VIDEO: MO arudisha tabasamu kwa wadau wa michezo nchini

Muktasari:

Mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ amekuwa akijihusisha na masuala ya michezo na sasa anakaribia kununua hisa asilimia 49 za klabu ya Simba

Dar es Salaam. Wadau michezo nchini wamepokea kwa shangwe taarifa za kupatikana kwa mfanyabiashara na mdhamini wa Simba, Mohammed Dewji 'MO'.

MO alitekwa siku tisa zilizopita akiwa anakwenda mazoezini amepatikana usiku wa kuamkia leo Jumamosi maeneo ya Gymkhana, Dar es Salaam.

Akizungumzia suala hilo Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la soka Tanzania (TFF), Fredrick Mwakalebela alisema kupatikana kwa MO kutaleta chachu ya maendeleo kama ilivyokuwa awali.

"MO katika soka si Simba tu bali ni muhimu katika soka la nchini nzima kutokana na anavyofanya au kujitolea katika maendeleo ya soka kurudi kwake akiwa mzima ni faraja kwa nchini haswa upande wa michezo," alisema Mwakalebela.

Kocha msaidizi wa timu ya Taifa ya wanawake Twiga Stars, Edna Lema alisema kurudi kwa MO kumerudisha furaha kwa mashabiki na viongozi wa soka wote hapa nchini.

Anasema alivyokosekana wachezaji wa Simba hata viongozi wa klabu hiyo hawakuwa vizuri kisaikolojia kama vile baba amekosekana katika familia.

"Kurudi kwake kutaongeza morali kwa wapenzi wote wa soka hapa nchini haswa wa Simba na hata wachezaji wa klabu hiyo watakuwa katika hali na mudi ya kushindana," alisema Lema.

Kocha wa makipa wa timu za vijana Tanzania, Peter Manyika alisema watu wote tulikuwa tunaomba arudi salama na imekuwa hivyo tunaomba asiache roho na moyo wake wa kuendelea michezo kwa changamoto hii ambayo amekutana nayo.

“Naimani kurudi kwake wanasimba wote wamefurahi na wamerudi katika moyo wa wa zamani tofauti na alivyokuwa MO alipokuwa amekosekana," alisema Manyika.