Vijana, Savio mechi ya kibabe RBA

Muktasari:

Pazi ilichomoza na ushindi mwembamba wa pointi 54-52 Jumanne iliyopita matokeo yaliyoipandisha hadi nafasi ya tano kwenye msimamo huku Oilers ikishuka hadi nafasi ya 11, JKT ikiongoza ikifuatiwa na ABC na Kurasini Heat ni ya tatu.

MASHABIKI wa mpira wa Kikapu wanahesabu saa kushuhudia mchezo wa wakongwe wa Ligi ya Mkoa wa Dar es Salaam (RBA), Savio dhidi ya Vijana.

Timu hizo ambazo msimu uliokwisha zilicheza fainali na Savio kufungwa katika mechi mbili kwa moja na Vijana kutwaa ubingwa zitakutana kwa mara ya kwanza msimu huu kwenye Uwanja wa Bandari, Kurasini.

Timu hizo zitakutana kila moja ikiwa na historia ya kufungwa mechi mbili msimu huu wa RBA unaochezwa raundi moja tofauti na msimu uliopita ambapo ilichezwa raundi mbili.

Vijana itacheza mechi hiyo ikiwa ni ya nne katika msimamo baada ya kucheza mechi sita na kushinda nne, Savio yenyewe ni ya nane ikiwa imecheza mechi tano na kushinda tatu.

Mechi nyingine za kesho Jumatano Julai 29, 2020, Chui itacheza na ABC wakati Mgulani JKT itaikabiri Polisi.