Timu za England zadhihirisha wababe wa soka Ulaya

Muktasari:

Liverpool imetinga hatua hiyo ikiisukuma nje kibabe Barcelona, wakati Spurs nayo ilifanya hivyo hivyo kwa Ajax, huku Arsenal ikipita kirahisi mbele ya Valencia, wakati Chelsea ilihitaji ushindi wa penalti mbele ya Eintracht Frankfurt, mambo ni moto. Bato la Waingereza tupu kwenye fainali za Ulaya msimu huu.

LONDON, ENGLAND

UKWELI ndio huo, Big Six ya Ligi Kuu England ndio habari ya mjini kwa sasa. Unajua kwa nini, vigogo vinne katika orodha hiyo ya vigogo sita wa England, vimetinga fainali zote za Ulaya msimu huu, Ligi ya Mabingwa Ulaya na Europa League. Hii ni historia.

Liverpool itacheza na Tottenham Hotspur kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na Chelsea dhidi ya Arsenal itamaliza ubishi kwenye fainali ya Europa League.

Hii ya Ligi Kuu England kufunika Ulaya nzima ni mara ya kwanza haijawahi kutokea kwenye sehemu nyingine yoyote.

Liverpool imetinga hatua hiyo ikiisukuma nje kibabe Barcelona, wakati Spurs nayo ilifanya hivyo hivyo kwa Ajax, huku Arsenal ikipita kirahisi mbele ya Valencia, wakati Chelsea ilihitaji ushindi wa penalti mbele ya Eintracht Frankfurt, mambo ni moto. Bato la Waingereza tupu kwenye fainali za Ulaya msimu huu.

Fainali moja itapigwa Madrid, Hispania Juni Mosi, wakati nyingine itakuwa huko Baku, Azerbaijan Mei 29.

Fainali ya Europa League itakuwa ya London derby wakati ile ya Ligi ya Mabingwa Ulaya itakuwa ni Top Four derby.

Divock Origi na Georginio Wijnaldum walifanya maajabu kuifikisha Liverpool fainali, wakati Spurs wao mtu wao wa maajabu alikuwa Lucas Moura, huku kwa Arsenal ni wakali wawili, Alexandre Lacazette na Pierre-Emerick Aubameyang ndio waliofanya balaa, huku Chelsea mkwaju wa penalti ya mwisho ya Eden Hazard ulihitimisha idadi ya timu nne kwenye fainali mbili kubwa kabisa kwa michuano ya ngazi za klabu huko Ulaya msimu huu.

Kwa maana hiyo kwa vyovyote itakavyokuwa bingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya na yule wa Europa League wote watakuwa wametoka kwenye Ligi Kuu England, tena kwenye zile klabu sita za juu, Manchester City, Liverpool, Chelsea, Tottenham, Arsenal na Manchester United.

Liverpool itaingia uwanjani kusaka taji lake la sita la ubingwa huo wa Ulaya, wakati Spurs itataka kuweka alama zake kwa kubeba kwa mara yake ya kwanza.

Arsenal kwa upande wake itataka kubeba Europa League kwa mara ya kwanza huku ikitaka kukamatia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, wakati Chelsea inatambua ikibeba taji hilo itakuwa mara yake ya pili, pia taji hilo litakuwa na faida huko kwenye Ligi Kuu Ufaransa, timu itakayoshika nafasi ya tatu kwenye msimamo wao, itapata tiketi ya kuingia kwenye makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Kwa England, hii itakuwa mara yao ya kwanza kutoa bingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya tangu msimu wa 2011-12 wakati Chelsea ilipoichapa kwa penalti Bayern Munich, lakini ikiwa mara ya kwanza pia kwa upande wa Europa League tangu msimu wa 2016-17, Manchester United ilipoichapa Ajax kwenye fainali.

Ubabe huo wa England kwa msimu huu si tu umeleta utamu wa vita ya kusaka ubingwa kwenye Ligi Kuu England, bali pia umeonyesha kuwa ni bora kwa sasa kwa sababu mabingwa wote wawili wa michuano mikubwa ya Ulaya watakuwa wametokea katika ardhi hiyo ya Uingereza na kuzifunika timu za Hispania ambazo zilizoea kubeba mataji hayo.