UCHAMBUZI: Dodoma, Tanga wanapenda FDL kuliko Ligi Kuu?

NILIKUWA miongoni mwa umati wa mashabiki waliojazana katika Uwanja wa Jamhuri Dodoma, Jumamosi, Julai 11.

Ulikuwa ni miongoni mwa mechi za mwisho za Kundi A la Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu uliopita iliyozikutanisha wenyeji Dodoma Jiji FC ya jijini humo na Iringa United ya Iringa.

Dodoma Jiji ilikuwa ikihitaji ushindi wa utofauti mzuri wa mabao dhidi ya Iringa United ili kujihakikishia kupanda Ligi Kuu msimu wa 2020/2021, hivyo kuvunja mwiko wa zaidi ya miaka 10 kwa mkoa wa Dodoma kutokuwa na timu katika Ligi Kuu tangu Polisi Dodoma iliposhuka 2011/2012.

Taswira ya Uwanja wa Jamhuri ilionyesha wazi kiu ya wakazi na mashabiki wa soka mkoani Dodoma kuwa na timu inayoshiriki Ligi Kuu na bahati nzuri timu yao haikuwaangusha baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 ambao uliwap tiketi ya kushiriki Ligi Kuu.

Uwanja ulitapika idadi kubwa ya watu waliokuwa na hamu ya kushuhudia mchezo huo ambapo hadi kufika saa 8.30 alasiri, mageti yote yalikuwa yameshafungwa ili kuzuia umati wa mashabiki waliokuwa wakishinikiza kuingia uwanjani baada ya tiketi zote za mchezo huo kuwa zimeshauzwa.

Kulikuwa na umati mkubwa nje ambao pengine ulikuwa unafanana au kuzidi ule wa mashabiki ambao walifanikiwa kuingia uwanjani kutazama mechi hiyo ya kihistoria jambo lililodhihirisha wazi kuwa kweli watu wa Dodoma walikuwa hawajaiona Ligi Kuu kwa muda mrefu.

Neema ilizidi kuwaangukia wapenzi na mashabiki wa soka Dodoma mara baada ya ligi kuanza pale uongozi wa JKT Tanzania ulipoamua kuhamisha makazi yake mkoani humo jambo lililofanya jiji la Dodoma kuwa na timu mbili zinazoshiriki katika Ligi Kuu.

Wengi walitegemea kuona hamasa ile iliyoonyeshwa na mashabiki na wakazi wa mkoani Dodoma katika mchezo wao wa nyumbani dhidi ya Iringa United ingeendelea kuonekana katika Ligi Kuu katika mechi za Dodoma Jiji FC na JKT Tanzania.

Fursa iliyotolewa na Bodi ya Ligi Kuu, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na viongozi wa Dodoma Jiji na wale wa JKT Tanzania ya kufanya viingilio vya chini kwa mechi nyingi za timu hizo kwenye Uwanja wa Jamhuri kuwa Shilingi 3,000 ilitegemewa wamba ingetumiwa na mashabiki wa jiji hilo kujazana kwa wingi katika mechi za Ligi kama ilivyokuwa katika mechi yao dhidi ya Iringa United.

Hata hivyo kwa bahati mbaya kile kilichotegemewa bado hakijatokea hadi sasa.

Pamoja na Dodoma Jiji kuanza vyema Ligi Kuu ikiibuka na ushindi katika mechi zake zote ilizocheza nyumbani, sehemu kubwa ya majukwaa ya uwanja wa Jamhuri huwa tupu katika mechi nyingi ambazo timu hiyo na JKT Tanzania zinacheza uwanjani hapo.

Licha ya juhudi kubwa ya uongozi wa Dodoma Jiji na makundi ya hamasa ya mashabiki kama vile tawi la makao makuu la timu hiyo kushawishi wapenzi wa soka na wakazi wa jiji la Dodoma kujazana Jamhuri ili kuziunga mkono timu zao, muitikio umeendelea kuwa wa chini.

Hali ni tofauti kwa mkoa wa Rukwa ambao mashabiki na wakazi wake wameonekana kuipokea kwa mikono miwili timu ya Prisons ambayo imechagua kuutumia Uwanja wa Nelson Mandela uliopo mjini Sumbawanga kwa mechi zao za nyumbani.

Mashabiki hao wa soka mkoani Rukwa wamekuwa wakijitokeza kwa wingi katika mechi za nyumbani za Tanzania Prisons na kana kwamba haitoshi huishangilia kwa nguvu zote kuanzia dakika ya kwanza hadi pale filimbi ya kumaliza mechi inapopulizwa.

Rukwa wanaonyesha kwa vitendo kuwa walikuwa na kiu ya kuona mechi za Ligi Kuu katika mkoa wao na uamuzi wa Prisons umekuwa kama neema kubwa kwao na fursa ambayo hawataki kuichezea.

Wanadodoma wanapaswa kuiga mfano wa wenzao wa Rukwa ambao wanaonesha wazi kuwa hawataki kupoteza fursa iliyokuja mkononi mwao ya kuwa na timu inayoshiriki Ligi Kuu.

Ligi Kuu ina thamani na heshima kubwa kuliko Ligi Daraja la Kwanza. Inashangaza kuona wale waliojitoa na kujazana kwa wingi katika mechi za Ligi Daraja la Kwanza, leo hawafanyi hivyo katika Ligi Kuu.

Tabia hii inakuwa ni kama muendelezo wa kile ambacho hufanywa na mashabiki wa soka mkoani Tanga pindi wanapokuwa katika harakati za kupandisha timu.

Timu inapokuwa Ligi Daraja la Kwanza wanajazana katika Uwanja wa Mkwakwani lakini ikishatimiza lengo wanayeyuka.

Tuseme wanaipenda sana Ligi Daraja la Kwanza au hawajui thamani ya kuwa na timu Ligi Kuu?