Van Dijk muosha madishi aliyegeuka mfalme Liverpool

Saturday July 25 2020

 

By Mustafa Mtupa

BREDA, UHOLANZI. KUNA mengi yaliyopo nyuma ya mtu aliyefanikiwa, jina la Virgil van Dijk wala sio geni kwako, hii ni kutokana na kiwango chake alichokionesha kuanzia akiwa na klabu ya Liverpool na hata timu ya Taifa ya Uholanzi.

Lakini unajua kuwa huyu ni mmoja wa wachezaji aliyeonekana mzigo sana kwenye timu ya Willem II ambayo ndio alianza kucheza soka akiwa bado kijana mdogo kabisa, hapa alijaribu kuonyesha kila alichokuwa nacho lakini aliishia kuambulia kuwa sehemu ya timu ya vijana na kuosha madishi tu.

Virgil Van Djik ni nani?

Virgil van Dijk alizaliwa Julai 8, 1991, huko Breda, nchini Uholanzi. Baba yake anajulikana kwa jina la Ray Van Dyke na mama yake ni Ruby Van Dyke.

Wakati yupo kijana mdogo, alikuwa anatengwa na kusemwa sana  kutokana na aina yake ya uchezaji, muda mwingi kuwa anacheza taratibu, hii ilitokana na matatizo ya kiafya aliyokuwa nayo wakati huo, Van Djik alikuwa anasumbuliwa na tumbo ambapo alipata nafuu baada ya kufanyiwa matibabu.

Lakini mpaka sasa ana makovu chini ya tumbo lake yaliyotokana na matibabu hayo na bado amekuwa akisumbuliwa na maradhi hayo mara kwa mara.

Advertisement

Baada ya kupona kabisa, ndio safari ya kujaribu tena bahati yake ilianza, wakati anacheza mpira  mitaani tu na mabonanza, pamoja na kufanya kazi ya kusafisha mabeseni klabu ya Willem II akiwa kijana mdogo.

Safari yake katika soka

Alianza safari yake ya soka Willem II baada ya kuwa muosha madishi kwa muda wa miezi kadhaa aliomba nafasi ya kujiunga na timu yao ya vijana ambapo alikubaliwa.

Wakati anaanza kucheza alianza kucheza kama beki wa kulia mpaka kufikia mwaka 2008, alipokuwa na umri wa miaka 17, na kuongezeka urefu kwa sentimita 18 zaidi.

Lichaya kuongezeka kimo na umri bado hakuwahi kuaminiwa na kuingizwa kwenye kikosi cha kwanza, mmoja wa makocha wa kikosi cha Willem II, Edwin Hermans alinukuliwa akisema kuwa Van Djik  ni mchezaji ambaye hawezi kukupa vitu vingi anapokuwa uwanjani  hivyo hawezi kabisa kupandishwa kikosi cha wakubwa.

Maisha ya dhiki na manyanyaso yaliendelea  ndani ya Willem hadi mwaka 2010 ambapo mmoja wa Maskauti kutoka FC Groningen, Martin Koeman  aligundua  Van Dijk ni mchezaji mwenye  kipaji, na  akaratibu mchakato  wa kumepeleka timu ya vijana ya Groningen ndani ya mwaka huo.

Akiwa hapo mambo yalizidi kuwa magumu baada ya kuwa anasemwa sana kama ni mchezaji anayechoka awapo uwanjani hali inayopeleka kuigharimu timu, lakini kufikia Mei 1, 2011 alibahatika kucheza mechi yake ya kwanza ya kimashindano ndani ya Ligi Kuu Uholanzi, baada ya kuingia dakika ya 72 katika ushindi wa  4–2 dhidi ya ADO Den Haag.

Mei 29 pia alianza kwenye kikosi cha kwanza na  kufunga bao lake la kwanza la kimashidano katika mchezo wa  kufuzu michuano ya  UEFA Europa League kwenye ushindi wa bao 5-1.

Katika msimu huo wa 2011/12 ndani ya Ligi Kuu nchini Uholanzi Van Dijk alicheza jumla ya michezo 23, huku bao lake la kwanza la Ligi Kuu akifunga katika ushindi wa 6–0  dhidi ya Feyenoord Oktoba 2011.

Lakini baada ya hapo alikumbana na maradhi ya peritonitis, pamoja na kuripotiwa kuwa na sumu kwenye figo yake moja hali hiyo iliyopelekea madaktari kutoa taarifa yakuwa kuna ana asilimia 40 za kuishi na 50 za kufa wakati anaenda kutibiwa.

Alifanikiwa kupona, baada ya hapo aliendelea na maisha yake ndani ya Groningen mwishoni mwa msimu, Juni, 2013 akasajiliwa kwenda Celtic ambapo alibahatika kushinda mataji mawili ya Ligi Kuu nchini Scotland msimu wa 2013/14, 2014/15 na taji moja la ligi msimu wa 2014/15.

Septemba mwaka 2015 akasaini mkataba wa miaka mitano kuitumikia Southampton kilichokuwa chini ya Ronald Koeman. Kwa ada ya Pauni 13 milioni ambapo  mwaka 2016 akaongeza mkataba mwingine wa miaka sita zaidi.

Kiwango chake kilionekana kumvutia sana Jurgen Klopp na January, 2018 akasaini Liverpool kwa ada ya uhamisho ya Pauni 75 milioni na kumfanya avunje rekodi ya usajili kwa upande mabeki. Celtic ilipata asilimia 10 ya kiasi hicho.

Mechi yake ya kwanza ndani ya Liverpool ilikuwa ni dhidi ya Everton katika mchezo wa FA na alifunga bao la ushindi. Timu ya Taifa amecheza michezo 33 na kufunga mabao manne.

Tuzo, maisha binafsi na bata

Mchezaji bora wa Celtic 2013/14, Mchezaji bora wa msimu wa Southampton 2015/16, mchezaji bora wa msimu ndani ya Liverpool 2018/19, beki bora wa UEFA 2018/19, mchezaji bora wa msimu ndani ya EPL 2018/19, PFA 2018/19.

Akiwa na Liverpool ameingia fainali mbili mfululizo za UEFA na kufanikiwa kuchukua mara moja msimu wa 2018/19. Na pia walichukua UEFA Super Cup mwaka 2019, pamoja na FIFA Club World Cup mwaka huo huo.

Yupo kwenye ndoa na mchumba wake wa utotoni, Rike Noitgedagt, mpaka sasa wamezaa mtoto mmoja aitwaye Nila, kuhusu bata jamaa sio mtu wa bata sana japokuwa wakati anachezea Celtic alikutana na skendo za kuchepuka na mwanadada wa Kiscotland.

Advertisement