Tshabalala, Gadiel wamweka njia panda Mbelgiji Simba

Muktasari:

Akizungumza katika mazoezi, Kocha wa Simba Patrick Aussems alisema Tshabalala na Gadiel ni mabeki hodari, lakini atampanga atakayekuwa fiti kulingana na aina ya mchezo.

Dar es Salaam. Wakati Simba ikijiandaa kwa mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya UD Songo, vita ya namba imeonekana zaidi kwa mabeki wa kushoto Gadiel Michael na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.

Gadiel ameongeza ushindani wa namba tangu alipojiunga na klabu hiyo akitokea kwa watani wao wa jadi Yanga. Beki huyo ndiye alicheza mechi ya awali jijini Maputo, Msumbiji.

Tshabalala anatajwa ni mahiri wa kumiliki mpira, kutengeneza nafasi za kufunga kwa washambuliaji na pia hufunga mabao katika mechi za mashindano.

Gadiel ni beki hodari wa kudhibiti mashambulizi ya viungo wa pembeni wa timu pinzani na alifanya hivyo katika mechi dhidi ya UD Songo.

Akizungumza katika mazoezi, Kocha wa Simba Patrick Aussems alisema Tshabalala na Gadiel ni mabeki hodari, lakini atampanga atakayekuwa fiti kulingana na aina ya mchezo.

"Si rahisi kuzungumzia kiwango cha mchezaji mmoja mmoja kimsingi wote wapo vizuri nataka wacheze kitimu ili kufikia malengo ambayo tumejipangia na si kuangalia aina yake ya kucheza binafsi," alisema Aussems.

Gadiel alisema ushindani wa kuwania nafasi ya kucheza upo katika timu yoyote na hashangai kucheza nafasi moja na Tshabalala ambaye pia wapo timu ya Taifa ‘Taifa Stars’.

Beki wa zamani wa Yanga Anwari Awadh alisema Tshabalala ni hodari, lakini amekutana na ushindani wa kutosha kutoka kwa Gadiel ambaye naye ni hodari, hivyo kocha atakuwa na wigo mpana wa kuchagua beki wa kucheza kulingana na aina ya mechi.