NO AGENDA: Tumsaidie Diamond kuzifikiria vizuri kodi zake za nyumba

Sunday May 3 2020

 

By Luqman Maloto

MAPEMA Machi, mwaka huu, mkurungenzi mkuu wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Profesa Mohamed Janabi alitoa makisio yafuatayo kuhusu kuingia kwa ugonjwa covid-19 nchini. Mosi, asilimia 80 ya wagonjwa wataumwa na kupona bila kuhitaji matibabu au watameza dawa nyumbani na kupona.

Pili, Profesa Janabi alisema asilimia 15 watalazimika kwenda hospitali, watatibiwa na kupona bila kuhitaji uangalizi wa hali ya juu. Tatu, alitaja ni asilimia 5, ambao wataugua sana, hivyo kulazimik kufungiwa mashine za kupumulia, yaani ventilator machines ili kunusuru maisha yao.

Profesa Janabi alisema ventilators zipo Hospitali ya Taifa Muhimbili, Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI) na JKCI. Hata hivyo, mashine hizo ni chache mno. Hazitatosha asilimia tano ya watakaoumwa covid-19 nchini na kuhitaji msaada wa kupumua.

Na uchache wa ventilator machines ni tatizo la dunia nzima. Italia ilibidi baadhi ya wagonjwa waliotumia mashine siku mbili wandolewe ili kupisha wapya. Matokeo yake watu wengi walipoteza maisha kwa kukosa msaada wa mashine za kupumulia.

Ilikuwa hivi; mashine zote za msaada wa kupumulia zilikuwa na watu waliozihitaji. Wakati huohuo wagonjwa wengine wenye kuhitaji msaada wa ventilator waliongezeka. Ikabidi waliopo kwenye machine waondolewe kwa mtazamo kuwa angalau walikuwa wameshaambulia. Wawapishe ambao hawajapata kabisa.

Profesa Janabi alitoa takwimu kuwa katika kila Waitaliano 100,000, ni watu 20 tu wakiugua ndio wanaweza kupata ventilators. Alisema na Marekani katika kila watu 100,000 ni watu 34 tu wanaoweza kupata ventilators. Ni kwamba katika watu 100,000, endapo kutakuwa na watu 35 wenye kuhitaji ventilators, mmoja atakosa. Na atakufa.

Advertisement

Ni kwa takwimu hizo imekuwa ni rahisi ‘kubet’ kuwa maelfu ya watu wanaokufa kwa covid-19 Marekani, sababu ni upungufu wa mashine za kupumulia. Wingi wa wagonjwa ni mkubwa. Hakuna ventilator machine inayobaki tupu. Wagonjwa wapya wanawekwa wapi?

Ni kwa sababu hiyo, Marekani, wadau mbalimbali wamekuwa wakinyooshea mkono kuelekea sekta ya afya, maana mapambano dhidi ya covid-19 yanawategemea madaktari, wauguzi na watumishi wengine wa afya. Hao ndio makamanda walio mstari wa mbele.

Aprili 12, mwaka huu, saa 4 usiku, saa za Afrika Mashariki, saa 9 alasiri saa za Ukanda wa Pacific (PST) au saa 6 mchana kwa Ukanda wa Mashariki (EST), Rapa P Diddy na familia yake walikuwa wanatoa shoo ya kudensi live kupitia Instagram. Shoo iliitwa “Dance A-thon”.

Awali, Diddy na wanaye walitoa matangazo ya shoo ili kila mmoja, panapo wakati akaribie. Lengo la shoo hiyo ni kuchangisha fedha kwa ajili ya kuwaongezea nguvu wafanyakazi wa sekta ya afya nchini Marekani.

Ni kampeni inaendelea Marekani kwa sasa. Taifa linashambuliwa kwa kasi kubwa na virusi vya Sars Corona 2, ambavyo vinasababisha ugonjwa wa covid-19. Jana saa 8:15 mchana (saa za Afrika Mashariki), Marekani ilifikisha rekodi ya waathirika 1,131,856.

Idadi hiyo ya wagonjwa wa covid-19 Marekani ni sawa na asilimia 29 ya waathirika wote waliorekodiwa ulimwenguni mpaka sasa. Dunia nzima, hadi jana mchana saa 8:15, wagonjwa wa covid-19 waliorekodiwa ni 3,417,609. Vifo duniani ni 239,900, Marekani ni 65,782.

