UCHAMBUZI: Natamani kuanza kumuona Senzo vitani Yanga

KUNA mtu mmoja katika uongozi wa Yanga anafanya kazi akiwa nyuma ya pazia- anaongoza vita mbalimbali akiwa katika kivuli cha wengine ambao wamejitanguliza mbele na baadhi wakiwa na silaha nyepesi.

Wakati timu zikiwa kwenye usajili wa wachezaji, Yanga ndio timu iliyosajili bosi wa kigeni katika uongozi wao wakimleta Senzo Mbata Mazingisa katika uongozi, lakini akageuka kufanyia kazi nyuma ya pazia katika uongozi wao.

Senzo mpaka sasa anafanya kazi kama mshauri wa uongozi katika klabu hiyo na nafasi hiyo inaelezwa katiba ya klabu hiyo inatakiwa kwanza kumtambua kisha ndio aingie katika uongozi ama sekretarieti ya Yanga.

Kwa maana nyingine ni kwamba katiba yao inazuia raia wa kigeni kupewa majukumu ya nafasi ya mtendaji mkuu wala haitambui kama nafasi hiyo ni zaidi ya katibu mkuu. Sio mbaya kwa klabu kwanza kutangulia kusajili kabla ya kujua watamtumiaje mchezaji husika kikanuni kutokana na wenye jukumu la kubadilisha katiba ni wao wenyewe ambao wamemchukua na kumleta katika nyumba yao, na kuamua kuishi naye.

Hakuna ambaye anaweza kumkataa Senzo ndani ya klabu kutokana na uzoefu wake katika masuala ya uongozi wa michezo, akiwa amefanya kazi sehemu mbalimbali na anatahitajika kuliko klabu anavyozihitaji yeye.

Klabu zetu nyingi hata Yanga wenyewe wako nyuma katika ubora wa muundo wa kiuongozi ambao unaondoa kasoro nyingi za ubora. Klabu zinahitaji watu kama Senzo kuweza kubadilika na kujiendesha kisasa zaidi.

Hakuna ambaye hakuona alichokifanya pale Simba katika muda mfupi na jinsi gani klabu hiyo ingeweza kupiga hatua haina ulazima sana kusubiri wahusika waseme hili hali ya kuwa linaonekana ingawa kiubinadamu hatukatai anaweza kuwa na upungufu wake. Maisha yako hivyo.

Yanga sasa bado sekretarieti yao inaongozwa na kaimu katibu mkuu, Simon Patrick, akiendelea kushika nafasi ya Dk David Ruhago ambaye aliondolewa mapema tu baada ya kuonekana alishindwa kabisa kumudu nafasi hiyo.

Angalau sasa kidogo mambo yalionekana kutulia kutokana na ufanisi wa Patrick ambaye kitaaluma ni mwanasheria na akiwa awali alihudumu idara ya sheria ya klabu hiyo. Inawezekana wapo ambao wanaona kama kutulia huku kuna sababu ya kuendelea kusubiri zaidi kumuona mtu kama Senzo akifanya kazi nyuma ya pazia. Akili yangu naona kama Yanga wanachelewa kumfaidi Senzo inavyotakiwa.

Natamani kuona sasa wanaingia katika kubadili katiba yao haraka ili imruhusu Senzo kuja mbele ya uongozi na kuwa mtendaji huru ili aanze kuibadilisha klabu hiyo kwa kasi zaidi kuliko uhalisia unaondelea sasa.

Patrick hawezi kuwa huru sana katika nafasi hiyo kutokana na kuwa na kamba ya ukaimu, lakini pia ikumbukwe awali aliingia hapo kama mkurugenzi wa sheria. Ni wakati sasa kumrudisha katika idara yake ili mtu muafaka ashike nafasi yake na kuona mambo yanakimbia kwa haraka zaidi.

Utendaji wa Patrick umeonekana amefaulu wapi na ameanguka wapi, lakini endapo atarudi eneo lake kisha kushirikiana na Senzo kuna uwezekano mkubwa ukomavu wa sekretarieti ya klabu hiyo kongwe ukaonekana kwa haraka.

Yanga naona wanajichelewesha kufika wanakotaka kwenda kwa kuendelea kupiga danadana hatua za mkutano mkuu wao, kwani muda sio rafiki kwao hasa wakati huu wakiwa katika mchakato wa mabadiliko.

Wanatakiwa kutambua kwamba wako nyuma sana katika maendeleo na sasa kama ambavyo walitafuta watu wa kuwafundisha muundo wa uongozi bora, pia ni wakati sasa wakaanza kuwaingiza ndani watu kama kina Senzo ili wakaondoe shida za uongozi wa klabu hiyo ili hatua ya maendeleo ionekane inafanyika kwa haraka.

Binafsi naona kama Yanga wameamua kujitesa katika kuishi na njaa kwa muda mrefu huku wakijua wanacho chakula ndani ambacho ni Senzo. Kazi ni kwao kupanga ni kuchagua muda, hauwasubiri wao.