Ushindi Bandari lazima kwa AFC Leopards

Muktasari:

Anasema wanasoka wote wako hali nzuri na atakaowachagua kucheza leo watawajibika kutambua kuwa wako kibaruani kutimiza kazi wanayokusudiwa kuitekeleza. “Alhamisi tutakuwa kibaruani na kwa umoja wetu tunalazimika kuifanya kazi ipasavyo.”

MOMBASA. NI lazima si hiari kwa timu ya Bandari FC kupata ushindi inapokutana na AFC Leopards hivi leo Alhamisi kwenye mechi Ligi Kuu ya Kenya (KPL), ambayo ina umuhimu kwa timu hizo mbili  na itakayochezwa Uwanja wa Mbaraki Sports Club.

Kocha Mkuu Bernard Mwalala amesema kwao leo ni lazima wawachape wapinzani wao wa Leopards kwani hakutakuwa na sababu yoyote itakayokubalika kwao kutoshinda mechi hiyo kwani wamejitayarisha vilivyo baada ya wachezaji kupata mapumziko ya kutosha.

“Sisi maofisa wa benchi la ufundi pamoja na wachezaji wetu tunawajibika kuibuka washindi dhidi ya Leopards sababu tumefanya matayarisho kabambe na wachezaji wote wako hali nzuri ya kucheza soka la hali ya juu na kutoka uwanjani tukiwa washindi,” akasema Mwalala.

Anasema wanasoka wote wako hali nzuri na atakaowachagua kucheza leo watawajibika kutambua kuwa wako kibaruani kutimiza kazi wanayokusudiwa kuitekeleza. “Alhamisi tutakuwa kibaruani na kwa umoja wetu tunalazimika kuifanya kazi ipasavyo.”

Alisema watawajibika kupigana kuanzia dakika ya kwanza hadi dakika ya 90 kuhakikisha wanapata ushindi.

“Leopards iko juu yetu na hivyo tunastahili kushinda pambano dhidi yao ili tuweze kupanda ngazi katika safari yetu ya kuzipiku timu zilizoko juu yetu,” akasema.

Anasema amewaambia wachezaji wake kuwa haitakuwa rahisi kuishinda Leopards katika mechi yao ya ugenini na hivyo akawataka wapigane kuhakikisha timu hiyo ya Nairobi haiondoki na pointi yoyote hivi leo.

Aliambia Mwanaspoti kuwa wanataka kushinda pambano hilo ili kudhihirishia mashabiki wao kuwa zile mechi walizopoteza kabla ya mapumziko ya mechi za kimataifa ni kutokana na uchofu walioupata kwa sababu ya kucheza mechi za kimataifa na kusafiri safari ndefu. 

“Aliwaomba mashabiki wao wajitokeze kwa wingi wawasukume katika kuwashangilia wachezaji wapate nguvu zaidi ya kuwapiku wapinzani wao. “Nina imani kubwa mashabiki wetu watakuja kwa wingi kutushangilia,” akasema Mwalala.