Vita ya makipa yaanza upyaaa

Saturday August 17 2019

 

By Yohana Challe

HAKUNA ubishi msimu uliopita katika Ligi Kuu Bara kulikuwa na makipa watatu bora Aishi Manula wa Simba, Nurdin Barola (Biashara United) na Aaron Kalambo (Prisons), huku Juma Kaseja akiwafuata kwa mbali, lakini msimu huu ni kama vita inaanza upya.

Barola na Kalambo wameachana na timu zao za msimu uliopita na kutua Namungo na Mbeya City, na kinachosubiriwa kuona kama wataenda na kasi yao dhidi ya Manula ama la, ila ongezeko la makipa ndani ya ligi hiyo linachochea ushindani zaidi msimu huu.

Farouk Shikhalo kutoka Kenya ni moja ya ingizo jipya huku kukiwa pia na Razack Abarola wa Azam, Metacha Mnata wa Yanga ni moja ya sababu ya vita ya msimu huu kuwa kubwa.

Juu ya vita hivyo kipa Barola aliyetua Namungo amefunguka kuwa anataka kuonyesha umahiri wake msimu huu akieleza kwamba amepanga mambo makubwa kwa timu hiyo yenye maskani yake Ruangwa mkoani Lindi.

“Nimepanga kufanya makubwa msimu huu na haina ubishi kila kitu kitaonekana uwanjani, na sio sehemu nyingine ambayo mchezaji anaweza kudhihirisha ubora wake na hapo itajulikana nani bora zaidi, kwani kila mchezaji ana malengo yake baada ya mwisho wa msimu awe ameyafikia na ndilo nimelipanga kwa sasa na kwa wakati huu,” alisema.

Msimu uliopita Barola aliiwezesha timu yake kumaliza nafasi ya 14 kwenye ligi, licha ya kufungwa mabao 35 kwani haikumzuia kuwa miongoni mwa makipa bora watatu wa Ligi Kuu.

Advertisement

Kuhusu ushindani wake na Manula, alisema anamkubali kutokana na uwezo wake, lakini changamoto hiyo ndio inayompa nafasi ya kuendelea kukazana na kubaki kwenye kiwango kizuri na kuwa miongoni mwa walinda mlango wazuri.

Barola anakumbwa kwa mikasa yake uwanjani hasa ule wa kuvimbiana na kocha wake, Amri Said akiwa Biashara kwenye mchezo wa Kombe la FA, Uwanja wa Taifa wakati timu hiyo ikitolewa kwa mikwaju ya penati baada ya sare ya mabao 2-2.

“Hakuna lolote juu yangu na Kocha Said, kwani ni kama watoto na mzazi wake, hivyo alinisamehe na tunaongea vizuri na hakuna baya linaloendelea baina yetu, kwani kwenye soka mambo kama hilo ni kawaida kutokea,” alisema Barola.

Advertisement