Vipi ukijiandiskisha tu unapata mzigo? daftari lisingetosha

Tuesday October 15 2019

 

By Luqman Maloto na Dk Levy

EBWANA Eeeh! Watu wachache wamejiandikisha mpaka sasa kwenye daftari la kupiga kura uchaguzi wa serikali za mitaa. Shida ni uchaguzi au aina ya uhamasishaji?

Wangeambiwa vituoni ukijiandikisha unapewa video mpya yaya yule mwanadada bure, vituo visingefurika kweli? Wabunge wa kijiweni, Luqman Maloto na Dk Levy wana kazi na wewe.

LUQMAN: Daktari Levy, mtu mwenye koneksheni zako mjini.

DK LEVY: Kabisa hujakosea somo. Bila hayo makitu utaishi kwa shida sana mjini. ‘Koneksheni’ ni zaidi ya ubunge na uwaziri.

LUQMAN: Sawa ndugu mheshimiwa wa koneksheni, ni mzigo gani unatrend mjini kwa sasa?

DK LEVY: Hamna kitu. Uliopo haujafikia ubora ule wa Mariam Birian. Hapo sijamtaja Amber Rutty... Huu wa sasa wa kibwege tu...

Advertisement

LUQMAN: Hujamtaja mchunga kondoo wa Bwana, kwani yake haizungumziki?

DK LEVY: Nilikuwa nakupima kuona kama na wewe una ‘koneksheni’? Kumbe upo vizuri. Pia kuna Maadam Tz Sweet Heart. Lakini wote hawana viwango vya Mariam Biriani na Amber Rutty. Kifupi acha kuwafananisha Amber Rutty, Mariam Birian na vitu vya kijinga. Wale ndo konki konki konki mastaa.

LUQMAN: Shida ni Menina au Mwijaku? Natambua wewe ni mchambuzi hodari wa hayo madude.

DK LEVY: Sikatai kwenye hili. Shida ni kwa wote pamoja na sisi. Lakini pia imetupa picha kamili kwamba usichanganywe na mashepu ya Instagram. Kumbe ndani kuna mabuja kama ya ugali unaochemka jikoni au Akachube Road. Kuhusu Mwijaku ameturahisishia kujua upeo wake kwamba ni mfupi kama kivuli cha saa sita mchana.

LUQMAN: Mabuja una maana ugali uliopikwa vibaya? Una mabonge mabonge. Unga katikati ya ugali. Ndio unamaanisha?

DK LEVY: Una akili sana ndo maana unanielewa haraka sana kijana. Na kosa letu sisi baadhi ya mashuhuda eti wanamshirikisha Mungu kwenye vitu vya kipuuzi. Niliona wadada flani mtandaoni eti wanasema “pole sana Menina, muombe Mungu tu haya yote yatapita.” Wanaosema hivyo ni madem. Wanaacha kumuombea mke wa Mwijaku, wanamuombea mwizi wa mume wa mtu. Aliyeshirikiana na mume wa mtu ‘mpuuzi’ kutengeneza ‘shoti muvi’ na kuisambaza makusudi. Mchawi wa dem ni dem. Kama kweli mwalimu wao ni kipofu basi mwalimu wao pia atakuwa dem.

LUQMAN: Kwani wanawake wamewahi kuhurumiana? Hapo wanampa pole Menina, pembeni wanamcheka. Halafu mke wa Mwijaku naye wanamcheka kuporwa mume. Kisha wanamvizia Mwijaku ili warekodi mzigo mpya. Mademu wa mjini huwa unawakubali wewe tu.

DK LEVY: Hawa wenzetu sijui waliumbwaje. Hamisa Mobetto walimuunga mkono kumpora Zari sukari yake Mondi. Ajabu ni kwamba hao hao madem wa mjini ‘wakammaindi’ Lulu kujiweka kwa Majizo kwa madai kuwa kampora Hamisa Mobetto. Hamisa akapora mwanaume mwingine wa mtu wakamuunga mkono, halafu wakammaindi Kajala kumpora Wema yule ‘Pedeshee Honga Honga’ wake. Madem huwezi kujua wanataka nini na hawataki nini. Tuishi nao kwa akili tu.

LUQMAN: Pamoja na koneksheni zako zote, hutapata ya Salama Jabir. Hutaambulia ya Lady Jaydee. Kuna wanawake wapo kwenye tasnia, huthubutu kuwaletea utani.

