Tetemeko Neymar azigonganisha Barca, Real

MADRID, HISPANIA.KAMA ulikuwa hujui, habari ni kwamba kwa sasa kuna vita kali kati ya Real Madrid na Barcelona, vita yao inasabishwa na Neymar wa PSG. Kila klabu inataka kumsajili ili itishe katika msimu huu.

Awali kulikuwa na tetesi kwamba klabu za England nazo zilikuwa zikimuhitaji mchezaji huyo, lakini kwa kuwa dirisha la usajili limefungwa kule Uingereza, kazi imebaki kati klabu nyingine za Ulaya ambapo wanasubiri mpaka Septemba mbili kukamilisha zoezi.

 Nyota huyo wa Brazil ameshaonyesha kila dalili kwamba hataki kuchezea PSG katika msimu huu na hiyo inailazimisha klabu hiyo ya Ufaransa imuuze. Taarifa kutoka katika klabu hiyo wiki iliyopita zilisema kuwa uongozi wa PSG umechoshwa na utovu wa nidhamu  wa mchezaji huyo.

Kutokana na suala hilo, swali linalobakia ni je, klabu gani inaweza kumnunua mchezaji huyo? Kwa sasa kila klabu inatumia mbinu zake kuhakikisha kwamba wanamnasa mchezaji huyo, Hata hivyo kibaya ni kuwa kuna ofa nyingine kutoka klabu za China ambazo zina pesa nyingi huku klabu za England zikiombea dili za Barca na Real Madrid zitibuke ili wamuwanie Januari.

Lakini habari kutoka kwa mtu wa karibu na Neymar zinasema kuwa mchezaji huyo hataki kwenda sehemu nyingine zaidi ya Hispania, sehemu ambayo anaona maisha yake yatanyooka.

Je anakwenda Real Madrid au Barca?

Kuhusu kutua Real Madrid

Kiongozi mkubwa wa Real Madrid, Florentino Perez amekuwa na tamaa ya kumsajili mchezaji huyo kwa muda mrefu, lakini suala la Neymar kuipenda zaidi Barca ni tatizo kwa klabu hiyo.

 Wachambuzi wa soka wanasema pamoja na yote hayo Neymar ana uwezekano mkubwa wa kutua Real Madrid kwa kuwa uongozi wa PSG hawapatani vizuri na Barcelona.

 Perez anafahamu kuwa Rais  wa PSG Nasser Al-Khelaifi anataka kumuuza mchezaji huyo Real, lakini hawezi kumtoa mpaka apate Pauni 200 milioni.

Ugumu uliopo ni kwamba   Real Madrid watatakiwa kuuza wachezaji watatu ili kupata kiasi hicho cha pesa, la sivyo itakuwa vigumu kumpata Neymar. Wachezaji ambao wanatakiwa kuuzwa fasta ni Gareth Bale, Mariano na  James Rodriguez.

Kuhusu kutua Barca

Kuna madai kwamba suala la Neymar kutua katika klabu hiyo ni gumu, lakini mchezaji huyo ana hamu kubwa ya kuchezea Barca. 

Mchezaji huyo ana shauku kubwa ya kuungana na Lionel Messi na Luis Suarez.

Wiki iliyopita ilifahamika kuwa Messi alipiga simu kwa Neymar akimtaka asisaini mkataba Real Madrid na badala yake ajiunge nao. Suala hilo limeongeza mafuta katika moto ambao tayari unawaka kichwani kwa mchezaji huyo wa Brazil na sasa yupo katika njia panda.

Imefahamika kuwa PSG wanaweza kukubali kumtoa Neymar kwenda Barca iwapo dili hilo pia litamuhusisha Philippe Coutinho na kiasi kikubwa cha pesa.

Lakini habari zinasema kuwa Barcelona wapo tayari kutoa wachezaji wawili lakini bila pesa yoyote, jambo linalofanya shughuli kuwa ngumu kwa PSG.

Lakini ukweli ni kwamba Real Madrid inamhitaji Neymar kuliko Barcelona inavyomuhitaji mchezaji huyo. Barca imejaza wachezaji wenye kiwango lakini wanang’ang’ani kumsajili Neymar kwa kuwa wameshamzoea na pia lengo ni kuwazibia wapinzani wao.