Top Four EPL ngumu kwa Man United

Tuesday July 14 2020

 

MANCHESTER, ENGLAND. MANCHESTER United imeendelea kujiweka kwenye mazingira magumu baada ya kutoka sare mchezo wa jana Jumatatu wa Ligi Kuu, England waliocheza na Southampton.

Katika mchezo huo ambao Southampton ndio ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia Stuart Armstrong dakika ya 12, lakini Marcus Rashford aliisawazishia United dakika ya 20

Baadaye dakika ya 23 Anthony Martial akaipatia bao la pili United, lakini ndoto yao ikaja kuzimwa dakika za mwisho kwa bao la Michael Obafemi dakika ya 90.

Ikiwa United ingeshinda kwenye mchezo huo, ingekuwa imefikisha alama 62 na kushika nafasi ya tatu, lakini baada ya kupoteza imesalia kwenye nafasi ya tano na pointi 59.

Baada ya mchezo huo kocha wa kikosi cha United Ole Gunnar Solskjaer alizungumza kupitia BBC na kueleza kuwa wachezaji wake walicheza vizuri lakini kutoka sare hiyo ilikuwa ni hali ya mchezo.

"Kiakili tulikuwa na uwezo mkubwa, tumekutana na wapinzani wakali nafikiri hii ni moja ya changamoto tuliyokutana nayo kwa msimu huu," alisema.

Advertisement

"Ninaamini kwenye uwezo wa wachezaji wangu, ingawa ni kweli nimeumizwa na matokeo, lakini tunalichukua hili kama funzo kwetu, nina imani kuwa makosa haya hayatojirudia,"aliongeza.

Southampton yenyewe baada ya kutoka sare mechi hiyo imefikisha alama 45, baada ya kucheza mechi 35, ikiwa inashika nafasi ya 12.

Ligi hiyo itaendelea tena leo kwa mchezo mmoja kati ya Chelsea inayoshika nafasi ya tatu na pointi 60, baada kucheza mechi 35, dhidi ya Norwich City ambao tayari imeshashuka daraja, mchezo utapigwa majira ya 4:15 usiku.

Advertisement