United yarudi upya kwa Koulibaly

MANCHESTER, ENGLAND. HABARI ndo hiyo. Manchester United imeripotiwa kurudi upya kwenye mpango wao wa kumnasa beki wa kati wa Napoli, Kalidou Koulibaly.

Beki huyo Msenegali tangu kwenye dirisha la majira ya kiangazi la mwaka jana amekuwa akihusishwa na Man United, lakini staa huyo alibaki katika kikosi cha Napoli, mahali ambako amecheza mechi 21 msimu huu.

Hata hivyo, Koulibaly kwa sasa anaripotiwa kuwa na mpango wa kuondoka Napoli wakati dirisha la usajili wa majira ya kiangazi litakapofunguliwa na kuna timu kibao zimekuwa zikiripotiwa kutaka huduma yake.

Newcastle United inatajwa kwamba kwa sasa inaongoza kwenye mbio za kutaka saini ya Koulibaly wakiajiandaa kuwa chini ya umiliki wa bilionea wa Saudi Arabia, Mohamed bin Salman, lakini kwa mujibu wa Gazetta dello Sport, Man United wamecharuka na kurudi kwa kasi kwenye mbio hizo za kumnasa beki huyo kisiki wa Simba wa Teranga.

Kinachoripotiwa ni timu hiyo inayonolewa na Ole Gunnar Solskjaer imeweka mezani mkwanja wa Pauni 89 milioni kunasa saini yake, licha ya Napoli kulazimika kushusha bei ya beki huyo kutokana na janga la corona.

Liverpool, Paris Saint-Germain na Everton ni klabu nyingine zilizoonyesha dhamira ya dhati ya kunasa saini ya beki huyo mwenye umri wa miaka 28, ambaye anaweza kupatikana kwa mkwanja wa Pauni 62 milioni tu wa kati dirisha litakapofunguliwa.