Ubishi umekwisha

Thursday December 6 2018

 

MANCHESTER, ENGLAND .SASA ubishi kwisha. Kilichotokea kimetokea kuhusu mchezo wa jana Jumatano usiku huko Old Trafford wakati Manchester United ilipoikaribisha Arsenal.

Mechi hiyo ya Ligi Kuu England ilikuwa na mambo mawili, kipimo kwa upande wa Arsenal kuona kama Kocha Unai Emery amekuja kubadili kila kitu kilichokuwa kikifanywa na mtangulizi wake, Arsene Wenger.

Pili ni mtihani kwa Kocha Jose Mourinho na Man United yake katika kuweka mambo sawa baada ya kuyumba kwenye michezo mitatu ya karibuni, akivuna pointi mbili tu. Mchezo huo wa jana ulidaiwa unahusika kwa namna fulani katika usalam wa kibarua cha kocha huyo. Kwenye msimamo kabla ya mechi hiyo, Arsenal iko nafasi ya nne na pointi zake 30 baada ya kushuka uwanjani mara 14, ikishinda tisa, sare tatu na vichapo viwili. Imefunga mabao 32 na kufungwa 18. Man United ilikuwa nafasi ya nane na pointi zake 22 ilizovuna kwenye mechi 14 na imeshinda mara sita tu, sare nne na kichapo vinne, huku ikiwa imefunga mabao 22 na kufungwa 23.

Kwa rekodi hizo za msimu huu, Man United imezidiwa kila kitu na Arsenal. Kilichokuwa kikisubiriwa ni matokeo tu baada ya mechi. Kwa muda mrefu, Arsenal imekuwa wateja wa Man United kwenye mechi za Ligi Kuu England na tangu Septemba 2006, Arsenal haijawahi kushinda.

Imepigwa mara nane na kutoka sare mara tatu. Arsenal mara yake ya mwisho kuifunga Man United ilikuwa kwenye robo fainali ya Kombe la FA, Machi 2015 uwanjani Old Trafford. Hivyo, usiku wa jana ilikuwa mechi ya mambo mawili, kufuta uteja na kuendeleza ubabe. Ilikuwa mechi ya kwanza pia kwa timu hizo kumenyana bila ya makocha wao waliodumu kwa miaka mingi, Sir Alex Ferguson na Wenger. Mara ya mwisho Arsenal ilipocheza bila ya makocha hao ilikuwa Agosti 1986, Arsenal ilishinda 1-0, pale Highbury, uwanja wa zamani wa The Gunners.

Lakini mchezo wa jana ulikuwa wa zama za kizazi kipya. Huko Man United kuna wakali kama Paul Pogba, Romelu Lukaku, Fred, Nemanja Matic, Victor Lindelof, Marouane Fellaini, Marcus Rashford, Jesse Lingard, Anthony Martial na wengineo, wakati huku kwa Arsenal kuna Pierre-Emerick Aubameyang, Alexandre Lacazette, Lucas Torreira, Matteo Guendouzi, Alex Iwobi, Aaron Ramsey na wengine, ambao wapo tayari kufungua kitabua cha historia tofauti.

Alexis Sanchez amekosa fursa ya kuwakabili waajiri wake wa zamani kutokana na kuwa majeruhi, lakini upande wa Arsenal nayo ilimkosa Granit Xhaka na kulikuwa na hatihati kubwa kuhusu Mesut Ozil.

Advertisement