ZEKICK: Kwa nini Simba isifungwe?

JUZI watetezi wa Ligi Kuu ya Tanzania, Simba SC, ilifungwa na Tanzania Prisons katika mechi iliyochezwa katika Uwanja wa Samora mjini Sumbawanga na dakika chache baadaye, nikaanza kusoma meseji za mashabiki waliokerwa.

Mazungumzo yalihusu kuhusu wachezaji ambao hawakucheza katika mechi ile, uamuzi mbaya wa mwamuzi wa pambano lile na namna Simba ilivyokuwa haina kikosi kipana kama inavyosemwa kila siku.

Kuna mjadala mmoja haukuzungumzwa kabisa. Kwamba ni namna gani Prisons walionekana kuwa na mpango maalumu wa namna ya kucheza mechi ile na kwamba matokeo yale yalimaanisha mpango wa kiufundi wa maafande hao ulifanya kazi vizuri.

Kuna msemo mmoja maarufu wa karibuni wa lugha ya Kiswahili ambao mimi hupenda kuutumia; Kwamba pale unamposifia mtu kwa kuwa na mbio ni muhimu pia kuwapongeza wale wanaomkimbiza.

Ifike wakati mashabiki wa soka waamini kwamba Simba na Yanga ni timu za Ligi Kuu ambazo zinashindana na timu nyingine za hadhi hiyohiyo. Wakati mwingine, mashabiki wanatakiwa kunyoosha miguu juu na kusema wapinzani walishinda na walistahili ushindi. Si kwa sababu timu yao ni mbovu au wachezaji waliocheza ni wabovu, lakini kwa sababu huo ndio mchezo wa soka ulivyo. Ni mchezo wa kitimu na lolote linaweza kutokea.

Real Madrid ya Hispania wiki hii imefungwa na Shakhtar Donetski ya Ukraine ambayo haikuwa na wachezaji wake 10 wa kikosi cha kwanza. Ni sawa na kusema Real Madrid iliyokuwa ikicheza katika uwanja wake wa nyumbani imefungwa na kikosi cha pili cha Shakhtar.

Mashabiki wa Madrid wana haki ya kuumia kwa sababu wamefungwa na kikosi cha pili cha timu ambayo kwa kawaida walitarajiwa kuifunga hata kama ingekuja na kikosi chake cha kwanza.

Simba imecheza na kikosi cha kwanza cha Prisons kilichopata muda mrefu wa kufanya mazoezi wakati wengi wa wachezaji wa Msimbazi walikuwa katika mashindano ya kimataifa ambako aina ya mazoezi ni tofauti, mifumo tofauti na matarajio ni tofauti pia. Na kwa mashabiki na wafuatiliaji wa mchezo wa soka, watakuwa wanafahamu kwamba mara zote Simba imekuwa ikipata taabu katika mechi dhidi ya Prisons ya Mbeya, Kagera Sugar ya Kagera na wakati fulani Toto African ya Mwanza.

Ninafahamu kwamba labda matokeo yangekuwa tofauti endapo kikosi kamili cha Simba kingecheza mechi ya Sumbawanga lakini nimeshuhudia mechi ambazo Lunyasi walikuwa na kikosi kamili na bado wakafungwa.

Nakumbuka sana wakati ule wakati kikosi cha Simba kikiwa na nyota kama Juma Kaseja, Patrick Mafisango, Haruna Moshi, Felix Sunzu na Emmanuel Okwi lakini kikashindwa kuifunga Kagera Sugar ya kina Salum Kanoni.

Kwa hiyo, inawezekana kabisa kwamba kina Medie Kagere, John Bocco, Clatous Chama na Luis Miquissone wangekuwepo uwanjani na bado Simba ingeweza kutoka patupu kwa sababu ndivyo mpira ulivyo.

Michezo na Uchaguzi

Kwa mara ya kwanza katika safu hii nitazungumzia kidogo kuhusu siasa. Sote tunafahamu kwamba Jumatano ijayo Watanzania watakwenda kuchagua viongozi watakaoongoza taifa hili katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Uzoefu wangu unaonyesha kwamba wengi wa mashabiki wa michezo; na wasomaji wa gazeti hili na mengine ya michezo ndani na nje ya nchi, mara nyingi hawapendi kujihusisha na masuala ya siasa.

Ujumbe wangu kwa wanamichezo wenzangu ni kwamba wanatakiwa kupanga ratiba yao ya Jumatano ijayo na katika mambo yote watakayopanga, wanatakiwa kupanga kupiga kura.

Haisaidii kwa wanamichezo kupiga kelele kwamba sekta hii inaachwa nyuma kwenye mipango mikubwa ya maendeleo, lakini wakati huohuo hawataki kupiga kura kwa sababu yoyote ile.

Popote pale ulipo, angalia nani na nani wanawania Urais, Ubunge na Udiwani na fanya uamuzi wa kuchagua mtu ambaye unadhani ataweza kusogeza ajenda za michezo katika duru zenye ushawishi.

Wapo wagombea ambao wanajulikana kuwa ni wanamichezo, wapo wagombea ambao hawajulikani kuwa ni wanamichezo, lakini mtu ukiwatazama unaona kwamba wanaweza kufuatwa na kushawishiwa na wakaweza kufanya mambo makubwa.

Wakati Rais Benjamin Mkapa anaingia madarakani, si watu wengi walikuwa wanamjua achilia mbali kufahamu ni klabu gani anaishabikia miongoni mwa timu pendwa za hapa kwetu.

Lakini, ni Mkapa huyo huyo ambaye wakati wa utawala wake alijenga Uwanja wa Benjamin Mkapa ambao kwa sasa ni mmoja wa viwanja mashuhuri vya Afrika.

Kazi kubwa ya mashabiki wanaokwenda kupiga kura ni kuwasikiliza wagombea au kujitahidi kuwafahamu wagombea hao na mwisho wa siku mtu aweze kufanya uamuzi wenye manufaa kwa maendeleo ya michezo hapa nchini.

Msikae pembeni, nendeni mkapige kura ifikapo Oktoba 28 mwaka huu.