Uwanja wa Simba waleta neema Bunju

Muktasari:

Gazeti hili liliweza kuangalia namna ambavyo shughuli nyingine zilivyochukua taswira kubwa baada ya uwanja huo kujengwa pale Bunju.

HAYAWI hayawi sasa yamekuwa imepita miaka mingi mashabiki wa Simba wakisubiria klabu hiyo kuwa na uwanja wake, kwa sasa kiu yao itafikia tamati.

Uwanja wa Simba wa Bunju umefikia hatua nzuri, zimetandikwa nyasi bandia upande mmoja jambo ambalo lililowavuta baadhi ya mashabiki kufika na kuanza kushangaa kinachoendelea, huku baadhi wakishangilia.

Mwanaspoti lilifika Bunju kuangalia maendeleo ya uwanja huo na liliwashuhudia baadhi ya mashabiki wakijipiga picha za kumbukumbu kutokana na timu yao kumiliki uwanja, huku baadhi wakisema ni muda wa kuonana na wachezaji ana kwa ana.

Gazeti hili liliweza kuangalia namna ambavyo shughuli nyingine zilivyochukua taswira kubwa baada ya uwanja huo kujengwa pale Bunju.

UWANJA WAGEUKA UTALII

Presha ya uwanja wa Simba tangu ianze imewafanya mashabiki kuwa na kimuhemuhe wakitaka kuona namna ahadi ya uwanja inavyokamilika.

Gazeti hili lilipofika katika uwanja huo liliwakuta mashabiki wakiwa wengi wakifuatilia kila hatua iliyokuwa ikifanywa katika uwanja huo.

Wengine walikuja na magari yao na kushuka kwenda kupiga picha (selfie) huku wengine wakiwa wanapiga picha ndani ya nyasi bandia. Sura zao zilikuwa zikionekana kujawa na furaha kufuatia timu yao kupiga hatua hiyo.

Mmoja wa mashabiki waliokuwepo uwanjani hapo, Salivatory Michael aliwaomba viongozi wa Simba kuweka taa kwenye uwanja huo ili wawe wanalala uwanjani hapo huku akifurahia hatua waliyofikia.

“Tulisubiria kwa muda mrefu kuona hatua hii ya uwanja kubandikwa nyasi bandia tunaishuhudia kwa macho sasa imekuwa, tunawaomba viongozi waweke taa ili tuwe tunalala hapa hapa,”alisema.

MAMA NTILIE, BODABODA

Kabla ya ujio wa maendeleo ya uwanja huo hakukuwa na sehemu yoyote ambayo ungeweza kupata chakula, lakini sasa sehemu ya kuingia ndani ya uwanjani huo unaweza kupata huduma hiyo na pia ile vinywaji kwa sababu kuna duka la bidhaa hizo.

Duka hilo ni msaada mkubwa kwa mafundi wanatengeneza uwanja huo na pia mashabiki wa Simba wanafika hapo kuangalia maendeleo ya uwanja huo.

Katika hatua nyingine madereva bodaboda wanaendelea kujipigia pesa kutokana na kwamba hakuna daladala linalofika katika maeneo hayo.

Kutoka barabarani mpaka uwanjani, bodaboda hutoza shilingi 300, 2000 hadi 1000 kutokana na uelekeo unatokea ili kufika uwanjani hapo.

Bodaboda wataendelea kunufaika hata baada ya uwanja huo utakapokamilika kwasababu bado mashabiki watakuwa wanaenda kwenye mechi au mazoezi kwa wingi zaidi ya hivi sasa.

AJIRA YAONGEZEKA

Utandawazi unakuja kwa kasi kuhakikisha unaondoa utegemezi wa binadamu pekee kufanya kazi katika eneo husika.

Hilo limetokea katika uwanja wa Bunju wa nyasi za asili kwani licha ya kuwa na vitendea kazi bado watu wamepata ajira/vibarua vinavyowafanya waishi mjini.

Mwanaspoti lilishuhudia wanamama wakiwa wanakata vichuguu ambavyo vimeotea katika nyasi, wamama hao walikuwa hawaongei na mtu yoyote zaidi ya akili zao kuwa bize na ufanyaji wao wa kazi.

MASTAA WASUBIRIWA

Uwanja huu ukikamilika bila shaka Simba wataachana na masuala ya kufanya mazoezi katika Viwanja vya Gymkhana au Boko Veterani. Jambo hilo limewafanya mashabiki kuomba uwanja huo kukamilika haraka ili kuweza kuwaangalia nyota wa kikosi chao kama Meddie Kagere.

Uwanja huu ukikamilika utawafanya mashabiki wasiwe na purukushani za kutoka Bunju na kwenda Boko au Gymkhana kwenda kuangalia mazoezi kwani watakuwa wamesogezewa nyumbani.

WADAU WAUUZUNGUMZIA

Mchezaji wa zamani wa Simba, Emmanuel Gabriel alisema Mohamed Dewji ameandika rekodi ambayo itakumbukwa na vizazi nenda rudi.

Alisema laiti kama angekuwa anacheza anaamini angefanya mambo makubwa akiwataka wachezaji kujitambua na kujiona wamefikia levo ya kimataifa.

“Uwanja wa Bunju uwe wa machinjioni ule wa taifa uwe wa ugenini, ni wakati wa wachezaji wa Simba, mashabiki kujidai kwa kufanya makubwa,” alisema.

Kocha wa zamani wa Stand United, Athuman Bilali ‘Bilo’ alisema walichofanya Simba kinaashiria soka la Tanzania kukua na kila timu ikiwa na uwanja wake ushindani utapatikana,” alisema.