VIDEO: De Gea kawaacha watu mdomo wazi

Muktasari:

  • Wataalamu mbalimbali wa soka wamemmwagia sifa kipa huyo namba moja wa timu ya taifa ya Hispania aliyetua Old Trafford mwaka 2011 akitokea Atletico Madrid huku wengine wakidai kwamba kwa sasa ndiye kipa bora zaidi duniani.

LONDON, ENGLAND .LIONEL Messi alifunga bao la 400 katika La Liga juzi Jumapili, Manchester United waliichapa Tottenham 1-0 dimba la Wembley, lakini yote hayo hayakuwa habari ya mjini. Habari ya mjini ilikuwa kipa wa Manchester United, David de Gea.

Juzi De Gea aliwaacha midomo wazi mashabiki wa soka kote ulimwenguni baada ya kuokoa michomo 11 ya hatari kutoka kwa mastaa wa Tottenham na hivyo kuweka rekodi mpya katika historia ya Ligi Kuu ya England.

Michomo hiyo aliyookoa inamfanya De Gea awe kipa wa kwanza katika historia ya Ligi Kuu ya England kuokoa idadi hiyo ya michomo bila ya kuruhusu wavu wake kuguswa.

Wataalamu mbalimbali wa soka wamemmwagia sifa kipa huyo namba moja wa timu ya taifa ya Hispania aliyetua Old Trafford mwaka 2011 akitokea Atletico Madrid huku wengine wakidai kwamba kwa sasa ndiye kipa bora zaidi duniani.

Kocha wa Tottenham, Mauricio Pochettino alidai kipa huyo ndiye ambaye kwa kiasi kikubwa aliwanyima ushindi katika pambano akiokoa michomo ya akina Dele Alli, Harry Kane, Christian Erikssen na wengineo.

“Ilishangaza sana na nadhani De Gea aliokoa michomo 11 kitu ambacho hauwezi kuamini. Katika soka wakati mwingine unastahili kushinda na haushindi halafu mwingine anashinda. Na ndio maana tunapenda soka.” Alisema Pochettino.

Naye mlinzi wa zamani wa Manchester United, Gary Neville ambaye kwa sasa ni mchambuzi hodari wa soka England alimsifu kipa huyo kwa kuokoa michomo mingi huku mingine akiokoa zaidi kwa miguu yake kuliko mikono.

“De Gea ametisha sana. amekuwa bora sana hata kwa kutumia miguu yake, amekuwa akiziba nafasi za wazi na kuokoa kwa miguu. Nadhani viatu alivyochezea (Dhidi ya Tottenham) atavitundika katika kioo baada ya mechi.” Alisema Neville.

Naye staa wa zamani wa Tottenham, Robbie Keane ambaye alikuwa pamoja na Neville wakichambua pambano hilo alidai kwa sasa inawezekana De Gea ndiye kipa bora zaidi duniani huku pia akimsifu kwa kucheza na miguu.

“De Gea hapana shaka ni kipa bora duniani. Unapopiga miguuni anakuwa bora zaidi. Labda wakati mwingine inabidi ubadilike na kupiga juu. Kama ningekwenda katika mechi na kukutana naye huku nikijua kwamba ni mzuri katika miguu labda ningepiga mashuti ya juu kwa nguvu. Unaona mara kadhaa aliokoa kwa miguu. Ni mwepesi na anajua kuipanga miguu yake haraka. Unahitaji kubadlika.” Alisema Keane ambaye enzi zake alikuwa mshambuliaji.

Naye kipa namba moja wa timu ya taifa ya England, Peter Shilton alisifu ubora wa De Gea katika kutumia viungo vyake vyote kuzuia mpira usiitinge nyavuni huku akidai kwamba makipa wamekuwa hawapewi sifa za kutosha pindi timu inapopata ushindi.

“Hakuna shaka United inabidi washukuru ubora wa David De Gea katika ushindi huu. Wakati mwingine makipa hawapewi sifa zinazostahili lakini hakuna ambaye anaweza kuhoji mchango wa De Gea katika mechi hii. Aliokoa mipira 11 katika kipindi cha pili na hakuna shaka kwamba yeye ndiye ambaye alipeleka pointi Old Trafford,” alisema Shilton.

“Kuna njia nyingi tofauti za kulinda lango na mojawapo ni kutumia miguu. Jinsi gani kipa anatumia miguu yake inatokana na wepesi wake katika kuichezesha. David alitumia miguu yake vema lakini mimi wakati nacheza nilikuwa naona salama zaidi kutumia mikono, naamini inakupa umiliki zaidi,” aliongeza Shilton.