Ubingwa Simba wawaibua Vodacom

Wednesday July 8 2020

 

By Mwandishi Wetu

Mdhamini Mkuu wa Ligi Kuu Tanzania Bara, kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom, imeipongeza klabu ya Simba kwa kutwaa ubingwa wa ligi hiyo msimu huu.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Kitengo cha Biashara wa Vodacom, Linda Riwa imeipongeza Simba iliyoibuka bingwa, timu nyingine shiriki, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kwa msimu uliokuwa na mafanikio.

"Kampuni ya simu za mkononi Vodacom Tanzania, PLC, ambaye ni mdhamini mkuu wa Kigi Kuu ya Vodacom inaipongeza Simba na timu nyingine zilizoshiriki.

Tunajivunia sana kuwa sehemu ya ligi kuu ya Tanzania bara kwani inaendelea kukua na kuboreshwa mwaka hadi mwaka. Pongezi zetu pia ziwaendee viongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), bodi ya ligi, vilabu vyote shiriki, waandishi wa habari, wadhamini wenza pamoja na Watanzania wote kwa ujumla kwa kushiriki kikamilifu katika ligi kuu mwaka huu,"alisema Riwa

Riwa alisema kuwa Vodacom imeamua kuidhamini ligi hiyo kutokana na mchango mkubwa ambao imekuwa ikitoa kuibua na kuzalisha vipaji pamoja na kutoa fursa za ajira kwa vijana.

"Kama mnavyojua mpira wa miguu ni fursa kubwa ya ajira kwa vijana na tunafurahi na kujivunia kuwa sehemu ya mafanikio tunayoyaona kutokana na udhamini wetu ambao umewezesha baadhi ya wachezaji kama Mbwana Samatta na Simon Msuva kupata fursa za kucheza nchi za nje na kufika ulaya.

Advertisement

Mpira wa miguu ni mchezo pendwa na muhimu sana hapa nchini na duniani kote.

Hii ni katika kuwapa burudani wateja wa Vodacom na watanzania kwa ujumla, kutoa nafasi za ajira kwa wachezaji na watendaji pamoja na kujenga umoja na mshikamano miongoni mwa jamii na nchi tofauti." alisema Riwa.

Advertisement