Usajili Simba wamuibua 20% mafichoni

Muktasari:

Akizungumza na Mwanaspoti, 20% alisema soka ni kama muziki akisema wapo wanaopata umaarufu licha ya kuwa na kazi mbovu, huku wengine wenye ngoma zinazobeba ujumbe mzito kwa jamii wakiwa hawana nafasi.

UNAMKUMBUA yule supastaa wa Bongo Flava aliyebeba tuzo tano za Kilimanjaro? Anaitwa Abbas Hamisi a.k.a 20%, ambaye ni shabiki lialia wa Simba, sasa ameibuka na kuupa tano usajili mpya wa klabu yake.

20% ambaye kwa sasa amepotea kwenye gemu ya muziki, amesema kuwa usajili uliofanywa na Simba msimu huu ni wa kisayansi na utakuwa na matokeo mazuri uwanjani.

Pia, amepongeza kazi ya benchi la ufundi katika kuwanoa mastaa hao pamoja na kutambua wako Simba kwa kazi maalumu.

Akizungumza na Mwanaspoti, 20% alisema soka ni kama muziki akisema wapo wanaopata umaarufu licha ya kuwa na kazi mbovu, huku wengine wenye ngoma zinazobeba ujumbe mzito kwa jamii wakiwa hawana nafasi.

Hata hivyo, alisema kwa Yanga na Simba ni lazima wachezaji wanaosajiliwa wafahamike viwango vyao na kwamba, lazima wajue kuupiga mpira mwingi uwanjani.

“Nimekiangalia kikosi cha Simba ni kizuri na cha ushindani na hilo litawafanya wachezaji wasibweteke. Jambo la msingi kazi zao uwanjani ziwe na manufaa kwa timu na kuwapa raha mashabiki na sio kuleta ustaa bila kuonyesha uwezo,” alisema.

Katika wachezaji wa kigeni ambao wamesajiliwa kwa msimu huu, alimtaja Deo Kanda kuwa ni bonge la mchezaji na shughuli aliyoifanya kwenye Simba Day ameikubali. Kwa sasa Simba inajiandaa na michezo ya kimataifa na Ligi Kuu.