Usaili wa wagombea vurugu tupu

Friday December 7 2018

 

By CHARITY JAMES

KAMA unadhani mambo yamepoa katika Uchaguzi Mkuu wa Yanga, pole yako kwani jana Alhamisi nusura watu wazichape.

Si mnajua jana ndiyo ilikuwa usaili wa wagombea wa uchaguzi huo uliopangwa kufanyika Januari 13 mwakani, lakini nusura mambo yatibuke baada ya mabosi wa Yanga kuleta hoja mpya mbele ya Kamati ya Uchaguzi wa TFF.

Ipo hivi. Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya TFF, Ally Mchungahela ameigomea kamati ya Yanga iliyoibuka jana kwenye usaili ikiomba kuahirishwa kwa zoezi la usaili na kutaka zoezi la uchukuaji fomu lianze upya tena kule Jangwani.

Kwa mujibu wa mwakilishi wa Kamati ya Uchaguzi wa Yanga, ambaye ni Mjumbe, Daniel Mlelwa aliyetaka kamati ya TFF iahirishe zoezi hilo na kuomba zoezi la uchukuaji fomu za kugombea nafasi zilizoachwa wazi lianze upya na lifanyikie makao makuu ya klabu yao.

Pia aliomba zoezi hilo lisimamiwe na kamati yao, huku wakitaka mchakato huo ufanyike ndani ya muda uliobaki na tarehe ya uchaguzi ibaki kama lilivyo.

Mlelwa pia aliomba wajumbe wote kuhakikiwa katika matawi yao ili wafahamike kama ni wanachama hai kwa madai kwamba kamati ya TFF haina leja ya wanachama wao.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mchungahela alisema hawakubaliani na hilo na wataendelea na mchakato kama walivyopanga na uchaguzi utafanyika kama lilivyopangwa.

“Mlelwa kaja hapa tena kwa kupigiwa simu, tuliwaandikia barua kikao cha uhakiki wa wagombea waliochukua fomu kugombea nafasi zilizoachwa wazi lakini hawajafanya hivyo,”

“Mkutano tulikubaliana ufanyike saa nne mwakilishi wao amefika hapa saa nane, halafu amekuja na vitu vingine vipya kabisa ambavyo sio tulivyokusudia kuvijadili leo,” alisema Mchungahela.

“Nikiwa kama Mwenyekiti sijakubaliana na hoja yake hata moja, tunaendelea na zoezi letu la usaili kama kawaida na uchaguzi utafanyika kama ilivyopangwa.”

WAGOMBEA WASALIMU AMRI

Mara baada ya mjumbe huyo wa kamati ya uchaguzi ya Yanga, Mlelwa kutaka wagombea wote wahakikiwe matawini, wagombea hao wa Jangwani wamekubaliana na pendekezo hilo kwa afya ya uchaguzi huo.

“Ni maagizo ambayo tumeambiwa tuyafuate, hivyo tutafanyia kazi suala hilo kuhakikisha tunafuata yale wanayoyataka kwa kuhakikisha tunapata viongozi imara,” alisema mmoja wa wagombea ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini.

WALIOFANYIWA USAILI

Katika zoezi hilo la usaili huo, wagombea kadhaa walifanyiwa wakiwamo wale wa nafasi ya Uenyekiti na Makamu Mwenyekiti.

Mpaka Mwanaspoti linaondoka makao makuu ya TFF waliosailiwa walikuwa ni Mbaraka Igangula, Erick Ambakisye wanaowania Uenyekiti, huku Dk. Jonas Tiboroha hakuonekana eneo la tukio.

Katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti waliosailiwa jana ni wawili tu badala ya wanne wanaowania nafasi hiyo.

Waliosailiwa ni Yono Kavela na Titus Osoro, huku Pindu Luhoyo na Salum Chota wakishindwa kutokea.

Wagombea wengine wanaowania nafasi ya Ujumbe wa Kamati ya Utendaji ndio waliokuwa wakifuata, japo ilielezwa zoezi hilo likitarajiwa kuendelea tena leo Ijumaa.

Advertisement