Tuanze kuchukua tahadhari mapema kabla ya maafa

Muktasari:

  • Hata hivyo kwa bahati mbaya ama ni kwa makusudi mechi nyingi ziwe za Ligi Kuu na hata za madaraja ya chini zimekuwa zikichezwa bila kuwepo kwa gari la wagonjwa na hata wakati mwingine kusiwepo kabisa hata watu wa huduma ya kwanza.

SOKA ni mchezo wenye pilikapilika nyingi na unaruhusu wachezaji kugongana ama kugusana, tofauti na ilivyo kwa gofu, tenisi ama kriketi.

Ni mchezo unaotumia nguvu kubwa na wakati mwingine kusababisha majeruhi wanaohitaji huduma ya kwanza kwa haraka zaidi kulinganisha na michezo mwingine.

Ajali zinazotokea kwenye soka zinafanana kwa kiasi kikubwa na zile za Raga ama ngumi, ambapo kama hakuna huduma ya kwanza ya uhakika ni muhali kwa wahusika hata wakati mwingine kupoteza uhai.

Hivyo kabla ya pambano la soka inasisitizwa na ni moja ya sheria inayosimamia mchezo huo kuwa ni lazima kuwa na uhakika huduma ya kwanza na gari la kubebea wagonjwa kwa ajili ya dharura inayoweza kujitokeza uwanjani.

Hata hivyo kwa bahati mbaya ama ni kwa makusudi mechi nyingi ziwe za Ligi Kuu na hata za madaraja ya chini zimekuwa zikichezwa bila kuwepo kwa gari la wagonjwa na hata wakati mwingine kusiwepo kabisa hata watu wa huduma ya kwanza.

Jukumu la kuhudumiwa wachezaji wanaopatwa na majereha huachwa kwa madaktari wa timu ambao baadhi yao hawana sifa za utabibu, ndio maana unaweza kuwaona wanapoitwa na refa linapotokea tatizo, wao hubeba barafu tu bila kujali kitu gani kilichompata mchezaji husika.

Hatukusudii kumnyooshea mtu kidole ama kumlaumu, ila kama wadau wa michezo tulikuwa tunatahadharisha tu, kuwa hiki kinachofanyika sasa ni hatari kwa maisha ya wachezaji na hata watazamaji.

Tuliwahi kuona jinsi Nsa Job alivyoumizwa kwenye mechi Uwanja wa Azam Complex, enzi hizo akicheza Ligi Kuu, lakini majeruhi alikuja kubebwa baada ya muda kwa gari binafsi aina ya Noah kutokana na kukosekana kwa gari la wagonjwa la kumuwahisha mapema hospitalini.

Ishatokea pia kwenye mechi ya Ligi Daraja la Pili mchezaji wa Kitayosce FC misimu mitatu iliyopita kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha alipoumia na kuvunjika, lakini uwanjani hakukuwa na gari la wagonjwa wala huduma ya kwanza ya kueleweka.

Hivi karibuni tena ndani ya msimu huu, limetokea Mwanza kwenye Ligi Kuu baada ya beki wa Coastal Union, Adeyum Saleh kuanguka ghafla uwanjani na kukaribia kupoteza maisha kabla ya mchezao wa Mbao kumvuta ulimi, lakini hakukuwa na gari la kubebea wagonjwa.

Kitu cha kushuruku ni kwamba matukio yote hayo yanayotokea, hayajawahi kuleta maafa, lakini bado haliwezi kupuuzwa kwa kusubiri litokea janga ndipo hatua zianze kuchukuliwa.

Imefika wakati sasa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi (TPLB) ikishirikiana na wasimamizi wa kituo ama chama husika cha mkoa, kuhakikisha mchezo hauanzi hata iweje mpaka kuwepo na gari la wagonjwa na huduma ya kwanza inayoeleweka. Tunajua hili ni lazima, lakini kuna kauzembe fulani kanafanyika kwa wasimamizi kufanya mambo kwa mazoea na mwisho kuwaumbua watu pale inapojitokeza tatizo kubwa kama yaliyojitokeza nyuma na hata hilo la Adeyum.

Ni miaka michache tulishuhudia mchezaji kinda wa Mbao FC alipoteza maisha uwanjani kwenye mechi za Ligi ya Vijana, kuonyesha tunapaswa kuchukua tahadhari mapema kwa kuwa uhai wa mtu hakuna mwenye dhamana nao.

Tunafahamu wakati mwingine mambo yanafanywa kienyeji kwa ajili ya kukwepa gharama, lakini ukweli ni kwamba hakuna fidia katika uhai wa mtu na hakuna chenye gharama kubwa kama uhai ndio maana tunakumbusha tu, hili suala ni muhimu kuzingatiwa kwa usalama wa wote.

Kuwepo kwa gari la wagonjwa sio kwa ajili ya wachezaji tu, hata mashabiki wanaweza kupatwa na tatizo la kiafya na kusaidia kuwanusuru kupoteza uhai. TUmekuwa tukiona mashabiki wakianguka na kuzimia kwa sababu ya presha za mechi, hivyo umuhimu wa gari la wagonjwa na huduma ya kwanza sio jambo la kuchukuliwa kiwepesi.

Kwa vile wahenga walishasema kuwa, kinga ni bora kuliko tiba, basi tuanze kuchukua tahadhari mapema badala ya kusubiri maafa yatokee uwanjani ndipo sasa yaye yatolewe matamko ama marufuku ambazo hazitaweza kurejesha uhai wa watakaokumbwa na maafa uwanjani.