DK LEVY: Kwanza sio mikato yangu. Pili hawana swaga. Hata kama nikipata ‘koneksheni’ binafsi ‘nitaidiskonekti’ ili nisiione. Tatu kile ni kizazi cha Mkapa wanawaza kuwekeza zaidi. Wenye haya madude ni wale wa ‘doti komu’ kizazi cha Mkwere. Wanaowaza bata muda wote utadhani walizaliwa disko au kaunta za bar.

LUQMAN: Kama ni kizazi cha Mkwere, mbona siku hizi ndio wamezibuka? Hakuna ishu ya kizazi cha mtu hapa, ni akili zao mbofumbofu.

DK LEVY: Kizazi cha Mkwere ndo chenye matukio ya Kiamber Rutty na Kimariam Birian. Huelewi nini? Au na wewe umetumwa uje kunichafua kisiasa? Kwanza umejiandikisha kweli wewe?

LUQMAN: Wahamasishaji wa daftari la mpigakura katika Serikali za Mitaa wanakosea ‘tyuni’. Wangetangaza ukienda kujiandikisha unaungwa kwenye koneksheni ya kutazama mzigo mpya wa Menina, Mariam Birian, Irene Uwoya, Nandy, Wema. Ungeona vituo vingejaa. Badala ya kutumia ujanja mdogo huo, viongozi wanatisha watu.

DK LEVY: Ili kuwe na mafuriko zaidi wangesema ukijiandikisha unapata bando la nguvu za kiume. Wenyewe ndo wangekosa nafasi ya kuandikisha watu. Kuna watu wangejiandikisha mara tatu tatu. Kifupi raia ndo wangekuwa wanaandaa ofisi ya mtendaji na kukesha hapo hapo.

LUQMAN: Kuna babu nilikutana naye Jumapili usiku, nikamuuliza, umejiandikisha? Naye akaniuliza, kwani ukijiandikisha unapewa koneksheni ya Irene Uwoya? Anadai ile koneksheni ya Uwoya ilikuwa ya kibabe sana. Ilitangazwa lakini hajainasa mpaka leo.

DK LEVY: Na kuna mama mmoja nilimuuliza kama kajiandikisha, akauliza kwani ukijiandikisha unapata ‘folowazi’ wangapi? Nikachoka kabisa. Mitandao imekuja na kuondoa akili zetu vichwani. Kama serikali ingejua mapema ingetumia ‘peji’ za umbea kule insta kuhamasisha watu. Maana huko ndo watu wako bize nako kuliko hizi kelele za majukwaa ya siasa. Watu wazima na watoto wanafuatilia penzi la Dangote na Tanasha kuliko taarifa za habari.

LUQMAN: Pierre Liquid angetangaza atamvalisha pete ya uchumba Wema Sepetu kwenye kituo cha kuandikisha wapigakura, hicho kituo kingetosha?

DK LEVY: Achana naye huyo. Wangesema tu kuwa ukijiandikisha utapewa nguvu ya kubet ligi kuu yote ya Uingereza vituo vyote vingekesha vikiandikisha. Habari ya mjini kwa sasa ni kubet tu.

LUQMAN: Kwani kubet kunahitaji nguvu? Wangetangaza ofa ya ukijiandikisha kwenye daftari la uchaguzi Serikali za Mitaa, unapewa msamaha wa Cybercrime, kupiga, kutuma au kufowadi picha na video za ngono mwaka mzima bila kushitakiwa. Kuna ambaye asingejiandikisha?

DK LEVY: Pia wangesema ukijiandikisha unaruhusiwa kulewa hata siku ya kazi. Wenye bar wauze usiku kucha. Dadapoa hawataguswa wafanye kazi yao kwa uhuru. Pia wangesema makondakta na madereva wa daladala wakijiandikisha wataruhusiwa kuua ruti, kuchepuka na kuwatukana trafiki ikibidi kuwatandkka makofi. Ungeona vituo vinavyojaa.

LUQMAN: Hii nchi yetu inapenda mambo ya ujingaujinga sana. Watu hawachagui viongozi serikali za mitaa, ila yakiwafika ndio wanakimbilia. Wengine kutafuta barua za utambulisho ili waweze kutambulika kwa waajiri wao au kudhamini ndugu zao mahakamani. Wanandoa wakivurugana usiku wanakimbilia ofisi za serikali za mitaa, wakati wa uchaguzi wanajificha. Akili zipo kweli? Mtaa wa kwako, hutaki kuchagua viongozi wanaostahili kuongoza. Halafu baadaye unaongea kwa sauti ya puani “huu mtaa una viongozi wa hovyo”. Siku tatu za ofa zinaisha kesho, hebu watu wakajiandikishe, waache uzezeta wao.

Advertisement