Thiago dakika 45 tu kashika watu vibaya

LIVERPOOOL,ENGLAND. Fundi wa mpira, Thiago Alcantara amehitaji dakika 45 tu ndani ya kikosi kipya cha Liverpool kuandika historia Ligi Kuu England.

Mhispaniola huyo alitua Liverpool akitokea Bayern Munich kwa ada ya Pauni 20 milioni Ijumaa iliyopita na kucheza mechi ya kwanza siku mbili baadaye, wakati kikosi chake kilipogawa dozi huko Stamford Bridge kwa kuwachapa Chelsea 2-0.

Sadio Mane alifunga mabao yote kwenye kipindi cha pili huku kikosi hicho cha Frank Lampard kikishuhudia staa wake Andreas Christensen akitolewa kwa kadi nyekundu.

Hata hivyo, takwimu za Thiago, aliyetokea mechi kwenye mchezo huo akiingia kipindi cha pili, alionyesha kwamba ametua Ligi Kuu England kwa kazi moja tu, amekuja kuwashika.

Kwa muda ambao amekuwa ndani ya uwanja, Thiago alipiga pasi sahihi 75, hakuna mchezaji yeyote wa Chelsea aliyefikia idadi hiyo kwa dakika zote tisini.

Hiyo ni rekodi pia kwa mchezaji kupiga pasi nyingi sahihi kwa dakika 45 kwenye Ligi Kuu England tangu msimu wa 2003-04.

Baada ya kucheza na kushuhudia mabao saba, wakati Liverpool ilipokipiga na Leeds United katika mchezo wa kwanza, hivyo iliamua kufanya usajili wa Thiago na straika wa Wolves, Diogo Jota.

Baada ya data za Thiago kuwekwa kwenye mtandao wa Twitter, mashabiki wa Liverpool walipagawa na kuanza kutoa maoni yao.