UCHAMBUZI: Makipa mmemsikia Etienne Ndayiragije?

KUNA mambo mengi ambayo Kocha Mkuu wa timu ya taifa star,  Etienne Ndayiragije aliyazungumza katika mahojiano yake na kituo cha habari cha Wasafi, mwanzoni mwa wiki hii.

Moja ya mambo aliyoyasema Ndayiragije ni udhaifu wa idadi kubwa ya makipa wetu katika kuucheza mpira kwa miguu ambapo ni wachache tu hapa nchini wanaoweza kufanya hivyo kwa maana ya kupokea, kupiga pasi na kucheza akimtolea mfano Juma Kaseja.

Ndayiragije alizungumza hayo muda mfupi baada ya kikosi cha Stars kuitwa kwa ajili ya mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya timu ya Taifa ya Burundi ambao utachezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam Jumapili.

Katika kikosi hicho cha Stars, makipa walioitwa ni pamoja na Aishi Manula, Metacha Mnata na David Kissu ambao pia walikuwemo katika kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars kilichoshiriki mashindano ya Kombe la Chalenji nchini Uganda, Desemba mwaka jana na kumaliza katika nafasi ya nne.

Kauli ya Ndayiragije imekuja katika kipindi ambacho kumekuwa na ushindani mkubwa wa makipa katika Ligi Kuu ambapo kuna idadi kubwa ya wanaocheza nafasi hiyo waliocheza mechi nyingi bila kuruhusu nyavu zao kutikiswa, kigezo ambacho kimekuwa kikitumika katika uteuzi wa mshindi wa tuzo ya kipa bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Metacha, Kissu, Daniel Mgore (Biashara United) na Aaron Kalambo wa Dodoma Jiji FC kila mmoja amecheza jumla ya mechi nne bila kuruhusu nyavu zake kutikiswa wakifuatiwa na Manula na Geophrey Msafiri (Polisi Tanzania) ambao kila mmoja hajaruhusu nyavu zake kutikiswa katika jumla ya michezo mitatu na wengineo wakiwa wamecheza mechi mbili huku wakiwepo pia waliofanya hivyo mara moja.

Hata hivyo kucheza idadi kubwa ya mechi bila kuruhusu bao, ni utaratibu tu ambao mamlaka za soka katika maeneo mengi duniani zimeamua kuuweka ili tu kuondoa migogoro na kupunguza lawama katika utoaji wa tuzo kwa mchezaji wa nafasi hiyo kwenye mashindano fulani, lakini kiuhalisia hakipaswi kuwa kigezo cha mwisho na hiki ndicho bila shaka Ndayiragije amekizingatia hadi akafikia kutoa kauli yake juu ya makipa.

Zipo sifa za msingi ambazo kipa bora na mahiri anapaswa kuwa nazo ambazo baadhi ni kama vile kuokoa mashambulizi, kuhamisha mipira, kupanga timu, kuuelekeza mpira, kuuchezea, kusoma mikimbio ya wapinzani, makadirio na pia kutawala eneo lake.

Kwa makocha ambao wamekuwa wakifundisha soka la kisasa, wengi wanahitaji kuwa na kipa au makipa ambao wana muunganiko wa sifa hizo hasa ya kuchezea mpira na kupasia wakiwa na lengo la kutaka kuvifanya vikosi vyao vianze kucheza au kujenga mashambulizi kuanzia nyuma lakini kuuweka mpira katika mazingira salama pindi unapokuwa kwao.

Hata hivyo kwa bahati mbaya hapa nchini, idadi kubwa ya makipa ambao tunawaona bora, ni wale ambao wana sifa chache tu hasa ile ya kuokoa mashambulizi hususani yale ya ana kwa ana na mipira ya krosi na sio sifa nyingine za muhimu na za msingi ambazo kipa wa kisasa anapaswa kuwa nazo.

Na kinachopelekea haya yote ni uhaba wa walimu bora na wabobezi wa makipa hapa nchini na badala yake wanatumika ambao wanafanya hivyo kwa vile tu waliwahi kuwa walinda mlango siku za nyuma na sio kwamba wamekidhi vigezo kwa kuwa na lesen za madaraja ya juu ya ukocha wa makipa.

Matokeo yake tunakuwa na kundi kubwa la makipa ambao wanakosa sifa nyingi za kiufundi kwa mahitaji ya soka la kisasa na kupelekea ugumu kwao kupiga hatua angalau hata kucheza soka la kulipwa nje ya nchi ama kupata uteuzi katika vikosi vya timu za Taifa.

Etienne anatukumbusha kuwa kipa anapokuwa langoni, anahitajika atimize majukumu mengi zaidi ya kudaka au kupangua mipira ambayo na badala yake awe sehemu ya mchezo kwa kushiriki kuichezesha timu na kuanzisha mashambulizi kupitia miguu yake jambo ambalo idadi kubwa ya makocha duniani wanapanda kuona likifanywa na makipa.

Lakini hilo halitoweza kufanikiwa kama makipa wenyewe pamoja na makocha wanaowanoa hawatokuwa tayari kujifunza na kubadilika na kuamua kuendelea na mazoea yao ambayo yamekuwa yakiwarudisha nyuma.

Kubadili utamaduni uliozoeleka sio jambo rahisi lakini kama kutakuwepo na nia ya dhati kutoka kwao, bila shaka hiki ambacho Ndayiragije anakihitaji kutoka kwa makipa kitabakia kuwa historia na tutakuwa na idadi kubwa ya makipa wa daraja la juu.