Kutokana na hali hiyo, ni dhahiri kwa sasa wafanyakazi wa sekta ya afya wanafanya kazi kubwa sana. Ndio maana P Diddy aliona ana wajibu wa kuchangisha fedha kusaidia kuwapa motisha wafanyakazi wa sekta hiyo. Na si yeye tu, ni kampeni yenye nguvu kwa sasa Marekani.

Kipindi hiki watu wengi wanajifungia nyumbani, wanaishi kwa tahadhari kubwa kusudi wasipate maambukizi, kuna watu wanawapokea au kuwafuata wagonjwa, wanawahudumia ili kuokoa maisha yao.

Watumishi wa afya, madaktari na wauguzi, ndio ambao wapo mstari wa mbele kupambana ili kuhakikisha wagonjwa wanapona na hata kama wanakufa, basi maambukizi yasiendelee. Lazima kuwaonyesha kuwa jamii inawathamini kwa kazi kubwa wanayofanya. P Diddy akaenda ‘live’ Aprili 12.

Hiyo ndio hamasa kila mtu anapaswa kuwa nayo. Hata Tanzania, wafanyakazi wa sekta ya afya wanajituma sana kwa sasa. Inatakiwa waungwe mkono. Wanamuziki na watu maarufu mbalimbali, kila mmoja kwa nafasi yake anaweza kufanya jambo kuwapa nguvu wafanyakazi wa sekta ya afya ili wajione wanathaminiwa kwa kujitoa kwao.

Mastaa wakubwa walikwenda sawa na Diddy; LeBron James mpaka Kelly Rowland, Drake hadi Oprah Winfrey, Demi Lovato, Justin Beiber, DJ Khaled na asisahaulike Jennifer Lopez ‘J Lo’, ex-girlfriend wa Diddy.

Wakati Diddy na J Lo wakicheza, J Lo alimtania “nilikufundisha kucheza hivyo?” Nyuma ya J Lo alikuwepo mpenzi wake wa sasa, Alex Rodriguez. J Lo alisema kuwa Alex ni shabiki mkubwa wa Diddy na Mase. Jumla ya Dola 4 milioni (Sh10 bilioni) zilikusanywa.

KWA DIAMOND

Diddy anachangia sekta ya afya kwa sababu ndiko kuliko na changamoto kubwa. Ndio maana mastaa wakubwa duniani waliamua kuungana naye.

Diamond Platnumz, ametangaza msaada wake wa kulipa kodi za nyumba kwa familia 500 katika kipindi hiki cha mapambano dhidi ya covid-19.

Msaada ni msaada. Yeye ameona hilo ndilo eneo la kusaidia, kwani kuna watu wanakosa kabisa vipato kipindi hiki. Tujiulize, huo ni msaada mwafaka kwa wakati mwafaka?

Yupo mtu atauliza, kipindi cha mlipuko wa covid-19 na upungufu wa vifaa tiba unawezaje kumlipia mtu kodi ya nyumba badala ya kumnunulia barakoa na vitakasa mikono ili ajilinde na covid-19?

Unamlipiaje mtu kodi ya nyumba wakati akiugua hatapata mashine ya kumuwezesha kupumua? Kwa nini Diamond asingenunua ventilators hata mbili angalau zitaokoa maisha ya watu?

Bei ya ventilator moja ni Dola 25,000 (Sh58 milioni) mpaka Dola 50,000 (Sh116 milioni). Ventilators zitaokoa maisha ya watu, kodi za nyumba zitaokoa watu wasikose makazi. Tofauti haionekani?

Chukua maelezo ya Prof Janabi kuhusu uchache wa ventilators nchini. Unganisha harambee ya P Diddy. Jawabu unalo kuwa kipindi hiki misaada ipelekwe sekta ya afya. Kama ambavyo mfanyabiashara Rostam Aziz alivyowezesha kupatikana kwa mashine ya kupumia covid-19 Zanzibar.

Uganda, Serikali ilizuia wenye nyumba kutoza kodi za pango kipindi hiki. Hata bila tamko la serikali, suala la kodi za nyumba ni la mazungumzo zaidi kati ya wenye nyumba na wapangaji. Wanaweza kuzungumza na kuelewana kwa kuitazama hali halisi. Ventilators, barakoa na vitakasa mikono si vya maridhiano. Lazima viwepo ili kuokoa maisha ya watu.

Advertisement