Ukame wa mabao tatizo washambuliaji Taifa Stars

Wednesday November 13 2019

 

By Eliya Solomon

Dar es Salaam. Washambuliaji saba wa timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ wamefunga mabao manne katika michezo ya ligi mbalimbali ndani ya wiki mbili zilizopita.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na mtandao wa Mwanaspoti kuangalia mwenendo wa washambuliaji wa Tanzania waliotwaa Taifa Stars ni wawili pekee waliofanikiwa kufunga ndani ya siku 14 zilizopita kabla ya kuivaa Equatorial Guinea Ijumaa hii.

Washambuliaji Stars wanaotegemewa kuongoza safu ya ushambuliaji ni pamoja na nahodha Mbwana Samatta KRC Genk ya Ubelgiji na Saimon Msuva wa Difaa El Jadida ya Morocco.

Wengine ni Ayoub Lyanga wa Coastal Union, Eliuter Mpepo wa Buildcon ya Zambia, Ditram Nchimbi wa Polisi Tanzania, Miraj Athuman wa Simba na Shaaban Chilunda wa Azam.

Katika wiki mbili zilizopita ni Samatta aliyefunga mabao

mawili kwanza lilikuwa dhidi ya Antwerp katika Ligi Kuu Belgiji, uliomalizika kwa sare ya mabao 2-2, Oktoba 30 huku mchezo mwingine ukiwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Liverpool, waliopoteza kwa maba 2-1, Novemba 5.

Advertisement

Naye Msuva pamoja na timu yake kuondolewa katika kombe la mfamle kwa kupoteza bao 1-0 dhidi ya timu ya daraja la kwanza, TAS Casablanca amefunga mabao mawili ndani ya wiki mbili ambayo yalikuwa katika mchezo dhidi ya FAR Rabat.

Katika mchezo huo wa Ligi Kuu Morocco ‘Batola Pro’, Difaa El Jadida, anayoichezea Msuva iliibuka na ushindi wa mabao 3-1 wakiwa ugenini.

Mshambuliaji wa Polisi Tanzania, Nchimbi tangu aifungia Taifa Stars bao dhidi ya Sudan katika mchezo wa kusaka kufuzu kwa CHAN ameshindwa kuzifumania nyavu katika Ligi Kuu Tanzania Bara.

Winga wa Simba, Miraj Athumani tangu amefunga dhidi Singida United kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha nyota huyo ameshindwa kuendelea na kasi ya kuzifumania nyavu.

Ukame huo wa mabao umeendelea kwa Ayoub Lyanga wa Coastal Union, Shaaban Chilunda wa Azam pamoja na Eliuter Mpepo wa Buildcon ya Zambia.

Hiyo ni tafsiri tosha kuwa Samatta na Msuva wataendelea kubeba jukumu la kuhakikisha Taifa Stars inapata ushindi katika mchezo ujao wa kuwania nafasi ya kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika Afcon2021 Cameoon dhidi ya Equatorial Guinea na baadaye Libya.

 

 

Advertisement