UKWELI NDIVYO ULIVYO: Kaze apewe muda, sio presha Yanga

JANGWANI kwa sasa roho kwatu. Kuanzia mabosi mpaka wanachama na mashabiki wao nyoyo zimetulia. Wamekipata walichokuwa wakikitafuta.

Kocha Cedric Kaze aliyekuwa akihitajika Yanga hata kabla ya ujio wa Zlatko Krmpotic ameshatua. Ameshajifunga mkataba wa miaka miwili. Kilichobaki sasa kwa mashabiki ni kutaka kuona ile kampa..kampa tena ikirejea Yanga.

Kocha huyo Mrundi anasifika kwa soka la kitabuni. Soka la pasi nyingi kuanzia nyuma na kushambulia mwanzo mwisho. Atletico Olympic aliyokuwa akiifundisha inakumbukwa ilivyoitoa nishai Yanga kwenye Kagame mwaka 2002. Kaze alikuwa benchini na Kavumbagu aliyafanya yake Yanga ikifa 2-0 na mwishowe akasajiliwa Jangwani.

Kocha huyo mwenye leseni daraja A aliyesomea Ujerumani na aliyewahi kuzinoa timu za taifa za Vijana za Burundi kuanzia U17, U20 na U23 sambamba na klabu mbalimbali za Burundi na Rwanda amebeba matumaini makubwa wanayanga.

Kaze aliyewahi kufanya kazi katika Kituo cha soka cha Barcelona (FC Barcelona Academy) na FC Edmonton ya Canada, hata yeye anajua kazi aliyonayo Jangwani. Anajua Yanga na Wanayanga wanasubiri miujiza kutoka kwake. Kwa misimu mitatu Yanga imekuwa nyonge mbele ya Simba.

Hakuna kitu kibaya na aibu kubwa kama unyonge mbele ya mtani. Simba ilitaabika kwa misimu karibu sita mbele ya Yanga. Waliburuzwa na Yanga kwa jeuri ya fedha za Yusuf Manji. Ubingwa wa Ligi walikuwa wakiusikia kwa jirani tu kwa miaka mitano. Yanga kwa sasa nao wana misimu mitatu hawajui utamu wa kunyanyua kwapa ili kuinua kombe lolote. Yaani hata kombe la mchangani hawajalibeba tangu Mohammed ‘Mo’ Dewji alipowapa jeuri Simba na tangu Manji alipoamua kujiweka kando Jangwani.

Yanga wameichoka hali hiyo. Bahati nzuri, Kampuni ya GSM imewarejesha jeuri kwa sasa Yanga kwa kusajili kikosi bora na kuwaletea makocha wazuri. Yanga haina njaa ya msosi kwa sasa. Ina njaa ya mafanikio. Alikuja Luc Eymael, hakuwa na tatizo ila ubaguzi wake ukamponza atatimuliwa akiipa timu nafasi ya pili Ligi Kuu iliyopita. GSM ikataka imleta Kaze, lakini ishu za kifamilia zikatibua. Wakambeba Zlatko. Mserbia huyo hakudumu kikosini, kwani kwa siku zisizozidi 37 ilitosha kuonyeshwa mlango wa kutokea. Hakufanya baya lolote. Timu ilicheza mechi nane, tatu za kirafiki na tano za Ligi Kuu na zote ilipata matokeo mazuri. Tatu za kirafiki zote ilishinda ikiwamo ile ya kimataifa dhidi ya Aigle Noir ya Burundi. Katika Ligi ndani ya mechi tano ilishinda nne na kutoka sare moja na kuiacha timu ikiwa nafasi ya tatu. Ikilingana na Simba japo tofauti ya mabao iliwatenganisha nyuma ya Azam FC. Yanga imefunga saba na kufungwa moja tu. Simba imefunga 14 na kufungwa mawili. Hata hivyo soka la kujihami na lisilo na mvuto lilikuwa tiketi ya kutimuliwa kwake siku ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Coastal Union. Jeuri ya fedha za GSM ndizo zilizoamua. Fasta Kaze kutumiwa tiketi na kuja.

Mabosi wa Yanga wanaamini ana miujiza itayowarejeshea heshima mbele ya wanachama na mashabiki. Wanachama na mashabiki nao wameweka tumaini hai kwa kocha huyo. Wanajua wamesaliwa na saa chache tu kuzima zile tambo na kelele za watani wao. Msimbazi wanawakerana kelele la Soka biriani...Soka kachori...Soka pishori linalopigwa kupitia nyota wake. Soka hilo lilikuwa likiwatesa. Ni kweli Yanga ina kina Carlinhos, Tuisila Kisinda, Mukoko Tonombe, Yocouba Songne na wengineo wakali, ila wote walionekana si mali kitu kwa kutulizwa na visigino vya Clatous Chama, Luis Miquissone na mabao ya Chriss Mugalu na Meddie Kagere.

Sasa wanaamini chini ya Kaze, Yanga itakuwa kama ile ya Hans Pluijm. Yanga ya kampa kampa tena yenye pasi, vyenga na mabao mengi uwanjani. Hii sio kazi rahisi ama inayoweza kutokea mara moja tu kama kutia chumvi kwenye mboga na kukoroga kupata ladha. Soka ni sayansi yenye ufundi inayoenda sambamba na muda.

Hapo ndipo hofu yangu inakuja. Hofu ni matumaini hayo makubwa kwa wanayanga yanapoweza kugeuka msalaba mzito kwa Kocha Kaze. Wanayanga wanatakiwa kuwa na subira na uvumilivu kwa Kaze. Hata kama ni kocha mzuri, lakini kiu waliyonayo inaweza kuwa presha kubwa kwa Mrundi huyo na mwishowe kushindwa kufikia malengo. Uzuri hata Mwenyekiti wao, Dk Mshindo Msolla amelifahamu hilo mapema, ndio maana kwenye mkutano wake aliwataka wanachama na mashabiki kutompa presha kocha. Dk Msolla ni kocha msomi. Amecheza na amefundisha soka. Anajua ugumu wa kuhimili presha za mashabiki wenye matumaini makubwa kwa kocha hasa kwa klabu kubwa kama ya Yanga. Ukweli ndivyo ulivyo, kama

wanayanga hawatakuwa na subira na kumpa muda, Kaze anaweza asidumu na kuimudu Yanga.

Kama umepitiwa ni kwa muda wa miaka miwili tu, Yanga imeongozwa na makocha wanne, Kaze akiwa ni wa tano. Hii ni rekodi kwao. Aprili 2018 iliachana na George Lwandamina. Baadaye Mei mwaka huo akaja Mwinyi Zahera, lakini Novemba mwaka jana ikamtimua na kumpa kazi Luc Eymael ambaye alianza kazi Januari na kutimuliwa Julai ikiwa ni miezi sita tu. Ndipo akaja Zlatko na siku zake 35 ndani ya timu na siku 37 tangu atue Tanzania. Hapo sijamtaja Charles Boniface Mkwasa aliyeishikilia timu tangu Zahera alipotimuliwa.

Ndio maana natadharisha tu, Yanga lazima impe muda Kaze ili afanye kazi zake, pia asiingiliwe wala kupewa presha kama kweli wanayanga wanataka kurejesha heshima yao mbele ya Simba na wadau wa soka kwa ujumla.

Vinginevyo, kama wataendeshwa na mihemko na ujuaji mwingi, watamfelisha Kaze mapema. Wajifunze kwa Simba walimvumilia Sven Vandenbroeck waliyekuwa na hofu naye na sasa wanakula raha. Kazi kwenu!