Ule 'Utamu' wa Ligi Kuu Bara umerudi tena!

Thursday September 13 2018

 

By Mwandishi Wetu

Dar es Salaam. Ule 'utamu' wa Ligi Kuu Bara kama mabao ya kina Mnyarwanda Meddie Kagere wa Simba na Mkongo Harieter Makambo wa Yanga na 'zengwe' za vijiweni, unaanza tena kesho Ijumaa katika viwanja viwili vya Mwadui Complex na Uhuru na wikiendi ndio itakuwa raha kabisa.

Hii ni baada ya kuwa kwenye mapumziko kupisha mechi za timu za taifa ambazo zinawania kufuzu fainali za AFCON na Taifa Stars ilikipiga na Uganda 'The Cranes' ugenini wakamaliza kwa suluhu.

Katika Uwanja wa Mwadui Complex, Azam FC itakipiga na wenyeji Mwadui FC saa 8:00 mchana na Uhuru, African Lyon itawakaribisha Wagosi wa Kaya, Coastal Union majira ya saa 10:00.

Kocha wa Azam, Hans Pluijm amesema, amekwenda Shinyanga akiwa na kikosi kamili cha ushindi na watarudi na pointi tatu.

 

JUMAMOSI

Mechi za Jumamosi Ndanda FC itawakaribisha Wekundu wa Msimbazi, Simba iliyosafiri wa ndege leo Alhamisi kwenda Mtwara na mchezo utapigwa Uwanja wa Nangwanda Sijaona saa 10:00 jioni.

Lipuli FC itacheza na Mtibwa Sugar Uwanja wa Samora mkoani  Iringa saa 8:00 mchana, wakati  KMC  itakipiga na Singida United Uwanja wa Uhuru muda wa Uhuru saa 10:00 jioni sawa na Mbao FC dhidi ya JKT Tanzania Uwanja wa CCM Kirumba na Tanzania Prisons na Ruvu Shooting, Sokoine.

 

JUMAPILI

Jumapili, Yanga itaikaribisha Stand United  Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam saa 10:00 jioni, muda sawa na wa mchezo kati ya Biashara United itakayoumana na Kagera Sugar mjini Musoma. Mbeya City ambayo ilicheza mechi tatu mfululizo ugenini, itakuwa mwenyeji wa Alliance FC  Uwanja wa Sokoine saa 8:00.