Ukiuziwa Neymar Euro 160m umepigwa mazima

Muktasari:

  •  Sababu zilizoelezwa kushusha thamani ya Neymar ni majeruhi ya mara kwa mara pamoja na utovu wa nidhamu huku akishindwa kufanya kitu cha maana tangu alipojiunga na mabingwa hao wa Ufaransa linapokuja suala la kutamba kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. 

PARIS, UFARANSA. UNAAMBIWA hivi, ukimtaka supastaa wa Kibrazili Neymar kwa sasa wala hupaswi kulipa pesa ndefu, kwa sababu staa huyo bei yake imeshuka huko sokoni.

Kwa mujibu wa CIES Football Observatory, thamani ya Neymar sokoni imeshuka sana tofauti na wakati aliponaswa na mabingwa wa Ufaransa mwaka 2017 kwa ada iliyovunja rekodi ya dunia ya uhamisho ya Euro 222 milioni.

Katika msimu wake wa kwanza kwenye kikosi hicho cha PSG, Neymar alifunga mabao 19 katika mechi 20 alizocheza kwenye Ligue 1, huku kubwa linalodaiwa kushusha thamani yake ni mambo ya nje ya uwanja pamoja na kuumia mara kwa mara.

Januari mwaka huu, gazeti la Hispania, Marca lilidai kwmaba thamani ya Neymar kwa wakati huo ilikuwa Euro 197 milioni, ambapo ilikuwa pesa kidogo sana imeshuka kutoka kwenye kiwango kile kilicholipwa na PSG miaka miwili iliyopita.

Lakini, CIES Football Observatory, ambayo imekuwa ikijihusha na mambo ya kuthaminisha wachezaji, inafichua kwamba thamani ya Neymar kwa sasa ni kati ya Euro 120 milioni na Euro 150 milioniu, ikiwa ni anguko la Euro 77 milioni tangu mwaka huu ulipoingia.

Sababu zilizoelezwa kushusha thamani ya Neymar ni majeruhi ya mara kwa mara pamoja na utovu wa nidhamu huku akishindwa kufanya kitu cha maana tangu alipojiunga na mabingwa hao wa Ufaransa linapokuja suala la kutamba kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Neymar pia amekuwa na matukio mengi ya nje ya uwanja ikiwamo kugombana na mashabiki huku tukio la sasa ni la tuhuma za kubaka jambo linalomfanya wadhamini wake kadhaa kuachana naye, ambapo Mastercard wameanza na huenda Nike na Red Bull wakafuatia. Ripoti za sasa zinamhusisha mchezaji huyo na mpango wa kurudi klabuni Barcelona huku Real Madrid wakimtaka pia.