Ubingwa! Yanga ilipoteza hapa

WAKATI Ligi Kuu Bara ilipoanza, Yanga ilikuwa timu tishio dhidi ya Simba, ilishinda mechi mfululizo kabla ya kutibuliwa na Stand United ‘Chama la Wana’ iliowafunga bao 1-0, Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.

Katika mzunguko wa kwanza, Yanga haikupoteza mechi hata moja zaidi ya kudondosha pointi mbili baada ya kutoka sare dhidi ya Ndanda FC na Simba, hivyo ilivuna pointi 55, hilo liliwaaminisha wadau wa soka kuona wana nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa.

Simba ilikuwa kwenye wakati mgumu kwani, ilikuwa imepigwa na Mbao FC, bao 1-0 ilitoka sare na Ndanda pamoja na Yanga, hivyo walikuwa wamepoteza pointi tano.

Yanga ilianza kuondoka taratibu kwenye laini ya ubingwa baada ya kufungwa na Stand United ‘Chama la Wana’ bao 1-0, mchezo uliofuata walitoka sare dhidi ya Coastal Union bao 1-1, kisha wakatoa suluhu na Singida United.

Mpaka sasa imefungwa jumla ya mechi tano, ikiwemo Stand United, Lipuli, Biashara, Mtibwa Sugar na watani wao Simba ambao waliwafunga bao 1-0 mzunguko wa pili.

Pia wametoka sare tano dhidi ya Simba, Coastal Union, Singida United na Ndanda FC kwenye mzunguko wa kwanza na wa pili, huo ndio ukawa mwanzo wa kujitengenezea njia finyu ya kutwaa ubingwa msimu huu.

Yanga imecheza mechi 36, ikashinda 26, kutoka sare tano na kufungwa mechi tano, imepoteza pointi 20, huku wakimiliki pointi 83 na mabao 55, imetikiswa mara 25, huku ikiwa imebakiza michezo miwili mkononi dhidi ya Mbeya City na Azam FC.

Endapo itazifunga Mbeya City na Azam FC, basi itakuwa inamaliza ligi kwa jumla ya pointi 89.

Simba imecheza mechi 34, imeshinda 27 ambazo ni sawa na pointi (81), imetoka sare nne na kufungwa mechi tatu (imepotea pointi 13), hivyo inamiliki pointi 85, imefunga mabao 72 na imetikiswa mara 14.

KAULIZA ZA WADAU

Kocha Kenny Mwaisabula, alisema kilichochangia Yanga kutoka kwenye njia kuu ni migomo ya wachezaji kutolipwa mishahara yao, akitolea mfano KMC ambavyo imekuwa na ushindani na wachezaji wanatimiziwa kila kitu.

“Unajua anayecheka mwisho ndiye anayecheka vizuri, Yanga ilicheka mwanzo wa ligi, Simba wanafunga ligi na kicheko kwa maana wana pesa, wanakuja kwa kasi na wamepata mbinu zaidi kwenye michuano ya kimataifa.

“Lakini sio hilo tu, inatakiwa kuchaguliwa kamati ya usajili ya kumsaidia kocha Mwinyi Zahera kupata wachezaji ambao watakuwa na jicho la kuona vipaji, sio mtu mwenye pesa ndiye awe kwenye kamati ya usajili hiyo sio sawa, wenye pesa kazi yao iwe kutoa pesa, kikosi kinatakiwa kuwa na mabadiliko makubwa kwa ajili ya msimu ujao”alisema.

Kwa upande wa staa wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa alisema,

“Kiufundi, Yanga ikiwa vizuri na Simba ikiwa vizuri ushindani unakuwa mzuri, wenzetu hawakuwa na kikosi kipana, vyema wakalitambua hilo ili waweze kujipanga upya kwa ajili ya baadaye.”