwa huwa anachukulia kama sehemu ya changamoto kwenye utafutaji wake maisha.

“Kuna kipindi ubaguzi utapotea na haiwezi kuwa leo wala kesho, itachukua muda. Kikubwa kinachotakiwa kufanyika ni kuendelea kupiga vita vitendo hivyo visivyofaa, nadhani kuna haja ya kutungwa kwa sheria kali juu ya vitendo hivyo,” anasema mkali huyo wa kucheka na nyavu.

Advertisement