Ulimboka kujadiliwa kesho TP Lindanda

Thursday July 30 2020

 

By Masoud Masasi, Mwanza

BAADA ya Ulimboka Mwakingwe kuibakisha Daraja la Kwanza timu ya Pamba FC,kamati tendaji ya klabu hiyo kesho ijumaa itakutana kumjadili kama watampa mkataba mpya au watatafuta kocha mwingine kwa ajili ya msimu ujao.

Mwakingwe nyota wa zamani wa Simba alikabidhiwa timu hiyo baada ya kocha Salvantory Edward kuachana na klabu hiyo na yeye kupewa majukumu ya kukinoa kikosi hicho chenye maskani yake wilayani Ilemela.

Kocha huyo aliyejiunga na timu hiyo akitokea Arusha FC alikiongoza kikosi kwenye mechi mbili za hatua ya mtoani dhidi ya Friends Rangers ambapo mchezo wa kwanza walitoka sare ya 1-1 na wa marudiano walishinda 1-0 na kufanya wabaki Daraja la Kwanza msimu ujao.

Hata hivyo kocha huyo alijiunga na kikosi hicho kwa ajili ya kusaidia na Edward kwenye mechi zilizobaki za ligi hiyo hivyo walikubaliana na uongozi huo watafanya mazungumzo ya mkataba mara baada ya mashindano hayo kumalizika.

Akizungumza na Mwanaspoti Online leo Alhamisi Julai 30, 2020 Katibu Mkuu wa timu hiyo Johnson James alisema baada ya kocha huyo kufanya vizuri kwenye mechi hizo mbili na kufanya wabaki daraja msimu ujao wameona jina lake liende kwenye kamati ya utendaji ambayo ndio itakayoamua kama apewe mkataba.

Alisema msimu ujao wa ligi hiyo wanataka kuwa na kikosi bora ambacho kitaleta ushindani kwenye mashindano hayo hivyo watakuwa na sura mpya kwenye timu yao kwani wachezaji sita pekee ndio watakabaki na wengine 21 watasajili wapya.

Advertisement

“Tumeona kazi yake kwenye mechi mbili alizosimamia lakini kesho kamati tendaji itakutana kuweza kujadili ripoti yake kisha kuona kama tunaweza kumpa mkataba kwa ajili ya kukinoa kikosi chetu msimu ujao.

Baada ya hapo ndipo tutaanza mchakato rasmi wa usajili kwani tutashirikiana na kocha na msimu ujao tunataka tuwe na kikosi bora ambacho kitaleta upinzani kwenye mashindano na hatimaye kupanda Ligi Kuu,” amesema James.

Advertisement