Vichwa vitano nyuma ya Ed Woodward Man U

Thursday February 13 2020

Vichwa vitano nyuma ya Ed Woodward Man U,MANCHESTER United, Ed Woodward, Angel Di Maria, Radamel Falcao, Paul Pogba, Alexis Sanchez, Romelu Lukaku,

 

MANCHESTER, ENGLAND . MANCHESTER United ikizingua kwenye usajili mtu wa kwanza kulaumiwa ni Makamu wa Rais Mtendaji, Ed Woodward, ndiyo maana haikuwa ajabu kuona nyumba yake ikivamiwa na baadhi ya mashabiki mwishoni mwa Januari.

Tangu kuondoka kwa David Gill mwaka 2013, Woodward ametumia Pauni 900 milioni kwenye usajili tu, lakini bado Man United imeendelea kufanya vibaya, licha ya kusajili mastaa kama kina Angel Di Maria, Radamel Falcao, Paul Pogba, Alexis Sanchez, Romelu Lukaku na wengine wengi.

Wakati Woodward akiendelea kuwa mbuzi wa kafara kwa kufeli Man United, si vibaya kuangalia vichwa vitano ambavyo viko nyuma yake katika masuala ya soka na usukaji wa kikosi.

MATT JUDGE MKUU WA MASUALA YA UTAWALA

Kama alivyo Woodward huyu jamaa naye hana historia kubwa kwenye soka, sehemu kubwa ya maisha yake ameyatumia kwenye masuala ya benki kama bosi wake, lakini pamoja na kutokuwa na uzoefu wa kutosha kwenye soka Judge ndiye ana jukumu la kupatanisha dili zote za usajili Old Trafford.

Judge pia amesoma Chuo Kikuu cha Bristol kama Woodward, na tangu mwaka 2016 amekuwa na jukumu la kupatanisha usajili, kuandaa mikataba ya wachezaji na hata wakala akitaka kumpeleka mchezaji wake Old Trafford lazima awasiliane na jamaa huyu kwanza.

Advertisement

JIM LAWLOR SKAUTI MKUU

Huyu ana uzoefu wa kutosha kwenye masuala ya soka, Lawlor amekuwa Man United tangu mwaka 2005. Huyu jukumu lake ni kukaa na Solskjaer, Judge, Mick Court na Marcel Bout kujadili kuhusu usajili kabla ya kuruhusu mchezaji kusajiliwa Man United. United ina maskauti 50 duniani kote wenye jukumu la kutambua vipaji na Lawlor ndiye mkuu wao.

Mfano kabla ya kumsajili Aaron Wan-Bissaka, Man United ilikuwa na majina ya mabeki wa kulia 804 kutoka kila kona ya dunia, orodha hiyo ikachujwa na maskauti wa kikosi cha kwanza 33 kupata majina 50-70, ambayo hupunguzwa na kubaki 10, kisha matatu, hao watatu video zao zinachambuliwa na hatimaye anachaguliwa mmoja wa kusajiliwa.

MICK COURT SKAUTI MKUU WA UFUNDI

Court amekaa Old Trafford kwa miaka 11, lakini ni Aprili mwaka jana tu alipandishwa na kupewa nafasi hiyo ya skauti mkuu wa ufundi, akiwa na timu yake ya wachambuzi wanne wazuri ndio ana jukumu la kupunguza majina hadi kubakiza machache yanayoweza kujadilika.

Majina hayo huwa matatu na hupangwa kwa kipaumbele kisha kupelekwa kwa Solskjaer na timu ya usajili, hawa ndio huwa na jukumu la kukubali kama mchezaji asajiliwe au la.

Hawa wana mamlaka ya kupinga usajili wa mchezaji kufanyika. Na hilo likitokea Woodward huwa na jukumu la kuzungumza na kocha kumshawishi.

JOHN MURTOUGH MKUU WA MAENDELEO YA VIJANA

Murtough ana jukumu moja kubwa nalo ni kupandisha vijana wenye vipaji kutoka kwenye akademi ya timu kwenda kwenye kikosi cha kwanza - nafasi hii aliipata mwaka jana.

Kitengo chake ndicho kimechangia kupatikana kwa mastaa kama akina Marcus Rashford, Jesse Lingard, Scott McTominay, Brandon Williams na Mason Greenwood katika siku za karibuni. Kwa hiyo jamaa yupo kwa ajili ya kuimarisha timu kutokana na wachezaji wa akademi.

MARCEL BOUT MKUU WA MASKAUTI WA NJE

Huyu Bout ni mtu wa mpira kwelikweli, amewahi kufanya kazi katika klabu za Feyenoord na AZ Alkmaar, kabla ya kuchukuliwa na Louis van Gaal kama kocha msaidizi wakati akiwa Bayern Munich. Mwaka 2014 aliajiriwa Man United kama kocha msaidizi mwenye jukumu la kuwachambua wapinzani.

Mwaka 2016 baada ya Van Gaal kutimuliwa yeye alipandishwa na kuwa Mkuu wa Maskauti wa Nje, akiwa na jukumu la kuunganisha Maskauti 50 wa Man United kutoka kila kona duniani, ni Bout ndiyo huwa anatoa uamuzi wa mwisho pale anapopatikana kinda mwenye kipaji.

Advertisement