Unataka mchezaji wachee? Nenda Barcelona

Thursday June 13 2019

 

BARCELONA, HISPANIA. HUKO Nou Camp kimenuka. Stori ni hii, Barcelona wamepanga kuwapiga mkwasi wachezaji wanane katika mpango wao wa kuondoa mastaa wa hovyo kwenye kikosi hicho baada ya kuboronga msimu uliopita.

Licha ya kushinda ubingwa wa La Liga, kikosi hicho cha kocha Ernersto Valverde kilikumbana na kipigo cha aibu kwenye nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Liverpool licha ya kushinda 3-0 uwanjani Nou Camp na kwenda kuchapwa 4-0 ugenini huko Anfield.

Taarifa nyingine zimedai kwamba huenda wachezaji 11 wakafunguliwa mpango wa kutokea, huku ikielezwa wanane ndio wenye uhakika zaidi baada ya kuonekana ni wa ziada tu katika kikosi hicho.

Wachezaji hao ni Thomas Vermaelen, Jeison Murillo na Kevin-Prince Boateng, ambao mikataba yao imefika tamati mwishoni mwa msimu huu, huku wachezaji ambao watapigwa bei ni Jasper Cillessen, Nelson Semedo, Samuel Umtiti, Ivan Rakitic, Andre Gomes, Denis Suarez, Malcom na Philippe Coutinho.

Taarifa hizo zinazifanya klabu mbalimbali kuzinduka na kuchangamkia fursa ya kuwasajili wakali hao, ambapo Arsenal na Manchester United zimetajwa kwamba huenda zikafanya kweli katika kunasa huduma za wachezaji hao wanaoonekana wamechoka huko Nou Camp.

Advertisement