USAJILI ARSENAL: KUMBE TATIZO KROENKE

LONDON,ENGLAND. NDO hivyo buana. Bilionea mmiliki wa klabu ya Arsenal, Stan Kroenke hajatia mkwanja wowote kwenye kikosi cha Arsenal ili kufanya usajili wa mastaa wapya kwa miaka mitano iliyopita.

Miamba hiyo ya Emirates inayonolewa na Mhispaniola, Mikel Arteta inajaribu kujitutumua kufanya usajili kwa sasa, lakini wanafanya hivyo kwa kujibanabana na si kwa mkwanja kutoka kwa bosi wao mmiliki.

Kushindwa kufanya usajili ni kitu kilichowakera sana mashabiki wa Arsenal na kumwandama aliyekuwa kocha wao Arsene Wenger wakimwita ni bahili, lakini kumbe halikuwa tatizo lake. Hakuwa akipewa pesa ya kufanya usajili.

Ripoti ya Swiss Ramble imethibitisha mmiliki wa Arsenal, bilionea Stan Kroenke hajawekeza pesa yoyote ya kujenga kikosi kwa takribani miaka mitano iliyopita.

Uchunguzi uliofanywa kuzihusu klabu zote 20 za Ligi Kuu England, ulianzia msimu wa 2014-15 – Chelsea ndio timu ambayo mmiliki wake alitoa pesa nyingi kuwekeza kwenye kikosi kuliko timu nyingine zote kwenye ligi hiyo.

Bilionea mmiliki wa The Blues, Roman Abramovich alitumia mkwanja wa Pauni 440 milioni– Kroenke amewapa Arsenal Pauni 0 The Gunner ili kusajili.

Ripoti hiyo ilisomeka hivi: “Arsenal hawajapokea pesa yoyote kutoka kwa mmiliki wao kwa miaka mitano iliyopita, ama kutoka kwa Kroenke au benki.

“Badala yake, timu ililazimika kutoa Pauni 101 milioni (deni la mkopo Pauni 40 milioni na riba Pauni 61 milioni). Pia walilipia kampuni ya KSE [Kroenke’s company] Pauni 6 milioni ambayo ni ada ya ushauri.”

Kinachovutia, klabu 13 zilipokea pesa kutoka kwa wamiliki wao, huku saba kati yao zikipewa mkwanja unaoanzia Pauni 100 milioni na zaidi.

Hata Brighton, Fulham na Aston Villa zote zilipewa pesa ndefu kutoka kwa wamiliki wao – zaidi ya Pauni 150 milioni za kufanya usajili. Jambo hilo liliwafanya Arsenal kulazimika kuuza mastaa wake wenye majina makubwa kuliko kufanya usajili wa wakali wapya.

Mwaka jana, idara ya usajili ya kikosi cha Arsenal ilifanya maajabu kwa kunasa mastaa Nicolas Pepe na Kieran Tierney kwa pesa ndefu, huku mwaka huu kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi wakihangaika kusaka saini ya Thomas Partey kutoka Atletico Madrid.

Lakini, dili hilo halijakamilika hadi sasa kutokana na kutakiwa kulipa Pauni 45 milioni, huku tayari ikiwa imeshamsajili beki wa kati, Gabriel Magalhaes kutoka Lille kwa ada ya Pauni 22 milioni. Kitu kizuri ni imeweka kibindoni Pauni 20 milioni baada ya kumuuza kipa Emiliano Martinez kwenda Aston Villa.

Hata hivyo, bado watahitaji kuuza wachezaji wengine zaidi ili kupata pesa inayotosha kukamilisha usajili wa Partey. ImewasajiliDani Ceballos kwa mkopo kutoka Real Madrid na Willian, aliyenaswa bure kutoka Chelsea. Straika wao, Pierre-Emerick Aubameyang amesaini mkataba wa miaka mitatu na kulipwa Pauni 350,000 kwa wiki.

Kufichuka kwa jambo hilo kumewafanya mashabiki wa Arsenal kuwa na hasira, huku mmoja akiamua kutumia ukurasa wake wa Twitter kuwasilisha maoni yake, alipoandika: “Tumekuwa biashara ya ajabu sana kwa Stan Kroenke.” Mwingine kwa hasira aliandika: “Kroenke ni wa ovyo.” Na shabiki wa tatu aliandika: “Hebu Arsenal muondoeni huyu Kroenke, mambo gani haya?”